Kartra

Hitimana Aanza na Mkwara Mzito Simba SC

BAADA ya kukabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi cha Simba, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Mrundi Thierry Hitimana amesema kwa kuanza atahakikisha anakuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji wake.

 

Kocha huyo amejiunga na Simba kwa ajili ya kuliboresha benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mfaransa, Didier Gomes na Selemani Matola.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Hitimana alisema kuwa amejiunga na timu kubwa yenye uhitaji wa matokeo mazuri ya ushindi, hivyo ni lazima apambane kuhakikisha wanafanya vema.

 

Hitimana alisema kwa kushirikiana na bosi wake Gomes, atatumia mbinu na ufundi wake wote ili wafikie malengo yao ikiwemo kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“Simba ni timu kubwa kwa sasa Afrika. kupata nafasi ya kufanya kazi na klabu kama hii ni jambo la kujivunia na fursa kukuza uzoefu wangu.

 

“Unajifunza kufanya kazi na timu yenye uhitaji wa matokeo chanya katika kila mechi inayocheza kitu ambacho kama kocha kinakufanya muda wote kuwa ‘stable’ kwenye mbinu zako, kuwasoma wapinzani , kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji wako.

 

“Pia kuimarisha umoja wa timu na klabu mbele ya wanachama wetu, mashabiki na uongozi kwa ujumla. Tunajukumu kubwa kimataifa pamoja na bosi wangu Gomes na hakika tutatimiza malengo ya timu na klabu,” Hitimana.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam


Toa comment