HATA KAMA HUMWAMINI, MPE UHURU WAKE

NI Ijumaa nyingine tunapokutana, ni wajibu wetu kumshukuru Mungu kwa kutufanya tuione siku ya leo. Leo ningependa kuzungumza na wewe msomaji wangu mwenye tabia ya kumbana mwenzi wako mpaka anahisi kero. Wivu ndiyo mapenzi, hilo halina shaka lakini kila kitu kinapaswa kuwa na kiasi. 

 

Kuna watu wanaamini kwamba eti mpenzi wako, awe mwanaume au mwanamke, ukimbana sana ndiyo hawezi kukusaliti. Kwamba muda wote lazima uwe unajua yuko wapi, anafanya nini na lazima atoe ushahidi wa kila ana­chokifanya kwako. Huko ni kujidanganya, mtu mwenye tabia ya usaliti, hata ufanye nini bado atakusaliti tu. Unachopaswa kukijua, ni kwamba hakuna kitu muhimu maishani kama kumpa uhuru mwenzi wako.

 

Najua inaweza kuwa ngumu kwako kuelewa ninachokisema kama umezoea ‘kukaba mpaka penalti’. Ni vizuri kufahamu nyendo za mwenzi wako na kuwa na taarifa juu ya kila anachoki­fanya lakini narudia kusisitiza, ni muhimu kumpa uhuru wa kutosha.

 

Kwa kawaida, kila mtu kuna wakati huwa anatamani uhuru wa kufanya mambo yake binafsi, hii haijalishi mtu yupo ndani ya ndoa au laah! Upo muda ana­tamani kukutana na rafiki zake waliosoma pamoja au waliokua pamoja, upo muda anahitaji kuji­kumbusha enzi zake na mambo kama hayo. Sasa kama wewe unatanguliza wivu kwa kila anachokifanya, hutaweza kumpa uhuru wake.

 

Utambana kwa kila namna, hata atakapokuomba ruhusa lazima utamnyima, matokeo yake, moyo wake utaingiwa na sononeko na mambo yakiendelea hivyo, taratibu ataanza kujenga chuki na wewe.

Mkiendelea hivyo kwa muda, mtajikuta ufa mkubwa umeanza kujengeka kati yenu. Mwache huru, na kama wasiwasi wako ni kwamba atakusaliti, hata ukim­bana bado anaweza kukusaliti pia. Tena muda mwingine, usisubiri akuombe, kuonesha kwamba unamjali mruhusu aende kutembea sehemu yoyote anayoipenda akiwa peke yake au na rafiki zake, ikiwezekana mpe hata fedha za matumizi kwenye matembezi yake.

 

Kama mna watoto, unaweza kuamua kubaki na watoto ili apate ule uhuru wa kuwa mwenyewe kwa sababu akiwa na watoto hawezi kuwa huru kwa asilimia 100. Wazee wa zamani, walikuwa na kawaida kwamba, akikaa na mkewe kwa muda fulani, anam­ruhusu aende nyumbani kwao kusalimia.

 

Anaweza kukaa kwa siku kadhaa na akiwa huko hamfuatilii kwa jambo lolote zaidi ya kuhakikisha yupo salama. Wapo ambao mpaka sasa huwa wanafanya hivyo na wataalamu wa saikolojia ya mapenzi, wa­naielezea mbinu hiyo kama njia nzuri ya kuimarisha hisia za mapenzi kati yako na umpendaye.

Mwanamke wa aina hiyo, akipata uhuru wa kwenda kwao ambao tafsiri yake ni uhuru wa kuwa mwenyewe, akirejea huwa na hisia mpya kabisa za mapenzi na hata kama kulikuwa na visasi na vinyongo ndani ya moyo wake kwa sababu ya jambo ambalo mmewahi kukwazana, vyote huisha na kuanzisha ukurasa mpya kabisa.

 

Sasa ukiangalia kwa kina, hiyo haina tofauti na uhuru ninaouzungumzia hapa, kama hana sehemu ya kwenda akakaa siku kadhaa, basi msaidie kwa kuwa unampa uhuru wa kuwa mwenyewe mara kwa mara. Alikupenda akiwa mwenyewe na ili aendelee kukupenda, lazima uwe unampa muda wa kuwa mwenyewe. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Toa comment