The House of Favourite Newspapers

HARMONIZE AMSHANGAA SARA AMPELEKA GETO LA UDONGO WATU WAPIGWA BUTWAA

STAA wa Bongo Fleva anayetumikia Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ (25), amefanya jambo ambalo vijana wengi wa kiume huwa wanaona soo kulifanya hivyo kumshangaza mchumba’ke, Sara, Risasi Mchanganyiko linakujuza. 

 

Ifahamike kuwa kila ifikapo Machi 15 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa (birthday) kwa Harmonize au Konde Boy.

 

KIJIJINI MAHUTA

Kwa mwaka huu, Harmonize aliamua kufanyia kumbukumbu hiyo nyumbani kwao alipotokea kijijini Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara na kuacha gumzo la aina yake kwani jambo kama hilo halijawahi kutokea kijijini hapo tangu kuanzishwa kwake.

 

TUJIUNGE NA SHUHUDA

Kwa mujibu wa shuhuda wa gazeti hili aliyeambatana na msafara wa Harmonize, jamaa huyo alimshangaza Sara ambaye ni raia wa nchini Italia kwa kumpeleka geto la udongo ambalo ndilo alilokulia kabla ya kutinga jijini Dar kutafuta maisha.

 

Kabla ya kumpeleka Sara kwenye geto hilo, Harmonize alimpeleka mchumba’ke huyo kwa mama yake katika nyumba ya kisasa aliyomjengea ambapo Sara alishiriki kazi na maisha ya kijijini kwa jumla.

WAPIGWA BUTWAA

Wakiwa kijijini hapo, Harmonize alitumia usafiri wa baiskeli kumpakiza Sara kisha kumzungusha kwa ndugu, jamaa na marafiki ambapo kila walikopita watu walipigwa na butwaa. Baada ya kutoka kwa mama yake, Harmonize alikatiza mitaa akiwa na Sara kisha alipita kwa shangazi yake kabla ya kutokea kwenye geto lake hilo la zamani.

 

REAL?

Baada ya kufika kwenye geto hilo na kuambiwa hapo ndipo jamaa huyo alipokuwa akiishi, Sara alimuuliza Harmonize kwa mshangao; “Real? Is this your home? (Kweli? Hapa ndipo nyumbani kwako?)”

 

YES…

Huku akionesha kujiamini na kutoona soo, Harmonize alimjibu mchumba’ke; “Yes…I was born here… (Ndiyo. Nimezaliwa hapa)”

 

CHOO CHA MAKUTI

Mbali na kumuonesha geto hilo lililochoka kuashiria kwamba ametoka kwenye familia duni, Harmonize alimuonesha Sara choo cha makuti alichokuwa akitumia.

 

TOFAUTI NA MASAKI

Katika hali kama hiyo, Sara alijikuta akishangazwa na mambo hayo, asiamini kile alichokuwa akikiona akilinganisha maisha ya Harmonize anayeishi kwenye mjengo wa kifahari maeneo ya Masaki jijini Dar. Hata hivyo, baada ya kumtembeza Sara kijijini hapo na kumuonesha maisha yake halisi kabla ya kuwa staa ndipo Harmonize akaingia kwenye kipengele cha shughuli yenyewe ya birthday.

KIPAJI KINGINE

Kabla ya kukata keki Harmonize alimuonesha Sara upande mwingine wa shilingi kuwa mbali na muziki ana kipaji kingine cha soka baada ya kutupia bao mbili kwenye timu yake ya kijijini iliyokuwa ikicheza na timu ya Nangwanda Sijaona.

 

Hata hivyo, pamoja na kufunga mabao hayo, lakini timu yake ililala kwa mabao 2-3. Baada ya hapo lilifuata zoezi la kukata keki ambapo Harmonize alianza kumlisha Sara kimahaba mbele ya wazazi wake kisha walifuata wazazi, ndugu, jamaa, marafiki na wanakijiji wa Mahuta waliofurika kwenye eneo la wazi kijijini hapo.

 

SOO BAAB’KUBWA

Baada ya kufanya zoezi hilo la kulisha keki, Harmonize aliangusha shoo baab’kubwa ya bure ambapo alipiga nyimbo zake zote na kukonga mioyo ya wanakijiji wenzake. Mbali na shoo hiyo ya kukata na shoka ya bure, wanakijiji hao walikula na kunywa vinywaji mbalimbali ikiwemo pombe ya mtama kisha wakakesha kwa muziki hadi majogoo.

 

WANAKIJIJI WAMFUNGUKIA

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wananchi wa Mahuta walikuwa na haya ya kusema; “Rajab ni kijana wetu, ni mtoto wa hapahapa Mahuta, kiukweli ametupa heshima kubwa mno ya kuja kushiriki nasi birthday yake,” alisema mmoja wa wananchi hao akiungwa mkono na wenzake.

 

“Mimi ninampongeza kwa kumleta wifi yetu (Sara) na kumuonesha maisha halisi aliyokulia. Wengine huwa hawapendi kuwapeleka wachumba wao nyumbani kwao kwa kuona aibu lakini Harmonize hakujali hilo,” alisema Mwanahawa. “Tangu kijiji hiki kimeanzishwa halijawahi kutokea tukio kama hili. Rajab (Harmonize) amefanya jambo kubwa mno lisilosahaulika,” alisema mzee Said.

HUYU HAPA HARMONIZE

Akizungumzia matukio yote yaliyojiri kijijini hapo, Harmonize alikuwa na haya ya kusema; “Nimezaliwa na kukulia hapa, mjini nilikwenda tu kutafuta maisha, lakini hapa Mahuta ndipo kwetu. “Nilitaka kuwapa feeling (hisia) za zamani nilivyokuwa ninaishi hapa kwa amani. Nilitaka kushiriki na ndugu, jamaa na marafiki wa zamani.

 

“Hii ni birthday yangu ya tatu tangu nimekuwa maarufu. Nyingine nilifanyia nje ya hapa, lakini sasa hivi birthday zangu zote nitafanyia hapa kijijini maana ninakuwa na amani sana. “Haya ndiyo maisha yangu halisi na hata ikitokea siku nikirudi hapa nitaishi kwa raha sana.”

 

TUJIKUMBUSHE

Harmonize alitinga jijini Dar mwaka 2009 alipohitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mkundi mkoani Mtwara. Baada ya kuwasili jijini Dar, Harmonize hakuwa na shughuli ya kufanya hivyo alijikita katika uuzaji wa chai maeneo ya Kariakoo.

 

Baadaye Harmonize alijihusisha na biashara ya nguo na vitu mbalimbali. Harmonize alianza harakati za muziki mwaka 2011, aliwahi rekodi studio, lakini nyimbo zake hazikuwa na ubora wa kupelekwa katika vituo vya redio hadi alipokutana na msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyemchukua kwenye Lebo ya Wasafi na ndiyo ukawa mwanzo wa kung’aa.

 

Kwa miaka minne aliyodumu kwenye Bongo Fleva ametikisa na nyimbo nyingi kama Aiyola, Birthday, Matatizo, Atarudi, Bado, Kwangwaru, Kainama na nyingine kibao.

Comments are closed.