The House of Favourite Newspapers

Hatari Ya Kula Nyama, Vyakula Vya Kopo

CHAKULA kinapoliwa na binadamu huwa na safari ndefu na husafiri kwa zaidi ya saa 13 hadi 72 kulingana aina ya kile kilicholiwa.

 

Utumbo mdogo au mwembamba una urefu mara nne ya urefu wa wastani wa mtu mzima. Unakadiriwa kuwa na urefu wa futi 18 hadi 23.

 

Tumbo huweza kuhifadhi vyote unavyokula kila siku huku vingine vikikaa tumboni kwa hata saa 72 bila kuyeyuka.Utumbo mwembamba umeungana na utumbo mnene. Huu una urefu wa futi tatu au futi tano.

 

Wakati wa umeng’enyaji chakula tumbo hukutana na kazi ngumu pale mtu anapokula vyakula vinavyosindikwa viwandani na kuwekwa kwenye makopo ambavyo vina kemikali za kuvifanya visiharibike mapema.

Kemikali hiyo ya kuhifadhi vyakula hasa nyama nyekundu husababisha ukinzani wakati wa chakula kumeng’enywa tumboni na matokeo yake husababisha vitumie muda mrefu kumeng’enywa.

 

Nyama nyekundu na vile vilivyopikwa na mafuta mengi huweza kuchukua hadi saa 72, sawa na siku tatu kukamilisha kazi ya umeng’enyaji. Mazingira hayo ya chakula kudumu muda mrefu husababisha sumu kwenye vyakula kuongezeka kama vile tindikali.

 

Tindikali pamoja na vitu vingine

hatari kwa afya kama mafuta, lehemu, chumvi na kafeini huathiri ini na kwenye ini ndiko mifumo mingine huathirika na mtu kujikuta akiugua maradhi ya moyo na damu kama vile shinikizo la damu, kisukari, kupooza na maradhi ya mara kwa mara.

Nyama nyekundu, ni moja ya sababu zinazosababisha tatizo hilo japokuwa ni muhimu kwa binadamu, lakini inapoliwa kupita kiasi ni tatizo. Kwa kawaida binadamu anatakiwa kula nusu kilo ya nyama nyekundu kwa wiki,

lakini walio wengi wanakula zaidi ya nusu kilo kwa siku. Hilo ni tatizo. Unashauriwa kula nyama nyeupe.

 

Nyama nyeupe ambayo ni samaki, kuku na dagaa ni muhimu sana kwa mwili na haina madhara kama ilivyo kwa nyama nyekundu ambayo ni ngumu katika kumeng’enywa hivyo kutumia muda mrefu.

Upo uthibitisho wa kutosha kwamba ulaji wa nyama nyekundu kwa kiasi kikubwa unaongeza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo mkubwa na kila gramu 50 inayoongezeka hufanya uwezekano wa kupata saratani kwa asilimia 15.

 

Aina nyingi za saratani huanzia katika mtindo wa maisha na ulaji wa mhusika. Mtu anapokula vyakula vinavyoushughulisha utumbo mwembamba na mpana kuchuja vyakula hivyo kwa muda mrefu, husababisha saratani, tumbo kujaa gesi, kuuma, kukosa haja na hata kukosa hamu ya kula.

 

Viko baadhi ya vyakula vinavyoweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani kama vile vyenye mafuta mengi ambavyo vinasababisha uzito mkubwa na huweza kumfanya mtu kupata magonjwa ya saratani ya matiti, kongosho na kizazi.

Vyakula vilivyosindikwa vimethibitishwa kwamba vinaongeza uwezekano wa kupata saratani na wataalamu hawajaweza kuona kiasi chochote kinachoweza kutumika bila kuongeza uwezekano wa kupata saratani.

Nyama iliyosindikwa ni pamoja na ile iliyohifadhiwa kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi. Aina hii ya nyama ni pamoja na nyama za kopo, soseji na zinginezo. Epuka.

Ili vyakula viweze kumeng’enywa vizuri, inashauriwa kula mbogamboga kwa wingi pamoja na matunda. Katika upikaji wa mboga, isipikwe sana ili kutoharibu viinilishe muhimu. Ikiwezekana baadhi ya mboga ziliwe zikiwa mbichi ili kukamilisha lengo hilo.

Comments are closed.