The House of Favourite Newspapers

HIVI NDIVYO MUUZA PWEZA ANAVYOMZIDI KIPATO MFANYAKAZI WA BENKI

SHIMO kuu la kwanza la umaskini wa milele ni pale mtu anapoamka asubuhi na kusema; ‘Sina kazi ya kufanya’. Ukiwauliza wataalamu wa masuala ya uchumi watakuambia mtu akitaka kufanikiwa NI LAZIMA AFANYE KAZI.

Hata Maandiko Katika Kitabu cha Biblia yanasema asiyetaka kufanya kazi, asile. Pengine ndiyo maana hata Rais John Magufuli amesema: HAPA KAZI TU. Waulize vijana wengi kadiri ujuavyo swali hili: “Vipi ndugu yangu, siku hizi unafanya kazi gani?” Wengi wamekuwa wakijibu kuwa; “Sina kazi yoyote, niponipo tu.”

Maofisini nako kuna pitapita hii: “Samahani bosi, mimi ni msichana nimemaliza Digrii Yangu ya Masuala ya Uchumi, nimekuja hapa kuomba kazi.” Majibu ya mabosi wengi nao yamekuwa hivi: “Hapa hakuna kazi.”

Sina kazi, hakuna kazi, sijapata kazi, serikali haina nafasi za kazi, ni maneno yaliyozoeleka siku hizi. Pengine cha kujiuliza cha kwanza; ‘Kazi ni nini?’ Maana kutafuta na kuhangaikia kitu usichokijua nao ni umaskini wa aina yake.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili neno kazi maana yake ni; Shughuli anayofanya mtu. Zipo nyongeza nyingi kwenye maana ya neno hilo kwamba, shughuli lazima iwe halali na yenye kumletea mtu faida na si vinginevyo.Image result for PWEZA

Wengi wanaweza kujiuliza shughuli pia ni kitu gani hata ikosekane kwa kiwango kikubwa namna hii miongoni mwa jamii?Kwa ufupi tena ni kwamba, shughuli ni kama kulima, kufuga, kuandika, kufundisha, uhunzi na uchuuzi wa samaki wabichi.

Kama hivyo ndivyo, ukimsikia mtu anasema SINA KAZI maana yake halimi, hafundishi, hauzi vitumbua, hafugi kuku, hahudumii wafungwa, hachuuzi mihogo na wala hafagii takataka kwenye ofisi za watu. Je, ni kweli nchi yetu haina fursa za shughuli halali za kijipatia kipato kwa kiwango hiki? Tafakuri ndogo tu tena kwa elimu ndogo ina jibu lililonyooka juu ya swali hilo kwamba, nchi haina mkwamo huo mkubwa.

Ikiwa hata mwenye elimu ndogo anayejua maana ya kazi niliyoieleza iweje watu waseme hawana kazi za kufanya hapa nchini? Inakuwaje kijana mwenye nguvu anaamka asubuhi na kusubiri mkate wa kupewa na wazazi wake kwa hoja kwamba HANA KAZI?

Mjadala kama huu unapoupeleka kwenye makundi ya vijana hasa wanaoamani kuwa hawana kazi za kufanya uwe umejipanga kwa hoja na nguvu; pengine unaweza kushambuliwa kwa mateke na ngumi kwa madai kuwa unawacheka wasiokuwa na kazi. Pengine hata wewe unaposoma makala haya hadi hapa nilipofikia umeanza kunitegea kitanzi kwamba huenda najivuna kwa sababu mimi nina nafasi ya kazi; usifike huko mapema hivi!

Katika maisha yangu nazijua kazi; nafahamu mamia ya shughuli na nyingi kati ya hizo nimezifanya kwa mkono wangu ndiyo maana nimeona nishee na wewe msomaji wangu makala haya ya jinsi muuza pweza anavyomzidi mshahara mfanyakazi wa benki.

Nimetumia mfanyakazi wa benki kama kiambatanishi tu katika makala haya kwa sababu nafahamu bila shaka mfanyakazi wa benki anaheshimika kwenye jamii kuliko mponda kokoto na muuza mchuzi wa pweza.

Wakati nafanya uchunguzi wa makala haya nilipata sehemu ya ushahidi kuwa hata wanawake na hasa warembo na wenye sura nzuri wako tayari mara mia mbili kuolewa na mfanyakazi wa benki kuliko baba lishe.Image result for PWEZA

Sababu za wazi ni kwamba wasichana wengi wanaamini kuwa mfanyakazi wa benki ana kipato kikubwa kuliko muuza pweza, jambo ambalo lilinifanya nikijike katika kufanya uchunguzi wa kujua ni kweli kwamba mfanyakazi wa benki anapata fedha nyingi kuliko muuza pweza?

Pengine wakati unasoma andiko hili unanicheka kwa sababu na wewe unaamini kama wanavyoamini wengine kwamba, kazi ni uhasibu, uandishi wa habari, ukarani, ukurugenzi na ukuu wa mkoa.

Hizi kazi za kulima, kufuga, kuponda kokoto si kazi ndiyo maana unapoamka asubuhi na kujikuta wewe si mfanyakazi wa benki, siyo mweka hazina wa kampuni fulani na wala hujawa mkuu wa idara umekuwa mwepesi wa kusema HUNA KAZI.

Wakati umesema hivyo ni asubuhi hiyohiyo umeamshwa na mama yako umsaidie kupeleka supu ya utumbo kando ya ofisi ya mkuu wa wilaya ili kuwauzia wafanyakazi, lakini hukuiweka shughuli yako kwenye orodha ya kazi kwa nini? Jibu unalo, nami ninalo.

Nihitimishe sehemu ya kwanza ya makala haya kwa kusema: Hivi Ndivyo Muuza Pweza Anavyomzidi Kipato Mfanyakazi wa Benki.

Ungana nami wiki ijayo ili ujue siri hii iliyofichika, naamini ukifunguka utaacha kuwadharau wauza pweza na wachoma mishikaki.

STORI: RICHARD MANYOTA, UWAZI

Comments are closed.