The House of Favourite Newspapers

Hekalu la Dogo TRA ni Jipu

0

Na Waandishi Wetu, AMANI
DAR ES SALAAM: Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili wameonesha kushtushwa kwao kufuatia mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Romuald Rumanyika kujenga nyumba kubwa ‘hekalu’ wakidai inawezekana kuwa ni jipu!
Nyumba hiyo imejengwa Goba Kibulu, Kinondoni jijini Dar es Salaam huku Rumanyika mwenyewe akitajwa kuwa bado mdogo akilinganishwa na hekalu lake hilo hivyo kumhisi kwamba, inawezekana amejenga kwa kutumia pesa zenye figisufigisu.

MSIKIE HUYU
“Jamani sisi ni wakazi wa Goba hapa kuna dogo (kiumri) mmoja wa TRA amejenga nyumba kubwa yale mnayosemaga mahekalu katika muda mfupi. Mimi simtuhumu vibaya ila nawaomba mfuatilie ili kama ni halali tujue, kama kuna namna za konakona, pia tujue.

“Nasema hivi kwani huyu dogo tangu ameanza kazi nadhani huu ni mwaka wa pili au tatu. Je, anaweza kuwa na mshahara wa kumudu kufanya makubwa kama haya? Hesabu za haraka ule mjengo unaweza kugharimu shilingi milioni 100. Sasa kwa mshahara wa watumishi wa umma, sidhani kama angeweza, ” kilisema chanzo hicho.
Amani: “Inawezekana ni pesa halali, kwani mtu anaweza kufanya kazi lakini akawa na biashara nyingine, nyie mtajuaje?”
Chanzo: “Mh! Labda, lakini tunaomba mfuatilie. Mwenye wasiwasi si mimi tu, wapo wengine.”

AMANI LAMSAKA
Baada ya maelezo hayo, Amani lilimtafuta Rumanyika kwa njia ya simu alipopatikana na kuulizwa, hali ilikuwa hivi:
Amani: “Naongea na Romuald Rumanyika?”
Rumanyika: “Ndiyo, nani? Unasemaje?”

Amani: “Wewe si unafanya kazi TRA? Sasa hapa ni Global Pulishers, Gazeti la Amani. Kuna madai kwamba, umejenga nyumba kubwa sana, Goba. Halafu watu wanasema una muda mfupi kazini. Kwa hiyo wana wasiwasi huenda umetumia pesa ambazo hazipo katika mtiririko wa mshahara wako, unasemaje?”
Rumanyika: “Acheni kufuatilia maisha yangu kwani nyinyi mnataka nini?” (akakata simu).

AMANI ENEO LA TUKIO
Juzi Jumanne, waandishi wetu walikwenda Goba kwa lengo la kukutana na mjumbe yeyote wa nyumba kumi sambamba na kuiona nyumba hiyo ambayo picha yake ipo kwenye maktaba yetu.

CHA AJABU
Cha ajabu ni kwamba, waandishi wetu walipofika nyumbani hapo, alitokea mtu aliyesema anaitwa Erick Sanga na ni mjumbe msaidizi. Baada ya waandishi kujitambulisha, akaomba vitambulisho, akapewa, alipoviweka mfukoni akasema:
“Leo mnapasuka. Tulikuwa tunawasubiri kwa hamu sana mkione cha moto. Mnamfuatafuata bosi wetu, mnataka kumuharibia maisha yake. Sasa leo mtakiona.”

Ilibidi waandishi watumie hekima ya kujieleza. Hata hivyo, Sanga aliita watu kibao na kuwazunguka waandishi wetu huku wakionekana kuwa na hasira.
Miongoni mwa walioitwa ni Gladness Manonge ambaye ni mjumbe wa nyumba kumi kwenye mtaa huo. Yeye aliwasikiliza waandishi wetu na kuahidi kuwasiliana na Rumanyika ili ajitokeze kwa waandishi wa habari aelezee kuhusu madai hayo, asipende kujifichaficha.

WAANDISHI TAKUKURU
Waandishi wetu waliwasiliana na Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Benn Zomba. Yeye aliomba jina lote la Rumanyika na kusema atafuatilia kwa karibu kwani ndiyo kazi iliyopo sasa nchini.

Leave A Reply