The House of Favourite Newspapers

Hatari Sana! Vitovu vya Vichanga, Maji ya Maiti Vyauzwa kwa Siri Kubwa, Dar

mtototooo

Na Mwandishi wetu | Gazeti la Uwazi Toleo la Desemba 20, 2016

DAR ES SALAAM: Hatari! Kuna msemo kwamba, kila mtu anakula anapofanyia kazi, lakini ulaji mwingine ni wa hatari sana! Mfano huu wa madai kwamba, baadhi (msisitizo baadhi) ya watumishi kwenye baadhi ya hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti (mochwari) jijini hapa wamekuwa wakiuza vitovu vya watoto wachanga na maji yaliyooshea maiti, Uwazi limechimba.

Kwa mujibu wa chanzo, biashara hiyo hufanyika kwa siri kubwa kwani ni kinyume na utaratibu wa utendaji kazi wa hospitali husika.

TWENDE NA CHANZO 

Kwa maelezo zaidi, chanzo kilisema: “Hii biashara jamani imeshamiri sana. Ila sasa kuizima itakuwa ngumu kwa sababu moja kuu, ni siri sana. Mnunuaji na muuzaji wanajuana.”

pesa-na-maji-ya-kuoshea-maiti-2

Maji ya maiti yakiuzwa.

BEI YAKE

“Kuhusu bei ni kama makubaliano. Lakini iko hivi, maji yaliyooshea maiti ukiyataka kwenye chupa ya lita moja na nusu ni shilingi laki moja (100,000), ila kama utalia sana, wanashusha hadi shilingi elfu tisini (90,000).

“Kitovu kimoja cha kichanga ni shilingi elfu themanini (80,000), kama utalia sana mwisho ni elfu sabini (70,000).”

WATEJA WAKUBWA

“Katika kufuatilia, imegundulika kuwa, wateja wakubwa sana ni waganga wa kienyeji. Hapa naomba nieleweke. Namaanisha waganga wa kienyeji na si waganga wa tiba asilia au wa mitishamba. Yaani wale wanaotibu zaidi kwa kutumia tunguli huku wakiwa wamevaa shanga na mikia ya wanyama.

“Lakini mbali na wateja wakubwa kuwa waganga, pia wapo watu ambao si waganga  bali wamepewa masharti na waganga. Kuna watu wakienda kwa waganga kuaguliwa, wanaambiwa ili tatizo liishe, lazima apate maji ya maiti au kitovu cha mtoto mchanga.

dokta-maneno-ambaDkt. Maneno Temba

KAZI YAKE KUBWA

“Kazi kubwa ya hivi vitu ni tiba, kuna waganga wanatumia maji ya maiti kuagulia watu. Mfano wale wenye kesi kubwa, magonjwa sugu, kuwazindua watu wanaoonekana kama mazezeta na pia hutumia kukinga mashamba au biashara isikutwe na mikono ya wabaya.

“Lakini vitovu vya watoto pia vinatumika kuzindikia nyumba, kuagulia utasa wa wanawake wanaosumbuka na kuzaa na kuzuia wachawi kuingia ndani ya biashara au nyumba zile za kifahari.

“Pia vitovu hutumiwa na waganga katika kuwaumiza wanaume wanaotembea na wake za watu. Nasikia kuna dawa, hasa mkoani Tanga, maeneo ya Handeni inajulikana kama usinga, mwanaume akitembea na mke wa mtu anakufa mara moja. Sasa nasikia katika dawa hiyo, kitovu cha mtoto kipo.”

SEHEMU HUSIKA

“Kama utataka maji yaliyooshea maiti utauziwa na watu wanaofanya kazi mochwari, ingawa si kila mfanyakazi wa mochwari anajihusisha na biashara hiyo. Ila wapo. Na kama utataka kitovu cha mtoto, wauzaji wakuu ni baadhi ya wauguzi wasio waaminifu, ingawa pia si wote,” kilisema chanzo.

dk-victoria-ludovickDkt. Victoria Ludovick.

MADAI YAFANYIWA KAZI

Ili kupata ukweli au uongo wa madai hayo, Uwazi kwa kutumia waandishi wake wa kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ wiki iliyopita lilifanya kazi ya kuzunguka kwenye hospitali ndogo na kubwa za jijini Dar.

Baadhi ya hospitali (majina tunayo), wauguzi wake walikuwa tayari kufanya biashara hiyo licha ya kwamba, walionesha tahadhari kubwa wakati wa ‘kubageini’ bei.

OFM haikufikia hatua ya kununua kwa kuwaambia wahusika itarudi tena, lakini ukweli ukawa umejulikana kwamba, biashara hiyo ipo.

Katika hospitali moja, OFM ilikwenda mpaka mochwari na kuzungumza kwa siri na mfanyakazi mmoja wa chumba hicho ambaye alikubali kuuza maji yaliyooshea maiti kwa gharama ya shilingi 90,000 baada ya kupunguza bei.

Mtu wa mochwari: “Sikia kijana. Bei ya mwisho kabisa ambayo siwezi kupunguza zaidi ya hapo kwa maji ya maiti ni shilingi elfu tisini. Kwa hiyo kama unayo lete pesa nikupe mzigo.”

OFM: “Sawa, lakini anayehitaji ni kaka yangu, yeye ana kesi, mganga kamwambia ampelekee maji ya maiti. Ngoja nimpigie ili ikibidi anitumie pesa kwa mtandao wa simu.”

OFM alikwenda kusimama pembeni na kuwasiliana na makao makuu ya kitengo hicho na kupewa maagizo kwamba, aongee na mtu huyo kuwa biashara ifanyike nje ya mochwari ili OFM iweze kupiga picha za kificho (kama machale yalimcheza), mhudumu huyo hakuwa tayari.

OFM LASAKA MITAZAMO

Ili kupata mawazo mbalimbali na angalizo pia, OFM iliwapigia simu baadhi ya watoa huduma ya utabibu jijini Dar es Salaam, lakini aliyeweza kupatikana mara moja ni tabibu Maneno Tamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania.

Yeye alianza kwa kuambiwa kuhusu kuwepo kwa biashara hiyo ambapo alionesha kushtuka sana na kusema:

“Kwanza sijui kama kiungo cha binadamu kinaweza kutumika kutibu. Lakini ni hatari sana. Mimi kwa upande wangu kwanza sitibu kwa kutumia viungo vya binadamu wala kitu chochote kinachotokana na mwili wa binadamu.

“Ila wateja wa hivyo vitu sijui watakuwa akina nani? Maana bwana kuna waganga, kuna wanga, kuna wachawi na kuna wajanja. Sasa sijui katika makundi hayo, kundi gani linaweza kununua vitu hivyo lakini huenda lipo.”

OFM NA WAGANGA WAKUU WA MANISPAA

Pia, OFM liliwatafuta waganga wa hospitali mbalimbali za jijini Dar. Awali, lilimtafuta Mganga Mkuu wa Jiji, Judith Kahama lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) na kuambiwa kuhusu madai hayo, hakujibu.

OFM lilifanikiwa kumpata Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Victorina Ludovick ambapo katika mazungumzo yake ana kwa ana na OFM kuhusu kuwepo kwa madai hayo, alisema:

“Hilo suala sijawahi kulisikia. Ila kama nyie mnaweza kufanya uchunguzi, andikeni barua kwa Afisa Habari wa Jiji iende kwa Mkurugenzi wa Manispaa, akitoa ruhusa mfanye mnaweza kutusaidia pia sisi.”

ANGALIZO

Muuguzi mmoja kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alisema kuwa ni vizuri wanawake wanapokwenda kujifungua kuhakikisha hakuna ujanjaujanja juu ya uhifadhi wa vitovu vya watoto wao.

“Ni kawaida kwa mzazi kupewa kitovu cha kichanga chake kabla hajatoka hospitali ili akakifukie mwenyewe anakotaka. Unajua mambo ya kitovu yana mila na desturi, nasi tunaheshimu hilo. Sasa hao wenzetu wanaouza vitovu wanavipata wapi? Ina maana huwa hawawapi wenyewe? Mimi nawaomba akina mama wawe makini,” alisema muuguzi huyo.

OFM, juzi ilimpigia simu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla ili kusikia kutoka kwake, lakini simu yake haikuwa hewani. Hata alipopigiwa waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, naye simu yake haikuwa hewani.

Irene Uwoya Afanya Kufuru Birthday Yake, Amkumbuka Samwel Sitta Aliyezaliwa Naye Des. 29

Comments are closed.