The House of Favourite Newspapers

HII NI 4G… BARA TUNAPIGA, CAF TUNACHAPA

KAMA ulidhani Simba inazifunga timu za Ligi Kuu Bara pekee basi  najidanganya kwani jana ilianza vizuri kampeni yake ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Gendarmerie Nationale ya Djibouti mabao 4-0.

 

Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, umekuwa wa saba sawa na dakika 630 kwa Simba kucheza bila kuruhusu bao wavuni mwake. Ushindi huo unaifanya Simba kuwa na kazi nyepesi ugenini katika mechi ya marudiano itakayochezwa Jumanne ya Februari 20, mwaka huu huko Djibouti

City, kwenye Uwanja wa El Hadj Hassan Gouled Aptidon nchini Djibouti. Katika mchezo wa jana, Simba ilipata bao lake dakika ya kwanza mfungaji akiwa ni kiungo Said Ndemla aliyefunga kwa mkwaju wa faulo iliyotokana na John Bocco kuchezewa vibaya nje kidogo ya lango la Gendarmerie.

 

Baada ya kuingia kwa bao hilo, Gendarmerie walionekana kuamka na kushambulia kwa kushitukiza huku wakijiimarisha zaidi katika ulinzi. Beki wa Simba, Asante Kwasi alikosa bao la kichwa dakika ya 22 baada ya mpira aliopiga kuokolewa na mabeki wa Gendarmerie. Kwasi alikuwa anaunganisha faulo ya Shiza Kichuya.

 

Huku Gendarmerie wakijitahidi kucheza kwa kujilinda zaidi, walijikuta wakifungwa bao la pili dakika ya 32 na Bocco aliyefunga kwa kichwa baada ya mabeki wa timu hiyo ya Djibouti kushindwa kuokoa mpira uliopigwa awali.

 

Huku mashabiki wakidhani Simba ingeenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0, Bocco aliifungia tena Simba bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi safi fupi iliyopigwa na Emmanuel Okwi.

 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 49 Gendarmerie walipata penalti baada ya Erasto Nyoni wa Simba kumchezea rafu, Abdorahim Mohamed ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, Moustapha Mousaa wa Gendarmerie alikosa penalti hiyo baada ya kipa wa Simba, Aishi Manula kupangua penalti yake na kuwa kona ambayo haikuleta madhara yoyote.

 

Ndemla alipiga shuti kali dakika ya 59 lakini kipa wa Gendarmerie, Bilali Ahmed alipangua mpira wake na mabeki wakauokoa. Simba ilipata bao la nne dakika ya 90 kupitia kwa Okwi ambaye alimaliza mpira aliotengewa na Nyoni katika faulo waliyoipata jirani na lango la Gendarmerie.

 

Kipindi cha pili wachezaji wengi wa Gendarmerie walionekana kukosa umakini katika stamina kiasi cha kudondoka kila mara hali iliyotokana na joto kali la Dar es Salaam.

 

Katika mchezo huo, Simba iliwafanyia mabadiliko Ndemla, Kichuya na nafasi zao zikachukuliwa na Mwinyi Kazimoto na Mzamiru Yassin. Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema; “Tulicheza kwa mpangilio bila ya kutumia nguvu nyingi kwa sababu mbeleni tuna mechi mbili mfululizo za ligi ambazo zote tunataka ushindi.”

 

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Gendarmerie, Mvuyekure Issa, alisema: “Nilidhani Simba wangetufunga mabao kumi lakini tumefungwa mabao 4-0, si mbaya kwani taarifa nilizopata zilikuwa zikisema ni timu hatari sana”.

 

MZEE RUKSA AIPONGEZA SIMBA

 

Mgeni rasmi katika mchezo huo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ally Hassani Mwinyi, alisifu kiwango cha Simba katika mchezo huo.

Mwinyi alisema: “Kwa sasa Tanzania siyo kichwa cha mwendawazimu, ni kichwa cha muungwana.”

 

Mara ya mwisho kwa Simba kucheza mechi za Caf ilikuwa mwaka 2013 ilipotolewa na Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba ilifungwa bao 1-0 nyumbani halafu ugenini ikafungwa mabao 4-0.

Simba: Manula, Kapombe, Kwasi, Mlipili, Nyoni, Mkude,Kichuya, Kotei, Bocco, Okwi, Ndemla.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.