Himid awapa Simba SC mbinu za kuwaua Al Ahly

KIUNGO wa El Entag El Harby ya Misri, Mtanzania Himid Mao amebainisha wazi kwamba Simba wana uwezo wa kuifunga Al Ahly endapo tu watatumia vizuri zaidi faida ya kucheza nyumbani.

 

 

Himid ameongeza licha ya ubora walionao Al Ahly lakini Simba wanaweza kuwafunga endapo watakuwa na maandalizi mazuri na pia kufaidika kwa kucheza juani (saa 10) kutokana na Misri kuwa na baridi.

 

 

Kiungo huyo ametoa siri hizi ikiwa kesho Jumanne, Simba watakutana na Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

 

Himid ambaye huu ni msimu wake wa tatu nchini Misri inapotokea Al Ahly, ameliambia Championi Jumatatu, kuwa wanaweza kuifunga Al Ahly kwenye mechi hiyo endapo tu watakuwa na maandalizi na kutumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani.

 

 

“Simba ni timu kubwa na bora kwa sasa Tanzania kwa mtazamo wangu. Ahly ni timu kubwa na bora kwa Afrika lakini sio sababu ya Simba kutopata matokeo kama wakijiandaa vizuri na kutumia faida ya kucheza nyumbani.

 

 

“Pia hali ya hewa ya joto itakuwa nzuri zaidi kwa Simba maana huku Misri ni baridi sasa tangu mwezi wa 11 mwaka jana kuna baridi,” alimaliza Himid aliyeichezea Azam FC kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa.

SAID ALLY, Dar es Salaam

Toa comment