The House of Favourite Newspapers

Hivi Ndivyo Waethiopia 20 Walivyonaswa Uvunguni mwa Lori

LIVE! Dereva wa lori aina ya FAW Scania (semi trela), Mbaraka Kassim (40), mkazi wa Tabata jijini Dar anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro akituhumiwa kubuni mbinu mpya ya kusafirisha kundi la wahamiaji haramu wapatao ishirini, wote raia wa Ethiopia alionaswa nao chini ya uvungu wa lori.

 

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo lililojiri mwanzoni mwa wiki hii mkoani hapa wakati wahamiaji hao wakisafirishwa kutoka Dar kwenda nchini Zambia, waliohojiwa na gazeti hili, walidai kwamba, watu hao huwashawishi baadhi ya madereva wenye tamaa kwa kuwalipa pesa nyingi ili wawasafirishe kuelekea Afrika Kusini.

 

“Huwa nasikia jamaa wanatoa pesa nyingi. Nasikia ni kati ya laki moja na laki mbili na huwa wanatoa kiasi wanachotajiwa na madereva kwani wanakuwa hawana uhakika na uhai wao. Kwao fedha ndiyo kila kitu na madereva wetu wakionesha tamaa ndipo hujikuta wakiwasafirisha na matokeo yake ndiyo kama hivyo kukamatwa,” alisema Fareed, mkazi wa Morogoro Mjini aliyeonekana kuujua vizuri mchezo huo na kuongeza:

 

“Hadi kufikia hatua ya kuwasafirisha wahamiaji hao haramu kwenye uvungu wa semi trela, inaelekea dereva huyo alilipwa pesa nzuri na Waethiopia hao.

“Kitu kingine ni kwamba wahamiaji hao wanapotoka kwao wanakuwa wanajua kabisa watapitia wapi kwa sababu katika kila nchi kuna watu wa mtandao huo wa usafirishaji. Hao maisha yao hutegemea kusafirisha wahamiaji haramu.”

 

Dereva huyo aliyekuwa akiendesha lori hilo likiwa na usajili namba T682 DCB aliyekuwa akitokea Dar kuelekea Zambia, alikamatwa mkoani hapa akiwa na wahamiaji hao haramu na kuibua gumzo la aina yake kutokana na mbinu hiyo aliyokuwa ameitumia ya kuwasafirisha jamaa hao.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi juu ya sakata hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Urlch Matei alithibitisha kumshikilia dereva huyo na wahamiaji hao waliokuwa wakisafirishwa kwenda Afrika Kusini wakitokea Ethiopia ambapo dereva huyo angewafikisha Zambia.

 

“Askari wetu, wakiwa doria, kwa kushirikiana na wananchi, walifanikiwa kuwakamata wahamiaji hao ambao ni raia wa Ethiopia. Walikamatiwa eneo la Mikumi wilayani Kilosa kwenye Barabara Kuu ya Morogoro inayoelekea lringa. “Watu hao walikuwa wamefichwa kwenye uvungu wa lori lililokuwa likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Mbaruku Kassimu ambaye ni mkazi wa Tabata jijini Dar.

 

“Lori hilo lilikuwa likitokea Dar kwenda Zambia na wahamiaji hao walikuwa wakielekea nchini Afrika Kusini hivyo walikubaliana awafikishe boda ili waingie Zambia, waendelee na safari yao,” alisema Kamanda Matei na kuongeza: “Tunatarajia kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani. Pia nitoe rai kwa waajiri kuajiri madereva wasiokuwa na tamaa hii kwa sababu ni hatari.”

STORI: DUNSTAN SHEKIDELE, MOROGORO

LIVE: MAKONDA AFUNGUKA A-Z ALIYOJIONEA ZOEZI LA WANAWAKE WALIOTELEKEZWA

Comments are closed.