The House of Favourite Newspapers

Harusi ya Kifahari, Baadaye Mnaachana, Nini Kinasababisha?

NI wiki nyingine ninapoku­karibisha msomaji wan­gu kwa moyo mkunjufu kwenye uwanja huu mzuri, leo tukiwa tunaendelea na sehemu ya tatu na ya mwisho ya mada tuliyoanza kuijadili wiki mbili zi­lizopita.

Mada iliyopo mezani, ni kwa nini baadhi ya wanandoa siku hizi wanafunga ndoa za kifahari sana lakini muda mfupi baadaye ndoa zao zinavurugika? Naen­delea kukushukuru msomaji wangu uliyeendelea kunitumia ujumbe wako kwa njia ya meseji na WhatsApp.

Kama tulivyoona wiki iliyopita, kushindwana kitabia, kushindwa kujishusha inapotokea mme­korofishana ndani ya nyumba hata kwa ugomvi mdogo, ku­toelewa maana ya ndoa na kuoa au kuolewa kwa ajili ya kuon­doa gundu, ni miongoni mwa sababu zinazofanya ndoa nyingi zisidumu licha ya kufungwa kwa mbwembwe nyingi.

Kama nilivyosema wiki iliyopita, makosa ambayo watu wengi wa­nayafanya siku hizi, ni kukubali kuoa au kuolewa bila kuwa na uhakika kama huyo unayetaka kuanzisha naye maisha ya famil­ia anakupenda au la.

Wengine hujikuta wakilazimisha kuingia kwenye ndoa na mtu fu­lani si kwa sababu anampenda bali kwa sababu ana kitu fulani au umri umeenda na watu wote wanamuuliza ataoa au ataolewa nini. Hili ni kosa kubwa ambalo kama kweli msomaji wangu unataka kudumu kwenye ndoa, unapaswa kuwa nalo makini.

Unapaswa kuwa na uhakika kama mtu unayetaka kuingia naye kwenye ndoa, anakupenda kwa dhati na yupo tayari kusi­mama na wewe katika hali zote, shida na raha. Njia pekee am­bayo itakufanya uwe na uhakika kama huyo unayetaka kuingia naye kwenye ndoa anakupenda au laa, ni kujipa muda.

Tofauti na zamani ambapo uchumba ulikuwa unatakiwa kudumu kwa kipindi cha an­galau mwaka mmoja mpaka mi­aka miwili kabla ya kuoana, siku hizi watu wanakutana leo, ke­sho wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi na miezi michache baadaye, wanafunga ndoa. Wengine wanalazimika kufunga ndoa kwa sababu tu wamesha­peana mimba kwa hiyo wanata­ka kuficha aibu lakini si kwamba wanapendana.

Si rahisi kwa watu wa namna hii kuwa wamesomana kiunda­ni. Hata kama mtu hakupendi bali anataka kuwa na wewe kwa sababu zake binafsi, unapo­jipa muda wa kumchungu­za, ni rahisi sana kuugun­dua ukweli wa moyo wake.

Sisemi kwamba watu wakae kwa muda wa mia­ka kadhaa kwenye uchum­ba ndiyo waoane, hapana! Namaanisha ni vizuri kila mmoja akamfahamu vyema mwenzake, ili hata mkiingia kwenye ndoa, kunakuwa hakuna kitu kipya.

Kwa wale wanaokurupuka na kufanya mambo harakahara­ka ilimradi tu na yeye aonekane amefunga ndoa, nawaambia kwamba watu wengi wanao uwezo mkubwa wa kuficha uhalisia wao wanapohitaji kitu fulani kitimie. Mwanamke anaweza kukuektia kwamba yeye ni mpole sana, amelelewa katika maadili mazuri, ana busara na kila sifa nzuri, kwa sababu tu anataka umuoe.

Ukifanya papara ukaamini zile sifa za nje, utajikuta umemuoa ila ak­ishaingia ndani sasa, hapo ndi­po anapoanza kuonesha rangi yake halisi. Watu wengi huwa na uw­ezo wa kuficha tabia zao halisi kwa muda wa miezi michache lakini mnapozidi kukaa pamoja, zile tabia halisi zitaanza kujionesha kwa hiyo hata ukiamua kumuoa, utakuwa unamuoa mtu ambaye unazi­jua tabia zake halisi kwa hiyo hawezi kukusumbua.

Hali kadhalika kwa wa­naume, wapo mafundi wa kuigiza aina fulani ya maisha wakati ukweli ni kwamba wapo tofauti kabisa. Nao pia, kitu pe­kee kinachoweza kuwa­fanya waoneshe tabia zao halisi ni muda. Leo ataigiza tabia am­bayo siyo yake, kesho pia lakini miezi kad­haa mbele, ataone­sha tabia yake halisi na hapo ndipo utaka­pompima na kuamua kama anakufaa au laah!

Ukimuoa au ukiolewa na mtu ambaye unamfahamu tabia zake halisi, utakuwa na nafasi nzuri ya kudumu naye kwa sababu hata kama unayajua mapun­gufu yake lakini bado umeamua kuishi naye, hayo ndiyo yanayoit­wa mapenzi ya dhati. Mambo mengine mnakuwa mnaen­delea kujifunza ndani ya ndoa, kadiri umri una­vyosogea.

Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Comments are closed.