Hivi unaziepukaje lawama kwa kutomuandalia mwanao kesho yake?

Ni wiki nyingine tunakutana tena kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na mishemishe zako za kimaisha kama kawaida.

Mimi mzima na niko tayari kukuletea mada ambayo naamini itayabadili maisha yako. Mpenzi msomaji wangu, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na ndiyo maana wengi wetu tunapobahatika kuitwa mama au baba, furaha inaongezeka ila tunaweka akilini kwamba majukumu yameongezeka.

Kutokana na hilo, ndiyo maana tumekuwa tukishuhudia watoto wakibadili mifumo ya maisha ya wazazi walio wengi. Wapo ambao walikuwa walevi sana lakini walipopata watoto wakaacha pombe.

Wapo waliokuwa wakiendekeza starehe kila siku lakini sasa hivi wana nidhamu kubwa ya pesa, kwa nini? Kwa sababu wamebaini ili watoto wao wakue katika misingi sahihi, lazima wapatilizwe kwenye mambo ya msingi yanayohitaji fedha.

Ukikuta mtu ana mtoto au watoto lakini anaendekeza anasa, huyo ukimfuatilia utagundua hata huduma kwa wale wanaomtegemea ni duni. Ndiyo maana leo nikaona niwakumbushe wazazi juu ya dhamana waliyonayo katika kuwatengenezea watoto wao maisha mazuri ya baadaye.

Nafanya hivi nikiwa na mifano ya wazazi ambao sasa hivi wanajuta kwa kushindwa kuwaandalia watoto maisha mazuri, badala yake sasa watoto wamekuwa wakiishi maisha yasiyo na nyuma wala mbele. Wamekuwa wezi, wavuta unga na wazururaji.

Watoto hao ukiwauliza ni kwa nini wanafanya hayo, wapo watakaojitetea kuwa maisha ni magumu na hawana kazi kwani hawajasoma wala kuandaliwa vyema kuyakabili maisha.

Upo mfano hai wa kijana mmoja ambaye mwishomi mwa wiki iliyopita alikamatwa maeneo ya Sinza jijini Dar akiwa kwenye jaribio la kutaka kuiba. Kijana yule hakuwa na muonekano wa kuwa kibaka na kwa waliomjua walidai wazazi wake siyo maskini kwani walikuwa wakifanya kazi serikalini.

Baada ya kukamatwa na kupewa kichapo alianza kutoa lawama kwa wazazi wake akisema: “Nisameheni, nina stresi za maisha. Mimi wazazi wangu walikuwa wakifanya kazi serikalini lakini hawakunisomesha, matokeo yake marafiki zangu naona wana kazi zao, wana familia zao, mimi sina kitu, kwa tamaa yangu ndiyo maana nimefikia hatua hii.”

Utetezi wa kijana huyo ni wa kijinga lakini ni wenye fundisho kwa wazazi. Kumbe vijana wengi wanafikia hatua ya kujiingiza kwenye vitendo viovu baada ya kutoandaliwa vyema na wazazi wao.

Najua wapo ambao wamesomeshwa na bado wanafanya mambo ya kijinga lakini mzazi tambua kwamba, ili kesho na keshokutwa mwanao akishindwa kujikimu usiwe lawamani, muandae kujitegemea.

Kama uwezo upo msomeshe, mkuze kwenye maadili mazuri, muwekee misingi mizuri ya maisha yake ya baadaye ila hata usipokuwepo, aweze kujitegemea.

Wapo wazazi wanaojisahau kutokana na utajiri wao. Unakuta mtu ana uwezo kiasi cha kuona hata asipomsomesha mwanaye atakula, atavaa na kufanya kila anachotaka, si pesa ya baba ipo? Mnaofanya hivyo mnakosea sana kwani leo upo lakini kesho ukiwa haupo, pesa zako za benki zikiisha huyu mtoto hatakuwa na maisha mazuri.

Kikubwa leo niwakumbushe tu wasomaji wangu hasa wale wenye familia kwamba, watoto wetu wanastahili misingi madhubuti ya maisha yao. Pambana kuhakikisha hata kesho ukiwa hupo mtoto aseme baba/mama ameniacha vizuri, tayari kukabiliana na changamoto za maisha.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

globalbreakingnews.JPG


Loading...

Toa comment