Heri ya Siku ya Wanawake 2023 kutoka Global Publishers
Leo, Machi 8, 2023 ni siku kama siku nyingine yoyote ile katika maisha yetu lakini kinachoifanya iwe na tofauti ya kipekee ni sababu kwanza Mwenyezi Mungu katujalia kuiona leo ukifananisha na wengi waliotangulia mbele ya haki, na pili sababu ni siku ya kumsheherekea na kumuenzi mwanamke na nafasi yake katika jamii na maisha yake ya kila siku.
Kwanini tunamsheherekea Mwanamke?
Sababu kubwa ya kumsheherekea na kumuenzi Mwanamke ni kumkumbusha kuwa nafasi yake katika maisha inathaminiwa, inaonekana, ina mafanikio na ni msingi kwa familia na jamii kwa ujumla. Kwamba inawezekana hajafika anapopalenga, inawezekana bado hajapata mafanikio anayotarajia, inawezekana anapata changamoto kubwa ya muda mrefu kama vile kuwa ‘single mother’ au mjane, inawezekana anaumizwa kwa mambo mengine mbalimbali hadi akasahau umuhimu na thamani yake lakini bado anasonga mbele bila kukata tamaa tena kwa bidii zote.
Kusheherekea kunatukumbusha kwamba hata hatua hii tuliyoifikia tayari ni sehemu kubwa ya mafanikio tunayostahili kujipongeza kwa jitihada hizo, haswa ukizingatia umetoka mbali na bado upo unasonga mbele.
Silaha thabiti ni kutokata tamaa na kujifunza kufurahia yale ambayo ni mazuri katika maisha yetu iwe mawasiliano, mahusiano na ushirikiano na pia kujifunza kujenga furaha kwa waliokuzunguka kwa kuwa mtu mwenye furaha na mwenye kusambaza furaha.
Sisi GlobalPublishers tunajivunia kuwa na Wanawake wanaojielewa, wanaojitambua na kuwa na michango thabiti kwenye katika mitandao yetu.
Ni kwa misingi hii, tungependa kuwashukuru kwa dhati kwa uwepo wenu hapa na hivyo kujiona wenye bahati ya kuwa nanyi na kuwatakia sikukuu njema ya Wanawake.
Mwaka huu kauli mbiu ni #BalanceForBetter ni matumaini yetu kuwa kauli hii haitaishia kutajwa hivyo bali kila mmoja katika jamii ashiriki katika kujenga jamii inayotoa haki sawa kwa wote.
Happy International Women’s day 2023!