Hatua nne za mtu kujijua ana ugonjwa wa ukimwi

UGONJWA wa HIV/AIDS umekuwa janga kubwa sana duniani kwa sasa kutokana kuathiri watu wengi na kukosekana kwa tiba ya maradhi hayo. Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi (HIV/ AIDS) hufahamika kama maambukizi ya VVU (Virusi vya Ukimwi). Mtu anapopata magonjwa nyemelezi kitaalamu opportunistic infections ndiyo huwa tunasema mtu amepata ugonjwa wa Ukimwi au AIDS. Natumaini kwa kupitia makala haya tutakuwa tumetoa mwanga kidogo wa hatua za ugonjwa wa Virusi vya Ukimwi (VVU). Kuna hatua (stages) kuu nne za ugonjwa wa VVU/Ukimwi ambazo ni:

HATUA YA KWANZA HUITWA PRIMARY HIV INFECTION

Hatua hii huwa kwa muda wa wiki nne baada ya maambukizi. Ni asilimia 20 tu ya watu wenye maambukizi ya VVU walio kwenye hatua hii ambao hupata dalili na viashiria vikali vya ugonjwa huu lakini mara nyingi madaktari hushindwa kutambua kama mgonjwa amepata maambukizi ya VVU kutokana na dalili na viashiria vyake hapa kufanana sana na dalili za magonjwa mengine.

Mgonjwa aliye katika hatua hii ya kwanza ya maambukizi ya VVU huweza kuonesha dalili na viashiria kama vile kuvimba tezi (swollen lymph glands), kupatwa na homa kali, kuumwa koo (sore throat), kujihisi mchovu, kujihisi maumivu sehemu mbalimbali mwilini (body aches), kutokwa na

vipele mwilini (skin rash), na pia kutapika, kuharisha au kuumwa tumbo

Mgonjwa anayepata dalili na viashiria hivi tunasema kwamba amepata “Acute HIV infections.” Dalili hizi hutokana na mwili wa mtu mwenye maambukizi ya VVU kuanza kutengeneza kinga dhidhi ya VVU.

HATUA YA PILI (CLINICALLY ASYMPTOMATIC STAGE)

Katika hatua hii ambayo inaweza kudumu kwa muda wa miaka kumi, mgonjwa anakuwa haonyeshi dalili/ viashiria vyovyote vile isipokuwa anaweza kuwa na tezi zilizovimba (swollen lymph nodes).

Kiwango cha VVU kwenye damu hupungua sana lakini mgonjwa anaweza kuambukiza mtu mwingine yeyote na vipimo vya VVU vina uwezo wa kutambua uwepo wa maambukizi ya VVU katika damu.

Katika hatua hii VVU katika mwili huwa bado virusi vinazaliana (active) na hukimbilia/hujificha kwenye tezi (lymph nodes). Kutokana na kujificha kwake katika hatua hii, kipimo cha kupima wingi wa virusi vya Ukimwi (Viral load test) katika mwili hutumiwa sana ili kuweza kutambua uwepo wa VVU.

HATUA YA TATU (SYMPTOMATIC HIV INFECTION)

Kutokana na kuongezeka kwa wingi wa VVU katika mwili, kinga ya mwili huzidi kudhoofika na hii husababishwa na; tezi na tishu zilizoathiriwa na VVU huharibika kutokana na maambukizi ya muda mrefu.

VVU hubadilikabadilika na kuwa na uwezo zaidi wa kuathiri tishu na sehemu mbalimbali za mwili na hata kuziua/kuziharibu seli zinazokinga mwili kutokana na maambukizi zinazojulikana kama T helper cell na kushindwa kuzalisha seli nyingine mpya.

Dawa za kufubaisha VVU au Antiretroviral therapy (ARV’s) huanza kutumiwa wakati seli aina ya CD4 zinapopungua na kuwa kiwango cha chini sana. Kupungua kwa seli hizi za CD4 ni kielelezo cha kinga ya mwili kuwa dhaifu.

Matumizi ya dawa hizi huboresha kinga ya mwili na kumfanya mgonjwa kuishi kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili au viashiria vyovyote vile. Kama mgonjwa wa VVU hatumii dawa au anatumia ARV’s ambazo hazimsaidii au hazifanyi kazi vizuri mwilini mwake, basi mgonjwa ataendelea kuingia kwenye hatua ya nne ya Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) au AIDS.

Hatua ya Nne (UKIMWI)

Kama nilivyoeleza hapo juu, hatua hii hujulikana kama Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) au AIDS, ambapo mgonjwa hupata maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na

saratani za aina mbalimbali kutokana na kupungua kwa kinga mwilini.

Kwa watu wazima na watoto walio na umri zaidi ya miaka mitano, uwepo wa ugonjwa wowote nyemelezi pamoja na kushuka kiwango cha CD4 chini ya 200 cells/mm3 au kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 15 hutambulika kama mtu huyo tayari ana ugonjwa wa Ukimwi.

Kwa watoto walio chini ya miaka mitano, uwepo wa ugonjwa wowote nyemelezi/kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 20 au kwa wale wenye umri kati ya miezi 12-35 hutambulika kama wana ugonjwa wa Ukimwi. Watoto wenye umri chini ya miezi 12, kupungua kwa seli za CD4 chini ya asilimia 25 ndiyo hutumika kutambulisha wana ugonjwa wa Ukimwi.

USHAURI

Uonapo dalili zozote kati ya tulizozitaja wahi kuonana na mtaalamu wa afya ambaye atakupima na kuona upo katika hatua gani. Akigundua kuwa unastahili kuanza kutumia dawa, atakuelekeza jinsi ya kutumia na afya yako itaimarika. Kwa ushauri zaidi, tuma sms kwa namba hiyo hapo juu.
Toa comment