Hatua za kuanza kujitegemea
hatua za kuanza kujitegemea na kuachana na maisha ya kula kulala bure-2
ilipoishia wiki iliyopita;
KUJIAMINI
Vikwazo au shaka juu ya kuweza kumudu maisha ya kujitegemea vimewafanya wengi wasijiamini. “Kwa kipato hiki nitaweza kweli kuendesha maisha yangu, nilipe kodi ya nyumba, chakula, mavazi na mahitaji mengine?” Maswali ya aina hii mara nyingi yamekuwa na majibu ya HAITAWEZEKANA!
Katika asili; tabia ya akili hasa katika kufikiria mambo yajayo ni kujenga hofu ambayo wakati mwingine haihitajiki; wenye kujiamini pekee ndiyo ambao hutupilia mbali hofu na kujaribu kufanya yasiyowezekana kitu ambacho huwasaidia kupata maendeleo wayatakayo maishani mwao.
Kwa msingi huo, unapofikiria maisha ya kujitegemea usiwaze sana juu ya kuwezekana kwa mambo, jiamini kuwa utaweza, ukifanya hivyo; kumbuka kuwa siku zote mwenye shaka havuki mto!
KUCHUKUA HATUA
Hatua nyingine muhimu baada ya kupita vipengele nilivyoanisha hapo juu ni hiki cha kuchukua hatua. Watu wengi wamekuwa wakipanga kujitegemea, lakini kila mwaka wanaahirisha kufanya hivyo. “Nafikiri nitahama mwaka ujao.” Mwaka ukifika anapanga kufanya hivyo mwaka unaofuata matokeo yake anazeeka akiwa kwenye maisha tegemezi.
Ushauri wangu, baada ya kujiamini kuwa unaweza; chukua hatua ya kutoka mahali ulipo! Jambo kubwa la kuzingatia hapa ni kuhakikisha kuwa uchukuaji hatua lazima uambatane na ushauri mzuri kutoka kwa ndugu na jamaa na hasa wale uliokuwa unaishi nao kama wanakuunga mkono katika suala hilo.
KUTORUDI NYUMA
Uchunguzi unaonesha kuwa, wapo watu ambao hupitia hatua zote za kuelekea kujitegemea, lakini wanapozikabili changamoto za maisha hayo huamua kurudi mahali walipokuwa wanaishi jambo ambalo huwaongezea fedheha na mara nyingine kuwaathiri kisaikolojia.
U
napokuwa umeanza maisha ya kujitegemea suala la kurudi ulipotoka lisiwe la kawaida. Kumbuka unapokuwa na wazo la “nikishindwa narudi kwa baba,” huwezi kujituma, hutapambana na changamoto za maisha binafsi kwa vile kinga yako haitakuwa kwako bali kule ulikotoka, kushindwa itakuwa ni sehemu yako.
ONGEZA MARAFIKI
Unapokuwa kwenye maisha ya kujitegemea hakikisha kuwa unajitahidi kupunguza maadui. Fanya kila linalowezekana kuongeza marafiki ambao siku zote ndiyo nguzo muhimu nyakati za shida. Kumbuka kazi ya rafiki ni kufariji na adui ni kuangamiza! Jenga marafiki usijenge maadui.
Jitahidi sana mahali ulipopanga, unapoishi baada ya kutoka kwenye maisha ya familia unakuwa na mafariki wengi sahihi kadiri iwezekanavyo, hawa watakusaidia kukupa uzoefu wa maisha na wakati mwingine watakuonesha njia za kukabiliana na changamoto unazokutana nazo.
B
aada ya kusema hayo, naamini mada hii itawasaidia wengi; furaha yangu ni kusikia baada miezi, miaka michache ijayo watajitokeza watu ambao watatoa ushuhuda kuwa walianza maisha ya kujitegemea kutokana na hamasa waliyoipata kwenye somo hili.
Asante msomaji wangu kwa kuwa pamoja katika somo hili naomba usiache kuungana nami kila siku ya Jumatano kwenye ukurasa huu ndani ya gazeti hili la Risasi Jumatano!