The House of Favourite Newspapers

HAYA NDIYO MAISHA YA MTOTO WA MASOGANGE

IKIWA imepita miezi kadhaa tangu Video Vixen wa Bongo, Agnes Gerald ‘Masogange’ afariki dunia na kuzikwa nyumbani kwao Mbeya, mengi yalisemwa ambapo Ijumaa limekusogezea maisha ya mtoto wake, Sania Sabri yalivyo kwa sasa.

 

Akizungumza kwa niaba ya mtoto huyo, baba wa Sania, Sabri Shaban alisema hadi sasa Masogange amewaachia pigo kubwa maishani mwao na kuna muda Sania huwa anahitaji mapenzi ya mama lakini hayapati.

 

Sabri amezungungumza mengi, ungana naye hapa chini ili kuyajua mengi;

Ijumaa: Nianze kwa kukupa hongera, naona binti yako kahitimu elimu yake ya shule ya msingi.

Sabri: Nashukuru sana, japo shughuli ilitawaliwa na kilio kikubwa, mara baada ya mwalimu wake kutangaza kuwa huyu ndiye mtoto wa mtu Masogange, alijiskia vibaya sana akawa analia tu.

Ijumaa: Vipi maendeleo yake shuleni baada ya mama yake kufariki?

 

Sabri: Mwanzoni wakati msiba ndiyo umetokea, kidogo aliyumba lakini baadaye akakaa sawa, akawa anaendelea vizuri kabisa na masomo yake, hata katika mitihani yake ya kila wiki, kidogo pafomansi yake imekuwa katika kiwango kikubwa.

Ijumaa: Hali ya maisha sasa hivi ikoje?

 

Sabri: Kiujumla tuko sawa, lakini kuna ugumu f’lani wa kulea mtoto peke yako bila mama yake, mtoto mara nyingi anamkumbuka mama yake, anakumbuka kuita mama, anakumbuka uwepo wake na mfano mzuri ni juzi tu kwenye mahafali yake, alihitaji kumuona mama yake lakini ilishindikana.

Ijumaa: Huwa ukikaa naye ni vitu gani ambavyo huwa anapenda sana kuviongelea?

 

Sabri: Mara nyingi anapenda kumuongelea mama yake, anamkumbuka sana, japo wakati mwingine huwa ananiumiza na mimi, lakini kwa kuwa mimi ni baba na yule ni mtoto najitahidi kumuweka sawa ili mradi maisha mengine yaendelee, kwa sababu kazi ya Mungu haina makosa.

Ijumaa: Masogange kakuachia pigo gani?

 

Sabri: Pigo kubwa sana, kwa sababu wawili ni wawili na mmoja ni mmoja tu, sisi tulikuwa wawili kumuangalia mwanetu lakini leo hii nimebaki mwenyewe, japo dada zangu wapo na wanaishi naye vizuri lakini kuna vitu vinakosekana kutokuwepo kwake, kwa sababu yeye ndo mama yake mzazi, lakini vile vitu tulivyokuwa tumepanga vyote inanilazimu nivifanye peke yangu bila yeye kuwepo.

Ijumaa: Changamoto gani unazozipitia sasa hivi katika kumlea mtoto peke yako?

 

Sabri: Ni kuhusu majukumu, kwa sababu mimi na yeye tulikuwa na majukumu ya lazima, hao waliokuwepo wanafanya kwa hiari, mfano nilikuwa na uwezo wa kumwambia Agness mimi nina hiki na wewe toa hiki tufanye kitu f’lani kwa mwanetu, lakini sasa hivi sina mtu wa kusema kwamba nitamwambia atoe zaidi.

Ijumaa: Vitu gani ukiviona kwa mtoto wako huwa unamkumbuka sana mama yake?

 

Sabri: Vitu vingi mfano nikimuangalia sura anafanana sana na mama yake, mimi na Agness tulianza uhusiano tukiwa bado wadogo, kwa hiyo katika umri ambao mwanangu anaukaribia ndiyo umri ambao tulikutana mimi na mama yake tukiwa bado wadogowadogo, kwa hiyo naanza kumuona kama vile mama yake alivyokuwa katika umri huo hivyo kuna muda naweza nikakaa nikamuangalia sana.

 

Ijumaa: Kuna wasanii wowote ambao huwa wanakuja kujulia hali mtoto?

Sabri: Ndiyo, wapo baadhi ambao huwa wanafanya hivyo, mfano mtu kama Rammy Gallis na Irene Uwoya, mara nyingi huwa wananipigia simu kuniuliza maendeleo ya mtoto yakoje, nawashukuru sana kwa hilo.

Comments are closed.