The House of Favourite Newspapers

Harmorapa Kiki Zimetosha, Fanya Kazi!

0

NA GABRIEL NG’OSHA| RISASI JUMATANO | BARUA NZITO

NIMSHUKURU Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuweza kuzungumza na waja wake kupitia karama ambayo amenijalia.

Barua yangu ya leo, imfikie popote alipo mdogo wangu, Athumani Omary ‘Harmorapa’ ambaye juzikati amezalisha a.k.a nyingine ya ‘Strong Woman’

Nimekufuatilia kwa umakini na kwa muda mrefu sana mdogo wangu, muda umefika sina budi kutoa yangu ya moyoni ili kama yatakuwa na umuhimu kwako, basi uyafanyie kazi.

Pongezi kwa sababu sehemu kubwa ya mashabiki wa Muziki wa Bongo Fleva wanakufahamu kupitia majibu, vitendo na mambo yako ya kila siku. Na hata ‘viewers’ unao wa kutosha kwenye mitandao yako ya kijamii ikiwemo Instagram. Lakini kumbuka kuwa kuna kipindi kiki zitakwisha au zitazoeleka kwa mashabiki wako, unadhani ‘utasavaivu’ vipi kwenye gemu?

Harmorapa, mtu akikuangalia anatamani kuendelea kukuangalia na kukusikiliza zaidi na zaidi kwa namna unavyojibu, kujieleza na hata vitendo vyako.

Ninachoamini una nyota ya kupendwa, una karama ya kufuatiliwa, siku zote Mungu hugawa karama au vipaji vya aina mbalimbali kwa watu wake. Wenye kung’amua huvitumia vyema na kufanikiwa wasiyotambua huishia kufa wakiwa maskini.

Wewe ni miongoni mwa wasanii wachache ambao wameibuka kwenye gemu ya Muziki wa Bongo Fleva na kujikusanyia mashabiki kibao bila nguvu nyingi, bila ya kuwa na kazi au wimbo wa maana kwenye gemu ila tu kwa sababu una nyota ya kupendwa.

Hivi karibuni ‘umeharibu’ mitandaoni kwa kunukuliwa ukijiita kuwa wewe ni ‘Strong Woman’, sijajua ulikuwa umedhamiria kweli kujibu ulivyojibu, menejimenti yako ilikupangia ujibu hivyo au ulijibu kwa kutokuelewa maana ya kile ulichojibu?

Pamoja na kujibu swali lako kwa kuivaa jinsia ya kike wakati wewe ni wa kiume lakini bado sentensi yako ilitengeneza vichwa vya habari mitandaoni. Kama ni kweli ulisema kwa sababu ya kiki, basi kiki zingine mdogo wangu si nzuri, kiki zingine zinaweza kukushusha na kuwafanya mashabiki wako waende mbali zaidi kifikra.

Kujiita ‘Strong Woman’ wakati wewe ni mwanaume unakosea sana hata kama menejimenti yako inaongozwa na mwanamke, lazima uangalie vitu vya kujibu kwa kuheshimu jinsia yako.

Kwa sentensi na matendo yako kuna siku unaweza kufanya jambo kubwa na baya sana kwenye tasnia likaharibu taswira na msingi ulioujenga kwenye sanaa.

Na kama kweli kiki ambazo umekuwa ukizifanya ni za kuchorwa kama wengine wadhaniavyo, basi si zote za kukubaliana nazo, zingine jaribu kuzungumza na uongozi wako kuwa si sawa.

Kama alivyoimba msanii Darasa, ACHA MANENO WEKA MUZIKI, mdogo wangu Harmorapa KIKI ZIMETOSHA, SASA FANYA KAZI.

Uongozi wako ni mzuri kwa sababu kwa muda mfupi umekufanya ufahamike vyema na juzikati pale Dar Live kwenye shoo ya Pasaka ukafanya poa kwa kujaza ukumbi ‘ndi’.

Umeshakubalika, unapendwa lakini kumbuka kuwa Watanzania na mashabiki wako wanataka muziki mzuri zaidi, ondoa fikrani mwao maneno kuwa huna kipaji cha muziki zaidi ya kiki. Hata kama kweli huna kipaji, lakini bado una nafasi kubwa ya kujifunza na kufanya vizuri. Kwani kwa sasa pamoja na mbwembwe nyingi una ngoma nyingi kali zaidi ya Kiboko ya Mabishoo uliyomshirikisha Juma Nature.

Upepo wako unanikumbusha Mshindi wa Shindano la Bongo Star Search ‘BSS’ mwaka 2007, Jumanne Idd katika shindano lile alionekana kung’ara na kupendwa sana na watu na mwisho aliibuka mshindi lakini maisha nje ya BSS alishindwa. Je, unaweza kuishi maisha nje ya kiki!?

By Gabriel Ng’osha

Leave A Reply