The House of Favourite Newspapers

HESLB Yatoa Siku Tano Kwa Wanafunzi Waliomaliza Mafunzo ya JKT

0

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inawajulisha wanafunzi waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hivi karibuni kuwa mfumo wa kuomba mkopo kwa njia ya mtandao utafunguliwa kwa siku tano (05) kuanzia kesho, Alhamisi, Oktoba 1, 2020 ili kuwawezesha kuomba mkopo.

Uamuzi huu unatokana na maombi ya wanafunzi, wazazi na walezi wa wanafunzi wahitaji ambao hawakuweza kuomba au kukamilisha maombi yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujiunga na mafunzo katika kambi mbalimbali za JKT kwa mujibu wa sheria.

Aidha, katika muda huo wa siku tano, mfumo pia utakuwa wazi ili kuwawezesha waombaji ambao maombi yao yana upungufu kurekebisha kwa kuweka nyaraka sahihi ili kuiwezesha HESLB kuendelea na hatua nyingine.

“Kwa wanaorekebisha taarifa, wanapaswa kuingia katika akaunti zao walizofungua kuombea mkopo na watapata ujumbe kuhusu maeneo ya kurekebisha. Tunawasihi watumie muda huu wa siku tano kurekebisha na kukamilisha maombi yao ili kutuwezesha kuendelea na hatua inayofuata ili hatimaye wenye sifa wawezeshwe kutimiza ndoto zao,” amesema Mkurugenzai Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru.

Katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga TZS Bilioni 464 zitakazowanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000. Kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo. Mwaka 2019/2020 jumla ya TZS 450 bilioni zilitengwa na zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119.

Leave A Reply