Hawa: Naogopa kuumizwa

 

HAWA Said almaarufu kama Hawa Nitarejea ni miongoni mwa wasanii ambao walifanya vizuri kipindi cha nyuma hasa baada ya kutoka kwenye Ngoma ya Nitarejea aliyoshirikishwa na staa wa muziki huu wa Bongo Fleva; Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’. Baadaye alishika vichwa vingi vya habari kutokana na matatizo aliyopitia. Mrembo huyu kwa sasa yupo poa na anatamba na ngoma yake ya Mpera ambayo inafanya poa.

IJUMAA SHOWBIZ imepiga stori na Hawa, fuatilia makala haya upate kujua mengi kumhusu yeye;

IJUMAA SHOWBIZ: Mashabiki wako wangependa kujua Hawa ni mtu wa aina gani?

Hawa: Mimi ni mtu wa kawaida sana, mpenda watu wote bila kubagua wala kujali hali zao na napenda sana kusoma mambo ya dini.

IJUMAA SHOWBIZ: Kazi ya muziki ilikuwa ni ndoto yako au uliamua tu kufanya kwa ajili ya kipato?

Hawa: Ukinikata hata damu yangu, ni muziki tu kwa sababu tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana kuimba na hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nijiingize kwenye muziki.

IJUMAA SHOWBIZ: Hongera ngoma yako mpya inafanya vizuri, vipi imekugharimu kiasi gani hadi hapo ilipofika?

Hawa: Kiukweli siwezi kusema uongo kuhusu gharama kwa sababu kwa sasa sina management (usimamizi), hivyo kazi ambazo ninazitoa, ninajiongoza mwenyewe, lakini pia ninapata msaada kutoka kwa watu ambao wana uhitaji wa kunisaidia wakiwemo maprodjuza.

IJUMAA SHOWBIZ: Baada ya kazi hii uliyotoa, je, una mpango wa kuachia album hivi karibuni?

Hawa: Kwa sasa bado sielewi kuhusu kutoa album kwa sababu muziki wangu nausimamia mwenyewe na muziki umebadilika, si sawa na zamani, hivyo album bado kabisa.

IJUMAA SHOWBIZ: Ni changamoto gani unazopitia kwenye muziki wako?

Hawa: Hakuna kazi isiyokuwa na changamoto, hivyo changamoto zipo na ni nyingi sana, japokuwa siwezi kuzitaja zote. Mojawapo ni kwamba, huwa ninahitaji vitu vitokee, lakini havitokei kwa sababu sina nguvu kubwa.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, ni mafanikio gani unayapata kupitia muziki wako?

Hawa: Mafanikio yapo kwa sababu mwanzo tulikuwa tunakaa kwenye nyumba ndogo ambayo haina umeme, lakini kwa sasa ninamshukuru Mungu nimeweza kupanga upande mzima.

IJUMAA SHOWBIZ: Uliwahi kuwa na ukaribu wa kimapenzi na Diamond, je, ana mchango gani kwenye muziki wako?

Hawa: Diamond ana mchango mkubwa kwa sababu ninapata sapoti kutoka kwake. Hata Wasafi (Lebo ya Diamond) wananipa sapoti kubwa tu na unapozungumzia Wasafi, unamzungumzia Diamond.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, kuna mpango wowote wa wewe kusainiwa Wasafi?

Hawa: Hakuna utaratibu wowote uliofanyika wa mimi kusainiwa Wasafi, lakini natamani sana kupata nafasi ya kuwa mmoja wa wanafamilia wa Wasafi.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, una mpango wa kufanya ngoma nyingine na Diamond?

Hawa: Mpango wa kufanya kazi na Diamond upo, natamani tufanye Remix ya Nitarejea, lakini bado sijamwambia.

IJUMAA SHOWBIZ: Tulitegemea ungekuwa miongoni mwa wasanii watakaomsindikiza Diamond katika kuadhimisha miaka kumi ya muziki wake kule Kigoma, lakini hukuwepo, kulikoni?

Hawa: Nilipata mwaliko, lakini sikuweza kuhudhuria kutokana na majukumu ya kifamilia.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamshauri nini Diamond kama mtu wako wa karibu juu ya kuzaa na  wanawake tofauti?

Hawa: Sina cha kumshauri, huwezi kujua anachokutana nacho huko kwa hao wanawake ambao anazaa nao, labda anatendwa au anaumizwa maana yeye pia ni binadamu.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, kwa sasa upo kwenye uhusiano wa kimapenzi?

Hawa: Hapana, kwa sasa siko kwenye uhusiano ila natamani na nina mpango huo, japokuwa naogopa kuumizwa kwa sababu ninahisi hawatanipenda kutoka moyoni, labda wananipenda kwa sababu mimi ni msanii.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, familia yako ilichukuliaje hali uliyokuwa nayo kipindi umejiingiza kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya?

Hawa: Kwanza kabisa hakuna mzazi ambaye anapenda mwanaye aharibike, kiukweli walijisikia vibaya mno. Hata watu wanaonizunguka walinionea huruma, ni vile tu hawakuwa na jinsi ya kunisaidia.

IJUMAA SHOWBIZ: Baada ya kupona, kuna vishawishi gani unavyopitia na unajizuiaje kurudi kwenye matumizi ya madawa ya kulevya?

Hawa: Naamini ukiamua kuacha kitu ni umeamua, hakuna kurudi nyuma, hata kwa upande wangu nimeamua kutojihusisha tena na sitajaribu.

IJUMAA SHOWBIZ: Una mpango gani kuwaokoa wanawake walio kwenye matumizi ya madawa ya kulevya?

Hawa: Nikiwezeshwa naweza kuwa na taasisi ya kuwasaidia maana nia ninayo ila kwa sasa napenda kuwatia moyo watu ambao bado wako kwenye matumizi ya madawa ya kulevya maana mimi ni kama balozi kwao, hivyo wanitazame na wajifunze kupitia mimi.

IJUMAA SHOWBIZ: Mbali na muziki, unajishughulisha na kitu gani kingine?

Hawa: Nashona nguo na kusuka nywele kwani hicho ndicho kipaji kingine nilichojaaliwa.

IJUMAA SHOWBIZ: Ni kitu gani ambacho huwezi kusahau kwenye maisha yako?

Hawa: Siwezi kusahau siku ambayo nilibadili dini kwa sababu ya ndoa na nikawa kwenye ndoa kwa muda wa miezi mitatu tu na kuachana na mume wangu.

HAPPYNESS MASUNGA NA QAISSY MOHAMEDY

Toa comment