The House of Favourite Newspapers

Hatua 7 za kukabiliana na nyakati ngumu maishani

0

SHIDA ni sehemu ya maisha ya binadamu. Katika dunia hii kuna wakati maisha hujaribu kuleta kila aina ya vizingiti na kama hutasimama katika mstari imara ni rahisi kushindwa.

Kila kitu huonekana kwenda mrama, na baadhi yetu hufikia hatua ya kukata tamaa na kuamua kuyaacha mambo yaende kama yalivyo, kitu ambacho si sahihi sana maishani.
Wakati mwingine ili uweze kusimama katika misingi imara kimaisha, basi ni lazima ukutane na vizingiti, dhoruba na vikwazo ikiwa ni moja kati ya njia za kukukomaza kimaisha.
Kuna vitu vikuu viwili maishani ambavyo mtu hawezi kuepukana navyo kwa namna yoyote ile, navyo ni Furaha na

Huzuni. Hivi ni vitu ambavyo kila mtu huvipitia, lakini cha kushangaza, watu wengi sana hupenda kukutana na furaha na inapokuja hali ya maumivu, basi wengi wetu hunyong’onyea na kuwa dhaifu katika utendaji wa mambo.
Hapa chini kuna badhi ya mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa ili kukabiliwa na wakati mgumu.

 

KUBALIANA NA HALI HALISI
Pindi unapokuwa unakabiliana na wakati mgumu maishani mwako, usikimbilie kukata tamaa, hatua ya kwanza kufanya ni kukubaliana na ukweli wa hali yenyewe ilivyokupata.

Kamwe hiki si kipindi cha kulaumu, hata kama wewe ndiyo chanzo cha tatizo hilo, bado hupaswi kujilaumu kwa kile ulichokifanya. Lakini pia usilipe nafasi kubwa tatizo hilo katika akili yako, kwani kufanya hivyo ni kuzidi kulikuza. Kuwa mtulivu tafuta njia ya kulitatua.

 

USIMWELEZE KILA MTU
Watu wengi hukosa uvumilivu pindi wanapokuwa katika nyakati ngumu maishani na kujikuta wakigeuka waropokaji kwa kila mtu wakidhani kwa kufanya hivyo kutasaidia kutatua matatizo yao, jambo ambalo si kweli.

Pamoja na ukweli kwamba matatizo huhitaji msaada wa kimawazo kutoka kwa watu wengine lakini si kwa kila mmoja unayekutana naye au kumuona. Jaribu kuwafuata baadhi ya watu ambao unaamini kuwa wanaweza kuleta suluhu, ukimweleza kila mtu ni rahisi kupata ushauri wa kukuvunja moyo.

 

USIKAE BILA KUJISHUGHULISHA
Epuka sana kukaa bila kujishughulisha kiakili na kimwili kila wakati ili kuitokomeza hali ya huzuni na maumivu unayokabilian navyo kwa kipindi hiki.
Pendelea kufanya baadhi ya vitu vinavyoweza kukuletea faraja na furaha, mfano labda kujisomea baadhi ya maandiko yatakayokupa mwanga, fanya mazoezi, angalia hata mechi mbalimbali za mpira pamoja na mambo ambayo unaamini ukiyafanya utapata mwelekeo mpya kimtazamo.

 

EPUKA MFADHAIKO
Hupaswi kukaa peke yako muda mrefu, kwani kwa kufanya hivi unakaribisha mfadhaiko akilini mwako kutoka na ugumu wa kimaisha unaokutana nao. Changamana na makundi ya watu wenye furaha ili wakusaidie kuponya huzuni yako.

 

JIAMINI, TUMIA UWEZO WAKO WOTE
Ndani yako kuna uwezo mkubwa sana ambao ukiutumia kikamilifu, unaweza kutatua baadhi ya mambo bila hata ya kuhitaji msaada kwa mtu mwingine. Unapaswa kujiamini. Usiwe na mashaka na uwezo ulionao ndani yako. Tambua maisha ni safari na dereva wake ni wewe.

 

USIKATE TAMAA
Katika maisha watu wengi hukwama kutatua changamoto zao si kwa sababu hawana uwezo la, ila ni ile hali ya kukata tamaa mapema inapowakumba.
Kwenye maisha hakuna kukata tamaa, hata kama hali ni ngumu kiasi gani usikubali kushindwa, endelea kupambana hadi tone la mwisho la jasho lako litakapoanguka ardhini, ari hii ni silaha kubwa sana ya kufanikiwa katika kupata furaha unayoitafuta.

 

PAZA SAUTI YA USHINDI
Watu wengi wanapokuwa kwenye hali ngumu za kimaisha hudhani kuwa watakuwa hivyo milele. Maisha yanapita, kila kwenye shida paza sauti moyoni mwako, kila mara jitangazie kuwa HILI NALO LITAPITA.

Leave A Reply