Hivi ni kweli huwezi kuishi bila kukopa?
Nilishawahi kuandika makala moja kwenye gazeti dada na hili la Ijumaa kwenye safu ya Saikolojia, Maisha na Wewe iliyokuwa inahusu madeni yanavyowakosesha amani watu.
Nikasema kwamba, kukopa siyo dhambi, lakini kuna watu kwa kuwa wanapata mwanya wa kukopa, basi wanakuwa ni watu wa madeni kila kukicha. Hawa ni wale ambao kila wakiona kichaka, wanataka kujisaidia.
Kufuatia makala hayo, wapo walionitumia sms na kuniambia kuwa, hakuna asiyekopa! Eti kama serikali yenyewe inakopa, sembuse mimi na wewe? Nikakubaliana nao na nikawajibu kwamba, wana hoja.
Lakini sasa, huwa kuna wakati najiuliza kwamba, hivi siwezi kuishi bila kuwa na madeni? Huwa najitajidi sana lije jibu na NAWEZA lakini niwe muwazi, mara nyingi jibu linalokuja ni SIWEZI kuepuka kukopa kutokana na maisha yalivyo.
Kwa nini natamani niwe sikopi kabisa? Hii ni kwa sababu huwa nakosa amani sana ninapokuwa nadaiwa kisha muda wa kulipa ukakaribia halafu bado mambo siyo mambo. Huwa najiuliza, aliyenikopesha atanielewa kweli nikimuambia anivumilie?
Wastaarabu wanaweza kuwa wepesi wa kukuambia hakuna shida, utakapopata utalipa lakini je, pale utakapokuwa umemkopa mtu ambaye ukifika muda anataka chake, utakuwa na amani kweli?
Achilia mbali hilo la kutokuwa na amani, kiimani tunatakiwa kuhakikisha tunalipa madeni kabla kifo hakijatufikia. Sasa, itakuwaje pale ambapo unakufa na madeni kibao huku ndugu zako wakiwa hawana uwezo wa kukulipia? Hilo ni tatizo lingine!
Hata hivyo, wakati mimi nikiwa na hofu ya kukopa, naamimi nina watu wengi nyuma yangu wanaoogopa madeni ila kama hujui wapo ambao bila kukopa hawasikii raha.
Yaani wao wakipata mwanya wa kukopeshwa hawalazi damu, hata kama hawana sababu za msingi za kukopa. Ni wangapi unaowajua ambao wakipelekewa bidhaa za mkopo wanachukua hata kama hawana uhitaji?
Ni wanawake wangapi ambao unawajua wana madeni ya nguo wakati hawakuwa na shida ya nguo kivile? Ni wanaume wangapi ambao unawajua wana vipato lakini wana madeni makubwa kwenye maduka ya akina Mangi na hata baa?
Hakika ni wengi na hii yote inatokana na mtu kutokuogopa madeni. Hivi utakuwa ni mtu wa aina gani kila sehemu unadaiwa halafu hauna uhakika wa kulipa leo wala kesho? Kama unataka kuishi maisha ya kuchengachenga, yaani nyumbani hutulii, ukikutana na anayekudai unabadili njia, endekeza madeni.
Niseme tu kwamba, hukatazwi kukopa kwa sababu ni kweli kuna wakati unalazimika kufanya hivyo. Ila sasa, ukikopa uwe na uhakika wa kulipa kwa wakati na kama utakuwa umekosa pesa ya kulipa deni halafu muda wa kufanya hivyo umefika, huna sababu ya kuchenga. Mfuate anayekudai kisha muambie ukweli ili ajue jinsi ya kukusaidia.
Kumbuka wapo waliojinyonga kwa sababu ya madeni, wapo ambao wanakonda kila siku kwa kuwa wanadaiwa kila kona. Jiepushe na madeni yasiyo na lazima ndugu yangu!