The House of Favourite Newspapers

Hivi Ndivyo Mkewe Alivyomponza Mugabe Ikulu

0
Rais wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe Grace Marufu.

RAIS Robert Mugabe (93), amefikia hatua ya mwisho kuondoka madarakani kwa nguvu kutokana na kuponzwa na mke wake, Grace (52).

Kutokana na hali hiyo, tayari ametoa ombi kwa makamanda wa jeshi wamhakikishie usalama wake, mkewe pamoja na mali zake anazomiliki.

Miongoni mwa mali anazodaiwa kumiliki ni pamoja na majumba ya kifahari yaliyopo katika nchi mbalimbali ikiwemo Malaysia, Singapore, Dubai na Afrika Kusini.

MKEWE AMEMPONZA

Sababu kubwa iliyomponza Rais Mugabe ambaye aliongoza nchi hiyo kwa miaka 37ni kumsikiliza mno mkewe katika masuala yanayohusu uongozi wa nchi.

Grace alikuwa akifanya kila aina ya vitimbi kuhakikisha anamweka Rais Mugabe kiganjani ili aweze kukwaa nafasi ya umakamu wa rais.

Nafasi hiyo alikuwa akiimezea mate kwa muda mrefu ndiyo maana alianza kampeni za kuhakikisha Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa anafukuzwa kazi.

“Lazima aondoke. Nitahakikisha hatua zinachukuliwa dhidi yake ndani ya chama na serikali,” alijigamba Grace na muda si mrefu Mugabe akamtimua.

Grace aliongeza kuwa,“Siku za nyuma tulikuwa na makamu wa rais, lakini hatukuona tatizo lolote ndani ya chama. Lakini alipokuja Mnangagwa na Phelekezela Mphoko matatizo ndipo yalipoanza,”.

“Sisi kama wanawake ni muda wetu wa kushikilia nafasi ya makamu wa rais. Nafasi ya Mnangagwa lazima irudi kwa mwanamke,” alisema.

Akionekana kumuunga mkono mkewe, Rais Mugabe kwa hasira alisema,“Nilifanya kosa kumteua Mnangagwa kama makamu wangu wa rais? Kama ndivyo nitamuondoa,”.

Mugabe alikwenda mbali zaidi na kusema kama Mnangagwa na wenzake wanataka kuanzisha chama cha siasa na waanzishe.

“Hatuwezi kuwa na chama ambacho kila mara kuna msuguano na kejeli zisizoisha,” alisema Mugabe kabla sekeseke la kumuondoa madarakani halijipamba moto.

Tangazo la kufutwa kazi kwa Mnangagwa lilitolewa na Waziri wa Habari, Simon Khaya Moyo, kwa kusema:

“Makamu wa rais amekuwa na mienendo isiyoridhisha. Hana nidhamu, haaminiki lakini pia hatimizi majukumu yake inavyotakiwa.”

Wakati hali hiyo ikiendelea, Mugabe ambaye alitikisa dunia na kuonesha ubabe wa kila aina kwa Wazungu, kwa sasa amejikuta njia panda.

Hatua hiyo inatokana na kuingia kwenye msukosuko mkubwa kati yake na viongozi wa serikali na chama tawala cha ZANU-PF, hivyo kujikuta akiwekwa kizuizini na jeshi la nchi hiyo.

Wakati hali ikiwa hivyo, Jumamosi chama hicho kilitangaza kuwa Mugabe si kiongozi wake tena, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa nchi nzima.

Hivyo kilimteua Mnangagwa ambaye alifutwa kazi kama kiongozi wake. Kufutwa kazi kumezua mambo mengi huku jeshi likitwaa madaraka na kumzuia kumteua Grace kama makamu wa rais.

Kitendo cha Mugabe kumfukuza kazi Mnangagwa kilikuwa sawa na kuchokoza nyuki kwenye mzinga.

Jumamosi iliyopita maelfu ya wananchi walijitokeza mitaani wakiwa na mabango ya kushinikiza Rais Mugabe aliyeingia madarakani mwaka 1980, aondoke.

Waandamanaji waliingia Mji Mkuu wa Harare wakiwa na mabango yaliyoandikwa Mugabe Must Go huku wakiunga mkono chochote kitakachoamuriwa na jeshi.

 

MKUU WA MAJESHI KUNENA

Mkuu wa majeshi, Jenerali Constantino Chiwenga ameweka bayana kuwa wataweka kila kitu bayana kwa ustawi wa wananchi wa Zimbabwe.

Wakati huo huo, Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC), limeripoti kwamba wanachama wa ZANU PF wanataka Mugabe ajiuzulu haraka.

Kwa miongo kadhaa, ZBC limekuwa likitumiwa na serikali kueneza propaganda za chama, lakini kwa sasa limebadilika ghafla.

Wakati hali ikiwa hivyo, Gazeti la Herald limeripoti kuwa chama hicho kinataka makamu wa Rais aliyefutwa kazi arejeshwe katika wadhifa wake.

Hadi tunakwenda mitamboni jana, Rais Mugabe alitakiwa awe ameachia ngazi na endapo hatafanya hivyo, wabunge watampigia kura ya kutokuwa na imani naye.

Rais Mugabe amefikia hapo kutokana na sababu nyingi, ikiwemo kitendo chake cha kurejesha ardhi iliyokuwa chini ya walowezi wa kikoloni na kuirudisha mikononi mwa Wazimbabwe.

Huu ulikuwa ukombozi kwa Wazimbabwe, lakini kitanzi kwa Rais huyo kwani alichukiwa na Wazungu na kuwekewa vikwazo kwenda Ulaya na Marekani.

Kwa hiyo, jaribio la kumpindua na mchanganyiko wa maadui aliojitengenezea ndani na nje ya nchi vina kishindo kikuu kwa yanayomtokea sasa.

Sababu nyingine ni ulafi wa madaraka ambao unasumbua viongozi kadhaa wa Afrika.

Mugabe licha ya umri wake wa miaka 93, ameshindwa kusoma alama za nyakati na matokeo yake dhoruba ya kisiasa inataka ‘kumzamisha baharini.’

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisoma vizuri alama za nyakati na mabadiliko ya kisiasa yalipoanza kuvuma aliamua kuondoka madarakani kabla bahari haijachafuka.

Mugabe hakupendelea njia ya Mwalimu na sasa anaelekea kubaya hasa ikizingatiwa kuwa hahimili tena mikikimikiki ya siasa za vyama vingi.

Kwa hiyo mahasimu wake wa kisiasa wanaona ndiyo njia ya kutokea. Akiwa kizuizini tulishangaa kusikia Morgan Tsivangirai, mpinzani wake wa siku nyingi, amerejea haraka haraka nchini humo.

Chanzo kingine cha mapinduzi yaliyoshindwa ni madai kuwa Rais Mugabe anaongoza nchi kwa ushauri wa mkewe, jambo ambalo halifurahishi wengi.

Pia kitendo cha kumfukuza makamu wake wa rais kilitafsiriwa na baadhi ya wanasiasa wa nchi hiyo kama alama ya kutopenda kumuudhi mkewe, Grace.

Hayo yote na mengine mengi, ikiwemo uchumi kudumaa, ukosefu wa ajira vinatosha kumfanya Rais Mugabe ashindwe kuongoza tena kwa amani.

Miaka ya 1990 uchumi wa Zimbabwe ulianza kuvurugika, umri wa watu kuishi ulishuka, mishahara ilikuwa kiduchu na hadi mwaka 1998 wasio na ajira walikuwa asilimia 50.

Kama hiyo haitoshi, makali ya maisha yalisababisha raia waanze kuihama nchi na mwaka 1997 waliopigana vita walianza kitimutimu cha kudai pensheni zao.

Kutokana na ukata, haikuweza kuwalipa na badala yake iliongeza kodi kwa wananchi, lakini haikusaidia.

Wakati hali ikiwa hivyo, Januari 1998, maandamano ya upungufu wa chakula yalilipuka mji mkuu wa Harare, jeshi likamwagwa mtaani kuwaondoa.

Katika tukio hilo watu takriban tisa walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa. Anatuhumiwa pia kubana wanasiasa wenzake na ukandamizaji mwingine mwingi.

UVAAJI NGUO

Anapenda sana suti zinazoutosha mwili wake sawasawa na tai zinazofanana na kitambaa. Huwavutia sana wanamitindo nchini Zimbabwe kwa mavazi yake.

ELIMU YAKE

Kwa jumla, Mugabe ana shahada saba. Digrii yake ya kwanza ni kutoka Chuo Kikuu cha Fort Hare, Afrika Kusini.

Alisomea shahada zake nyingine kupitia mtandao akiwa gerezani. Shahada hizo ni za elimu, sayansi, sheria na usimamizi.

Kifupi; huyo ndiye Rais Robert Gabriel Mugabe, mkongwe wa siasa barani Afrika.

MAKALA: Julian Msacky

Leave A Reply