The House of Favourite Newspapers

HAWA: NATESEKA, TUMBO LINAJAA MAJI KILA WIKI

Hawa Masanja ‘Hawa wa Nitarejea

KAMA watoto wakinililia, waambie kesho nitarejea,

Wadanganye na vibagia, waambie pipi ntawaletea,

Nawe usichoke kuvumilia, na kila siku kuniombea,

Unapokwenda kama ukifika salama, utukumbuke na sisi,

Usisahau kwamba mkeo na wana, umetuacha na dhiki,

Vile usijali ila naomba chunga sana, ogopa na marafiki,

Wakikulaghai hata kwa mbegu za mtama, waambie sidanganyiki…

Ni moja kati ya kiitikio kutoka Wimbo wa Nitarejea wa Diamond Platnumz akimshirikisha mwanadada Hawa Masanja ‘Hawa wa Nitarejea’. Ni wimbo unaoishi, ngumu kusahaulika kwa mashabiki na hata kwa msanii Hawa kwani ndiyo uliomuangazia maisha yake ya kimuziki katika ulimwengu wa Bongo Fleva.

Miaka inakwenda kasi, ni zaidi ya mwendokosi, ‘jana’ Hawa alikuwa hakamatiki baada ya kuachiwa kwa Wimbo wa Nitarejea lakini ‘leo’ Hawa huyuhuyu yupo hajiwezi, amekata tamaa ya kuishi baada ya kupata tatizo la kujaa maji kwenye tumbo lake kwa takribani mwaka mmoja sasa.

Bi’dada huyu mwenye sauti tamu, alipotea kwa muda katika gemu ya muziki wa Bongo Fleva kutokana na kinachodaiwa kuwa alikuwa akitumia vilevi vikali aina ya konya na gongo, vilivyomfanya aumwe mara kwa mara na hata kupoteza ladha nzuri ya sauti yake ya kuimba.

Kwa muda sasa, ameendelea kuishi kwa tabu na mateso makali baada ya kuambiwa na madaktari kuwa tatizo lipo kwenye Ini lake kubwa hivyo linashindwa kupeleka na kusukuma maji mwilini, ambalo limesababisha tumbo lake kujaa maji na kumfanya kwenda hospitali kila baada ya wiki mbili au tatu kwa ajili ya kunyonywa maji hayo wakati akisubiri matibabu zaidi. Inasikitisha sana ukimuona!

TUMSIKIE MWENYEWE

Tatizo hili la Ini lilinianza tangu mwaka jana mwezi wa saba, nilivyoacha tu kutumia mihadarati, lakini sikuwa na hali kama hii ya tumbo kujaa maji, lilianza taratibutaratibu mpaka lilipofikia miezi tisa ndiyo hali ikaanza kuwa mbaya kwa sababu lilikuwa limejaa sana.

Nikaenda hospitali, wakaanza kunitoboa kupunguza maji ilimradi niweze kulala, mara ya kwanza nilitolewa maji lita nane, ila nikawa kama nimelichokoza kwa sababu sasa hivi natakiwa niwe naenda kutolewa maji kila baada ya wiki mbili au tatu na kila nikienda lazima nilazwe kwanza.

ULISHAWAHI KUWAULIZA MADAKTARI KAMA KUNA UWEZEKANO WA KUKUTIBIA NA TATIZO LIKAISHA KABISA?

Ndiyo nilijaribu kuwauliza madaktari wa pale Muhimbili, kama kuna uwezekano wa kunitibu ili hili tatizo liishe kabisa, waliniambia kuwa uwezekano upo kwa sababu wanaweza kunipandikiza Ini lingine japo sijajua watanipandikiza vipi, lakini kwa sasa hivi bado naendelee kusubiri hivyo nitakuwa natolewa maji tu basi. Kuna muda mwingine maji yakijaa sana yanapanda mpaka kifuani nashindwa kuhema, ikifikia hali hiyo huwa napata tabu sana.

VIPI KUHUSU GHARAMA ZAKE?

Gharama mara nyingi huwa anatoa dada yangu, Pili Massana (Msimamizi wa kituo cha matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya), kwa sababu mimi bado nipo soba, ila nina kama mwezi na wiki hivi nimekuja hapa nyumbani kwa mama yangu (Buguruni jijini Dar) baada ya kuona hali yangu inazidi kuwa mbaya, niliogopa nikaona nisije nikafa bila kumuaga mtoto na mama yangu.

ATAMANI KURUDI KWENYE GEMU LA MUZIKI

Natamani kurudi kwenye muziki, natamani kuimba tena kama zamani, mara ya kwanza nilipopelekwa soba niliamini hali yangu ingekuwa nzuri na nilitegemea sasa hivi waandishi mngekuwa mnanihoji labda kuhusu wimbo wangu mpya, lakini ona nilivyokuwa, ona hali yangu yaani imekuwa tofauti na nilivyokuwa nikitegemea kuwa.

AMLILIA DIAMOND

Naamini Diamond atakuwa ameiona hali yangu kwenye vyombo vya habari, nawashukuru sana watu wa media kwa kunisaidia kuitangaza hali yangu kwa Watanzania ili wanisaidie, hivyo namuomba Diamond pia anisaidie mimi naumwa sana jamani nahitaji msaada.

MSIKIE MAMA YAKE MZAZI

Kiukweli nimepata shida sana na binti yangu, ni kama mwaka sasa tangu aanze kuugua, nilikaa kimya kwa muda mrefu lakini baadaye nikaona nalemewa na mimi hali yangu kifedha sio nzuri, ndio maana nikaamua kwenda kwenye vyombo vya habari ili kama kuna Mtanzania yeyote ataguswa na hali ya mwanangu aweze kunisaidia.

CHANGAMOTO ANAZOPITIA

Changamoto ninazopitia ni kubwa, mfano kama hivi nashindwa hata kwenda kwenye biashara zangu, kwa sababu muda wote natakiwa kukaa na mgonjwa tu (Hawa), muda wote nashinda hospitali, inafikia hatua mpaka na mimi mwenyewe kutokana na mwili wangu jinsi ulivyo (Mnene) nakuwa mgonjwa lakini sina jinsi nitafanyaje inabidi nijikaze kwani mwanangu sina wa kumuachia.Image result for diamond platnumz 2018

ATOA USHAURI KWA WATU WANAOTUMIA VILEVI

Nawashauri waache, tena waache kwelikweli, wamuone mwenzao anavyopata tabu sasa hivi (Hawa), yaani wasithububutu waache kabisa kabisa, unajua hawatayaona madhara mwanzoni watakuja kuyaona baada ya muda mrefu kupita na ndivyo ilivyotokea kwa huyu mwenzao.

AWAOMBA WATANZANIA WAMSAIDIE

Nawaomba Watanzania waweze kunisaidia, au kama kuna Daktari au mtu yeyote mwingine ambaye anaweza kujua tiba ambayo naweza nikaipata au sehemu gani rahisi ambapo mimi naweza nikatibiwa nikarudi katika hali yangu ya kawaida, hapa nilipo siwezi kufanya kazi yoyote tumbo likijaa maji, zaidi ya kuoga na kulala tu basi.

Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo hili anaweza kutoa kumchangia kiasi chochote cha pesa au akatoa ushauri kupitia namba 0712032705 au unaweza kutuma pesa kupitia akaunti ya NMB no. 2031

MEMORISE RICHARD

 

 

 

Comments are closed.