The House of Favourite Newspapers

Hili la mawaziri, miluzi isimpoteze Rais Magufuli!

1

RAIS John Pombe Magufuli anatarajiwa kutangaza Baraza lake la Mawaziri muda wowote kuanzia wiki ijayo, atakapokuwa ameshamtangaza Waziri Mkuu, kisha kuthibitishwa na Bunge mjini Dodoma.

Mamilioni ya Watanzania wanasubiri kwa hamu kubwa kutangazwa kwa baraza hilo, kwani wanaamini ndiyo itakuwa mwanga wa kujua kama kweli, matumaini yao kwa rais huyu wa tano ni yenye kuleta matumaini au ni yaleyale ya kila msimu.

Wengi wana imani na Magufuli na hasa mwanzo wake wa ziara za kushtukiza na maagizo mawili matatu aliyokwishatoa hadi sasa. Waziri Mkuu na baadaye Baraza la Mawaziri, litakuwa ndilo kipimo cha kuanza kuakisi kasi na dhamira yake katika kuipatia Tanzania mabadiliko inayohitaji.

Hata hivyo, wakati kila mmoja akitegemea mazuri kutoka kwake, kuna miluzi mingi inapigwa na watu binafsi, taasisi na hata kada mbalimbali, kama wanasiasa, wanasheria na wengine kadha wa kadha. Kila mluzi unamwita na kumwelekeza nini cha kufanya.

Lakini miongoni mwa miluzi ninayoitilia shaka, ni ile inayomtaka, katika Baraza lake la Mawaziri, Rais Magufuli aweke uwiano wa kile CCM wanachosema 50/50, yaani idadi iliyo sawia kati ya wanaume na wanawake. Kwa lugha nyepesi, nusu kwa nusu ya mawaziri wawe wa kike na kiume.

Simaanishi kuwadharau mama, shangazi na dada zangu, lakini najaribu kusema kile kilicho ndani ya moyo wangu, kwamba nchi yetu ilipo na kule tunakoamini Magufuli anaweza kutufikisha, bado tunahitaji kuwajengea wanawake uwezo wa kiuongozi, hasa katika kusimamia majukumu yao kama watendaji.

Wanawake wengi waliopewa madaraka, hawajawahi kuthibitisha ubora wao, badala yake wamekuwa wakifanya kazi kwa masilahi ya aliyewateua badala ya kufikiria majukumu yao kikatiba yanasemaje.

Mifano ya wanawake hao iko mingi, maana tunao wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na hata mawaziri. Nchi haijawahi kushuhudia kiongozi mwanamke akiwa mfano wa wenzake katika kusimamia majukumu yake, kama tulivyowahi kuona kwa mabosi wanaume, mfano wa Dk. HarrisonĀ  Mwakyembe alipokuwa Uchukuzi, Profesa Sospeter Muhongo akiwa Nishati, Magufuli mwenyewe akiwa Ujenzi na wengine wachache.

Wanawake mara zote wamethibitisha kuwa nafasi wanazopewa ni zawadi, kama ilivyokuwa kwa spika aliyepita, Anne Makinda ambaye mara nyingi aliponda hoja na mawazo ya upinzani, hata pale yaliposimamia masilahi ya taifa, badala yake alijitoa kwa chama chake bila kujua wajibu na majukumu ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tuwe na mawaziri wanawake, lakini katika baraza dogo kama alivyoahidi Rais Magufuli, tusifanye makosa ya kuwaweka wengi kwa sababu ya kutaka sifa za kimataifa tuonekane tunajali jinsia.

Zipo nafasi nyingi tunazoweza kufanya majaribio ya uongozi, lakini siyo kwenye sehemu tunazohitaji wasimamizi thabiti wa kututoa hapa tulipo.

Rais Magufuli anahitaji askari shupavu katika kipindi hiki cha mpito. Katika kauli mbiu ya Hapa ni Kazi tu, hatutaki nafasi hiyo apewe mtu, kesho na keshokutwa ikimshinda na kuondolewa, tuanze kusikia kelele kutoka kwa makundi yakidai kuonewa kwa sababu ya jinsia yake.

Tunapotafakari akina mama wanaostahili kupewa nafasi za kufanya kazi kumsaidia Magufuli, hatutarajii kuona mtu anayepewa kwa sababu ya kuwepo kwake katika mtandao uliofanikisha rais kuukwaa ubwana mkubwa.

Tumeshuhudia nafasi nyingi zikitengenezwa na kupewa wanawake ambao waliwaacha watu midomo wazi, kwa sababu walisababisha maswali mengi yaliyokosa majibu. Tusingependa haya yajirudie, kama yupo mwanamke wa kazi apewe, lakini asipewe mtu kwa sababu ya uhodari wake wa kupiga picha za pozi, eti tu ili tuwe na 50/50.

1 Comment
  1. Mtunda says

    Hii ni kudharau wanawake. Huwezi kuto hoja ya “ujumla” namna hii. Tumeisha ona wanawake wanaopewa madaraka ndani na nje ya nchi wanafanya kazi vizuri. Nisingependa kupoteza muda kwaorodhesha wanawake hao, lakini wapo.

Leave A Reply