Hili la kubaki vituoni kulinda kura ni kuingizana chaka!

JUMAPILI ijayo, baada ya hii ya keshokutwa, Watanzania kwa ujumla wetu, tutakuwa katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, tayari kwa zoezi ambalo limetufanya kuwa na presha kubwa kwa miezi kadhaa sasa, kupiga kura.

Zoezi hilo kwetu ni muhimu sana kwa sababu ndilo litakaloamua hatima ya maisha yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Ni muda mchache maana miaka mitano iliyopita tulifanya kama hivi, lakini leo tunalia kwa kinachoendelea.

Ni siku ambayo wengi tunaamini tutakwenda kutumia vichinjio vyetu kwa ajili ya kuleta mabadiliko, maana maisha haya ya sasa, kila mmoja yamemchosha. Ufisadi kila kona, ubadhilifu serikalini ndiyo usiseme, wapiga dili kila sekta, rushwa nayo ni hatari, ilimradi kila mtu anayepata nafasi katika utumishi wa umma, anautumia yeye na wanaomzunguka kujinufaisha.

Kila mmoja anaona jinsi ambavyo watumishi wa serikali wanavyojipatia utajiri unaokosa maelezo. Mtu kapata nafasi ya kuitumikia nchi katika cheo f’lani akiwa hana kitu kabisa, lakini unashangaa kuona kuwa baada ya miaka michache tu, mtu ameshakuwa na utajiri wa kutisha, anamiliki mali nyingi ambazo kwa hakika, hazina maelezo.

Nchi yetu imekuwa ya wapiga dili, yaani mtu yupo sehemu f’lani kule serikalini, basi ndugu zake wanapewa upendeleo, ardhi yenye rutuba wanachukua wao, tenda wanapeana wao na vitu vingine chungu nzima. Njoo kwenye utendaji kazi wao sasa, muda mwingi wanafanya kazi zao binafsi lakini kwa gharama za vifaa na muda wa serikali. Kifupi nchi yetu inahitaji mabadiliko makubwa. Tunahitaji kumpata kiongozi ambaye anaweza kusema hapana na ikawa.

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo ningependa sana kuwashauri wapiga kura wenzangu ambao Jumapili ile tutakuwa pamoja vituoni. Kuna baadhi ya wagombea wanatangaza hofu ya kuibiwa kura. Ili kuhakikisha kura zao zipo salama, wanawahamasisha wapiga kura wenzangu kubaki vituoni ili kuzilinda.

Sitaki kujadili uhakika walionao kwamba wana kura nyingi zitakazoibwa, ninachotaka kushiriki na wenzangu ni kwamba kama viongozi wanasema baada ya kupiga kura tusiende umbali mrefu zaidi ya mita 100, kisha tukae hapo kuhakikisha kura haziibwi.

Huenda wana hofu hiyo kutokana na uzoefu wao katika zoezi hili tangu lianze 1992. Lakini katika kutekeleza hili la kutoondoka umbali mrefu vituoni, nishauri kwamba viongozi wanaohubiri jambo hili, wawe wa kwanza kukaa na kusubiri umbali huo baada ya kupiga kura.

Mgombea wa urais, ubunge na udiwani awe wa kwanza kusimama umbali huo, ili sisi wapiga kura tuwe na uhakika na wanachokitetea. Akae hapo atuongoze kwa sababu yeye anajua zaidi sheria na kanuni za uchaguzi, kwani hata mamlaka zingine zitakapokuja kuuliza kwa nini tupo hapo, awe wa kwanza kutuongoza kuzungumza.

Ninaogopa wapiga kura wanaweza kutumiwa kama chambo, wao wakae hapo waimbe nyimbo za ushindi, viongozi wao wakiwa wamekaa sebuleni wanatazama televisheni zao jinsi wanavyopata usumbufu kwa mamlaka zingine.
Kama kweli viongozi hawa wanamaanisha, basi na iwe hivyo, vinginevyo, nisingekushauri kufanya hivyo kwa sababu nyingi, lakini muhimu zaidi ni swali, tangu lini kura moja ikaamua mshindi?

Nilisema na nitarudia tena, kura ya uhakika ambayo mgombea wako amepigiwa ni yako peke yako, zingine si zako kwa sababu hujui mwenzako kampigia nani. Kuna watu watajiunga na wewe kukurubuni kuwa wamempigia chaguo lako kwa sababu wanataka uanzishe fujo ili wao waanze kupora au kufanya uhalifu mwingine. Chonde mpiga kura, jukumu lako ni kupiga kura na kuondoka, mambo mengine waachie wenyewe wanasiasa, wanajuana hao!

Loading...

Toa comment