Kartra

Hatimaye Okwi Atangaza Kurejea Simba SC

MSHAMBULIAJI na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Uganda (Cranes), Emmanuel Okwi, amesema anaamini ipo siku atarejea kwa mara nyingine kwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Simba ya jijini Dar es Salaam.

 

Okwi ambaye aliwahi kuichezea Yanga ya Tanzania, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Al-Ittihad ya Misri tangu Juni 30, mwaka huu.

 

Mshambuliaji huyo alikuwa jijini hapa Ijumaa iliyopita akiiongoza Cranes katika mchezo wa Kundi E wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar dhidi ya Kenya ambao ulichezwa Jumamosi iliyopita na kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

 

Okwi alisema bado yuko katika kiwango cha juu na nafasi ya kurejea kucheza soka la kulipwa Tanzania ipo endapo atafikia makubaliano na klabu yoyote.

 

Okwi alisema kwa sasa ameielekeza akili na nguvu yake kuisaidia Uganda ifanye vizuri kwenye mashindano hayo na anaamini watapambana kuhakikisha wanatimiza malengo yao.

 

“Naamini siku moja nitarejea Simba, ni suala la muda,” alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda.

 

Aliongeza kuwa anafurahi kuona amekutana tena na Kocha Mserbia Milutin Micho katika kikosi cha Uganda na wameanza vema kwenye kampeni hiyo ya kuelekea Qatar.

 

“Ni kocha ambaye anaifahamu vema Uganda, naamini atatumia uzoefu wake kutufikisha mbali, akiwa nje amejifunza mambo mengi ambayo yatasaidia kukiimarisha kikosi chetu cha Uganda,” Okwi alisema.


Toa comment