Kartra

Harmonize Atinga Studio ya Mpenzi wa Rihanna

MSANII wa muziki wa Tanzania, Harmonize au Konde Boy Mjeshi anaendelea kutisha na kuthibitisha msemo wake wa Konde Boy for everybody; akimaanisha Konde Boy ni kwa ajili ya kila mtu.

 

Harmonize ambaye ni C.E.O wa Konde Gang Music yupo nchini Marekani akiendelea na ziara za shoo zake tangu Agosti 15, 2021 ambapo ziara hizo atazihitimisha Januari, 2022.

 

Mbali na kufanya shoo, akiwa nchini humo, Harmonize au Harmo amekuwa akiingia studio mbalimbali kubwakubwa kwa ajili ya kuandaa albam yake nyingine ambapo awali alifanya hivyo kule mjini Arizona, Marekani.

 

HARMONIZE NDANI YA STUDIO KUBWA

Hata hivyo, kubwa kuliko, ni baada ya kuzama kwa siku mbili mfululizo kwenye studio nyingine kubwa nchini Marekani ya A2F Studios iliyopo Miami, Florida ambapo alikwenda kufanya wimbo na msanii mkubwa mwenye asili ya Latin America baada ya kutangaza kuandaa albam nyingine huku ili ya High School ikiwa bado hajaizindua.

Baada ya kufanya wimbo huo, ukurasa rasmi wa A2F Studios umetoa waraka wa kumkubali Harmonize ile mbaya.

 

WAMUITA LEJENDI WA AFRIKA MASHARIKI

Wenyewe wameposti picha mbalimbali za Harmonize akirekodi wimbo ndani yake na kuandika; “Ni wasanii wachache waliowahi kufika hapa wenye uwezo mkubwa kama Harmonize alivyofanya!

“Tunashawishika kumuita lejendi wa Afrika Mashariki! Amezaliwa nchini Tanzania, Afrika!

 

“Staili ya muziki inayofanywa na Harmonize inamfanya kuwa msanii mwenye ushirikiano sana! Anafanya vizuri muziki wa Afro-Pop na Afro-Beat! Muziki wa Harmonize ni wa kimataifa na hii ndiyo maana tunamuita lejendi wa Afrika Mashariki…”

Ukiacha ukubwa wa studio kwa maana ya kuwa na vyombo vikubwa na vya kisasa, lakini kutumiwa kwake na mastaa wakubwa duniani.

 

STUDIO INATUMIWA NA ASAP ROCKY

Studio hiyo ndiyo ambayo inatumiwa kwa sasa na mpenzi wa mwanamuziki wa kiwango cha dunia, Robyn Rihanna Fenty ambaye ni rapa mkubwa duniani aitwaye Asap Rocky.

 

Hata hivyo, Harmonize hakumkuta Asap Rocky, lakini alipata fursa ya kutumia vifaa ambavyo hutumiwa na staa huyo wakati akirekodi nyimbo zake.

Mastaa wengine wakubwa ambao waliwahi kutumia au hutumia studio hiyo pamoja na Rick Ross, Stef London ambaye ni mpenzi wa Burna Boy na wengine.

 

SASA INA FAIDA GANI?

Mtu anaweza akajiuliza, sasa hii ina faida gani kwa Harmonize kurekodi wimbo kwenye studio kubwa kama hiyo ilihali ni studio kama studio nyingine za Bongo?

Lakini jibu ni rahisi tu; kuna usemi wa Kiswahili usemao; ‘Kaa karibu na uaridi unukie!’

 

Mbali na hilo, pia inamsaidia kujiongezea wasifu wake kwamba ameshafanya kazi na studio kama hiyo kubwa duniani hivyo itamfanya naye kuonekana mkubwa zaidi hivyo kumuongezea uaminifu.

 

Pia katika kurasa zao studio hiyo imeonesha kumkubali Harmonize na ni kurasa ambazo zimefuatwa (ku-follow) na mastaa wengi wakubwa duniani hivyo haitakuwa kazi kubwa kwa Harmonize kujitambulisha kwao kwani wameshamuona kwenye kurasa hizo.

 

Kwenye uwaniaji wa tuzo kubwa duniani kama BET au Grammy, pia huangalia wimbo unaoshindanishwa umetengenezwa katika studio gani na kwa prodyuza gani; hii ndiyo maana Diamond amejishikiza kwa Producer Swizz Beatz wa Marekani au Burna Boy alivyomfanya P Didy kuwa prodyuza wake.

 

Mbali na Diamond, kwa sasa Harmonize anafanya vizuri na kupeperusha kimataifa bendera ya muziki wa Bongo Fleva.

STORI: IJUMAA WIKIENDA, DAR


Toa comment