The House of Favourite Newspapers

HATARI YA KUCHOKONOA KWA PAMBA MASKIO YA WATOTO

BADO wataalamu wa afya tunasisitiza kwamba, haitakiwi kutumia pamba kusafisha masikio ya mtoto au mtu mzima. 

 

Zile pamba ambazo hutumiwa mara kwa mara na watu kutolea uchafu masikioni si salama kwa kazi hiyo. Haitakiwi kabisa kuingiza chochote ndani ya sikio. Watu wengi duniani wanatumia vijiti vilivyo na fundo la pamba kwenye ncha (cotton swap) kutolea uchafu masikioni mwa watoto au wao wenyewe, ambavyo vingi vinauzwa madukani.

 

Aidha wapo wengi pia ambao hutumia vijiti vya vibiriti kwa ajili ya kutoa uchafu ama nta ndani ya masikio ya watoto (au watu wazima). Kwa nini watu wasitumie njia hii maarufu ambayo imekuwa ikitumika miaka na miaka kutolea uchafu ndani ya masikio yao?

ATHARI ZA PAMBA ZA MASIKIONI

Pamba, njiti za vibiriti, funguo, ama vijiti vingine ambavyo huwa tunavitumia kutoa uchafu kwenye masikio ya watoto au kwa wazazi, vinaweza kukatika ama kusababisha kuchunika kwa mifereji ya masikio, kutoboa ngoma za sikio na kutengua mifupa iliyoko ndani ya sikio la watoto.

 

Athari yoyote kati ya hizo inaweza ikasababisha kupungua kwa uwezo wa kusikia, kizunguzungu, milio au dalili zingine za maumivu ya sikio. Badala ya watu kuendelea kutumia vitu hivyo, ni bora wakaiacha asili ifanye kazi yake.

 

Yaani kuacha kuutoa uchafu ndani ya sikio la mtoto hata mtu mzima kwa sababu utatoka wenyewe kulingana na asili ya ufanyaji kazi wa mwili. Miili yetu huzalisha nta masikioni mwetu ili kuyafanya masikio kuwa laini, safi na yaliyo na ulinzi wa kutosha. Kwamba uchafu, vumbi na kitu kingine chochote ambacho kinaweza kuingia ndani ya sikio basi kikanase ama kikakwame kwenye nta hiyo.

Kwamba nta hiyo ndani ya sikio, ni maalumu kwa ajili ya kuhifadhi chembechembe zozote ili zisipenye ndani zaidi kwenye mifereji ya sikio la mtoto. Kwa watoto au watu wazima walio na tatizo la kujaa kwa nta ndani ya sikio, kutumia pamba ama njiti za vibiriti, kunaweza kusababisha nta isukumwe ndani zaidi ya mfereji wa sikio na kuiharibu ngoma ya sikio.

 

Ikiwa mtoto au mtu mzima ana tatizo la kujaa kwa nta, anaweza kwenda kwa daktari iwapo watakuwa na tatizo la kutosikia kama dalili. Kwani tatizo la aina hii hutatuliwa na daktari bingwa na sio kuchokonoa sikio kwa pamba. Ni desturi kwa watu kutaka kulifanyia usafi sana sikio la watoto au hata watu wazima, lakini kuondoa ile nta ya ziada inapokuwa imetoka nje ya sikio, kunatosha kabisa.

USHAURI MUHIMU

Matone ya maji yanashauriwa kuwa yanaweza kuwa na faida ya kulainisha nta ndani ya sikio, unatia ndani ya sikio na kuyatoa kwa kuinamisha kichwa. Ukiwa na tatizo la kujaa kwa nta ndani ya sikio, ni vizuri kumuona daktari badala ya kuchokonoa kwa pamba au kijiti.

 

Siyo kitu kipya kuwa na nta ndani ya sikio la mwanao au lako, kwani kila mtu huwa nazo. Inakuwa ni tatizo tu kama zitazidi. Mtoto au mtu mzima anapokuwa na dalili kama vile za maumivu, kutokwa maji, damu, usaha au kupoteza usikivu, anapaswa kujua kuwa kuna tatizo na katika sikio lako, hivyo muone mtaalamu.

 

Kama mwanao au wewe una dalili hizo, mara moja kamuone daktari, ila nisisitize kwamba, kuna watu ambao hufungamanisha dalili hizo na kujaa kwa nta sikioni wakati siyo kweli. Kwa wazee, tatizo la kukosa usikivu linakuwa ni la kawaida kabisa.

Comments are closed.