The House of Favourite Newspapers

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-2

0

ULIPOISHIA GAZETI LA AMANI LA JANA:
“Wale siyo Wazungu bwana Tolu, wale ni viumbe wa ajabu wa majini na wengine wapo nchi kavu. Lakini majini wapo wengi zaidi na ndiyo makao yao makuu,” aliniambia Nurdin.
“Una maanisha nini kusema viumbe wa ajabu Nurdin?” nilimuuliza huku nikimtumbulia macho.
“Majini.”
ENDELEA SASA…

Nilishtuka sana kusikia kwamba, wale ni majini japokuwa akili yangu ilikuwa ikijiuliza kama ni Wazungu waliwezaje kusimama juu ya bahari bila kuzama?

Niliwahi kusimuliwa sana juu ya uwepo wa majini duniani lakini sikuwahi kujua wapo katika mwonekano gani japokuwa niliamini ni viumbe wenye sura mbaya sana, pengine wana meno marefu kupita ya mnyama ngiri na pia wana macho makubwa kuliko chungwa kubwa, kumbe sivyo.
“Bwana Tolu hujawahi kusikia habari za kuwepo kwa majini hapa duniani?” Nurdin aliniuliza.
“Nimeshasikia.”

“Ndiyo wao, sasa tumepita kwenye eneo lao ndiyo maana unaona meli inakwenda sawasawa sasa. Lakini pia huko mbele tutakutana na eneo ambalo halijajulikana ni la nani na linakuwaje.”
“Lina nini Nurdin?” nilimuuliza haraka sana huku moyo ukiwa na wasiwasi.

Katika maisha yangu, hakuna kitu sikipendi kama kuishi kwa hofu, wasiwasi, shakashaka au kuogopa jambo. Napenda sana uhuru na amani ya moyo wangu.

“Kuna sehemu meli ikipita inakuwa kama imeingia kwenye msitu mnene ulioshikana miti na majani, kwani kuna kuwa na gizi totoro, taa za meli tu ndiyo utajua nipo ndani ya chombo kama hiki.”
Bado nilikuwa na maswali kibao kichwani, kwamba kama ni hivyo, kwa nini watu wanaamua kuwa manahodha, yaani madereva wa meli.

“Bwana Tolu, wewe kama umeamua kufanya kazi hii hakikisha unakuwa imara, ndiyo maana sisi wengine tunatumia pombe kali na kuvuta bangi. Si kwa kupenda bali mazingira,” alisema Nurdin.
“Ina maana wafanyakazi wote wa melini wanavuta bangi na kunywa pombe kali?” nilimuuliza.

“Hapana, kila mtu ameumbwa na ujasiri wake. Ninachokwambia mimi ni ujasiri wa mtu. Lakini bwana Tolu hujaniambia kama kabla ya kuja kufanya kazi hii ulikwenda kwa wataalam kukingwa.”
“Nurdin kusema kweli sikwenda na wala sikuwahi kuwaza kwenda. Nimekuja mimi kama mimi nikimtegemea Mungu wangu tu.”

”Oke, sasa tunakaribia hiyo sehemu yenye kiza kinene kama nilivyokwambia,” Nurdin alinikumbusha huku akinikodolea macho.

Meli yetu ilikuwa ina sehemu ya juu kabisa ambayo, unaweza kupanda huko na kukaa kuangalia maji ya bahari. Nurdin akaniambia twende nikamkatalia kwa woga wangu. Aliniambia hakuna baya, ndiyo nikakubali kwenda.

Kwa mara ya kwanza niliweza kuona mambo yenye maswali kibao kwa baharini na usiku huo. Miongoni mwa mambo hayo ni kuona vitu vikimetameta kama nyota za angani.
“Nurdin, vile vinavyometameta kwenye bahari ni nini?” nilimuuliza mwenyeji wa majini.
“Bwana Tolu ni kwa sababu ni usiku tu lakini ingekuwa mchana ungeona mambo ya kushangaza sana. Vile ni vinyama vidogo sana lakini viko kwa wingi sana. Wingi wao wewe hujapata kuuona, hata makundi ya nyumbu hayafui dafu.

“Najua unataka kujua kama ni vinyama kwa maana gani! Ni vinyama kwa maana ni vidogo sana, vidogo kama panya puku, lakini wanaishi juu ya maji na wanatembea juu ya maji. Hivi meli inavyotembea, vinapisha kwa ubishi. Macho yao ni makali sana ndiyo maana unaona hali ya kumetameta kama hivi. Itaendelea katika Gazeti la Ijumaa siku ia Ijumaa, usiko kufuatilia.

Leave A Reply