The House of Favourite Newspapers

HATARI KUBWA… DAKTARI AMFANYIA KITU MBAYA MGONJWA

DAR ES SALAAM: Kabla hujafa, hujaumbika! Anna Majaliwa (35), Mkazi wa Tabata-Mawezi jijini Dar amezaliwa salama lakini ukubwani amejikuta akipata tatizo la afya linalodaiwa kusababishwa na daktari kumpa dawa ambazo si sahihi.  

 

Anna ambaye sasa amekuwa siyo mtu mwenye furaha tena kwa muda wa miezi 17 kutokana na mateso anayoyapata kitandani, mwili wake umepooza baada ya kupatiwa dawa aina ya ‘flagili’ na ‘powercef’ alizopewa baada ya kusafishwa tumbo kutokana na mimba ya miezi mitatu kuharibika.

 

Anna ambaye muda wote kwake ni maumivu makali, anasema yupo kwenye ulimwengu mwingine hivi sasa kwa sababu hasikii njaa, hasikii maumivu, hawezi kusikia utamu au uchungu wa chakula na mbaya zaidi hapati usingizi hata kidogo. Gazeti hili lilifanya mazungumzo naye nyumbani kwao licha ya kukosa nguvu ya kuzungumza kwa muda mrefu na hata kama utaongea naye unahitaji muda wa kumsikiliza kutokana na kushindwa kukuelewa kutokana na hali yake.

 

Akizungumzia kilichomsibu Anna alisema Mei, mwaka jana alipata tatizo la mimba kuharibika, akaenda katika hospitali moja jijini Dar (jina tunahifadhi kwa kuwa daktari mhusika hajapatikana) na akapimwa, hivyo kuambiwa ana kansa ya tumbo na ini.

 

“Nilipoambiwa hivyo nilichoka, alinipa dawa za kunywa na za kuchoma, lakini kila nikichomwa sindano nguvu zilikuwa zikiniishia. “Kwa kuwa nilikuwa kwa mama na ndiye aliyekuwa akinipeleka kuchoma sindano akanishauri niache kuchoma, nirudi tena kwa daktari.

“Nilifanya hivyo, nilirudi kwa yule daktari, nikamueleza tatizo akaniambia kwa kuwa tatizo langu la kwanza lilianzia kwenye mimba kutoka, nikamuone daktari wa magonjwa ya wanawake pale pale hospitali. “Nilipomuona daktari nilimueleza kilichonikumba naye baada ya kuangalia vipimo akaniuliza naumwa nini? Nilimwambia kwenye vyeti itakuwa vimeandikwa.

 

“Nilimwambia eti nina kansa ya tumbo na ini, alishangaa, akaniandikia vipimo upya, nilipopimwa akasema siumwi magonjwa hayo. Nilipigwa na butwaa. “Baada ya hapo nilimweleza kwamba sasa hivi sisikii njaa, wala mtu akinifinya sisikii maumivu, sipati njaa wala usingizi ndipo akanishauri niende Muhimbili kwenye kitengo cha mishipa na fahamu.

 

“Muhimbili nilionana na wataalamu wakanipima wakasema sina kansa lakini mishipa yangu ya fahamu imeathirika, hivyo nilipewa dawa ambazo nimezitumia hadi leo, hazijanisaidia,” alisema Anna. Alisema akiwa Muhimbili alipimwa pia akili, Ukimwi na kuonana na watu wa ushauri nasaha lakini matatizo hayo ikaonekana hana.

 

Hali halisi ya maisha yake Anna anasema maisha yake si mazuri kwa sababu hana nafasi ya kufanya kazi yoyote ile ya kumuigizia kipato kwa sasa. Anaishi na mzazi wake ambaye pia ni mjane ambapo wakati mwingine anakosa hata fedha ya matumizi katika maisha ya kila siku kutokana na hali duni ya kiuchumi.

Alisema anamuomba msaada Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aweze kutibiwa tatizo lake ambalo limemfanya awe katika ulimwengu mwingine kwani hasikii njaa, maumivu, usingizi, na mbaya zaidi hata kwenda haja zote mbili ni kazi kubwa, anaweza kukaa hata zaidi ya siku tano bila kujisaidia.

 

“Nilishaandika barua ya kuomba msaada wa matibabu wizarani lakini hadi leo sijapata msaada wowote… ninachoomba ni tiba, sitaki kesi nataka afya yangu irejee kama zamani,” alisema Anna huku akibubujikwa na machozi. Yeyote aliyeguswa na habari hii na kutaka kumsaidia chochote Anna anaweza kuwasiliana naye kwa namba 0655 42 51 00.

STORI: ZAINA MALOGO, Risasi Jumamosi

Comments are closed.