Kartra

Hitimana: Gomes Atabaki Kuwa Bosi Wangu Simba

SIMBA imetambulisha Thierry Hitimana raia wa Rwanda baada ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja kama kocha msaidizi wa timu hiyo inayojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

 

Simba imefikia hatua hiyo baada ya Shirikisho la Soka Afrika CAF, kutoa orodha ya majina ya makocha 11 wa klabu zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambao hawana vigezo vya kukaa kwenye benchi kuziongoza timu zao akiwemo Didier Gomes kutokana na sheria mpya zitakazotumika msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Caf imezitaka klabu kuwa kila kocha mkuu anayepaswa kukaa kwenye benchi kuwa na leseni A ya Caf au Uefa Pro ambazo Gomes hana hali iliyopelekea Simba kumpa mkataba wa mwaka mmoja Hitimana ambaye Caf itamtambua kama kocha mkuu kutokana na leseni yake Uefa Pro kukidhi mahitaji ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Hitimana siyo jina geni katika Ligi Kuu Bara kutokana na kuwahi kuzifundisha Biashara United kabla ya kwenda Namungo aliyoipandisha kutoka daraja la kwanza hadi Ligi Kuu ambapo mwanzoni mwa msimu uliopita alitimuliwa na kwenda Mtibwa Sugar ambayo hakudumu akarejea kwao Rwanda.

 

Kocha huyo amefanya mahojiano maalum na Championi Jumatatu, baada kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.

 

Kocha huyo ameliambia Championi Jumatatu, kuwa hana presha yoyote kufanya kazi kwenye timu yenye presha ya mashabiki wengi kwa kuwa siyo mara yake ya kwanza kufanya kazi kwenye timu zenye presha ya mashabiki.

 

“Binafsi kwangu siyo jambo la kupata presha kwa sababu nimeshafanya kazi kwenye klabu ambazo zinapresha ya mashabiki, nimefundisha Rayon Sports ya Rwanda ni timu kubwa na ina mashabiki wengi.

 

“Nadhani hakuna kipya ambacho pengine kitanipa hofu ila utofauti utakuwepo kwa sababu hapa ni Tanzania na nilipotoka ni Rwanda hata ukubwa wake haupo sawa licha ya zote kuwa zina mashabiki wa kutosha.

 

Baada ya Simba, kukutangaza, Mtibwa kupitia baadhi ya viongozi wao wanadai kuwatendea haki maana umeshindwa hata kuaga?

 

“Hapana, binafsi naamini nimeondoka kwa wema kwa sababu kabla ya kuondoka niliwaaga sasa kama watakuwa wanasema sikuwapa taarifa za kuondoka itakuwa wananikosea, hawanitendei haki kabisa huenda wanataka nifikiriwe vibaya na mashabiki kama mtu msaliti lakini si kweli.

 

SIMBA WALIKUFUATA LINI?

“Mazungumzo na Simba hayakuja jana wala juzi, tuna zaidi ya miezi miwili tulikuwa tunaongea isipokuwa wao ndiyo walikuwa hawajakamilisha kwa upande wao lakini mazungumzo yalikuwa ya muda mrefu.

 

UMEWEZAJE KUONDOKA MTIBWA WAKATI ULISHAANZA MAA NDALIZI YA MSIMU UJAO?

“Ni kweli nilikuwa nimeanza maa ndalizi lakini bado mimi na Mtibwa tulikuwa hatujasaini mkataba wowote ambao unaweza kuzuia kitu kingine.

 

“Lakini inatakiwa kufahamika kwamba Mtibwa, waliniita kwa ajili ya mazungumzo kwa sababu wao walinitumia mkataba lakini kuna vipengele nilikuwa sikuweza kuvielewa.

 

“Kutokana na hivyo ndiyo wakawa wamenitumia tiketi ili kuja kufanya mazungumzo ambayo pia hata kutumwa kwake ilichelewa na wakati nilishaongea na Simba tayari pia kuna timu Uganda ilinitumia ofa.

 

“Lakini niliwaambia wasubiri hadi nirudi Tanzania ndiyo maana nashangaa kusikia kwamba wanalalamika kama sijawaaga wakati siku ya Alhamisi niliongea na viongozi na kuwaambia kwamba Simba wanahitaji, naenda kuwasilikiliza ikiwa tofauti nitarejea.

 

“Kuhusu tiketi, nilishakubaliana nao kwamba gharama zilizotumika zinarudishwa na hata Simba wanatambua ni jambo la kuweka sawa.

 

“Unajua wakati huo wote, nilikuwa nafanya kazi ya kukaanda timu na bado sikuwa na mkataba nao sasa nilivyokwenda kuwasikiliza mambo yakawa vizuri.

 

CAF INAKUTAMBUA WEWE KAMA KOCHA MKUU KUTOKANA NA LESENI YAKO NA SIYO GOMES LAKINI SIMBA IMEKUTAMBULISHA KAMA KOCHA MSAIDIZI, UNADHANI KWA NINI?

“Kiukweli mkataba wangu nipo hapa kama kocha msaidizi halafu sikuja hapa labda kufanya mambo ya tofauti au kutaka kumuondoa Gomes, Gomes atabaki kuwa bosi wangu na yeye ndiyo mwenye kauli ya mwisho, ninachokijua mimi ni kocha msaidizi.

 

SIMBA INA WACHEZAJI WENYE MAJINA MAKUBWA TOFAUTI NA TIMU NYINGINE ZA HAPA ULIZOFUNDISHA, UMEJIPANGA VIPI KUKABILIANA NAO?

“Nadhani wengi hawajui kwamba hata mimi nimecheza mpira hadi kwenye levo kubwa kabla ya kuwa kocha, hakuna ambacho sikutambui, nimecheza hadi timu ya taifa ya Rwanda na niliondoka kwa sababu ya majeraha.

 

“Sasa suala kuwa na wachezaji wana majina makubwa haliwezi kunipa wakati mgumu kwa kuwa maana nimekuja kushirikiana na waliokuwepo ili kuifikisha timu ilipo na siyo kufanya mapinduzi,” anasema Hitimana.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam


Toa comment