HIZI NDIZO SIKU 180 ZA MATESO YA RUGE

DAR ES SALAAM: Wakati mwili wake ukiwasili nchini leo ukitokea nchini Afrika Kusini, bado wingu jeusi limetanda nchi nzima kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.  

 

Hadi anafikwa na umauti, Ruge alipitia mateso makali yapata miezi sita, sawa na siku 180 kabla ya kufikwa na umauti. Ruge alifariki dunia jioni ya Februari 26, 2019 nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu ya matatizo ya figo na presha.

 

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa Clouds Media Group aliyeomba hifadhi ya jina kwa kuwa siyo msemaji wa familia ya Ruge, jamaa huyo alianza kuumwa kitambo kidogo tangu mwezi Mei, mwaka jana. Hata hivyo, pamoja na kwamba alikuwa akilalamika maumivu, lakini aliendelea na kazi kwa kuwa alikuwa akipenda mno kazi.

 

“Alianza kuumwa katikati ya mwezi wa tano kulelekea mwezi wa sita (mwaka jana). “Mwanzoni alijitahidi kuendelea na kazi, lakini hali ya mkurugenzi haikuwa nzuri.

“Nakumbuka aliomba kupewa muda kidogo ili ashughulikie afya yake. “Tuliona litakuwa ni jambo dogo tu na akapewa baraka zote. “Baadaye ripoti za kitabibu zilisema muda wa kupumzika ni mdogo hivyo akaongezewa muda na katikati ya mwezi wa sita na wa saba alirejea na kasi ya kawaida kwenye kazi. “Wiki mbili au tatu tukawa naye na hapo ndiyo tulikuwa tunakaribia kuanza Fiesta.

 

“Ilipofika Septemba hali ya mkurugenzi ilikuwa mbaya zaidi. “Ruge akatuambia inabidi aelekee kwenye taratibu za kimatibabu. “Kiukweli Ruge alikuwa mpambanaji sana, lakini alihitaji muda mwingi wa kupumzika.

“Baada ya hali kuzidi kuwa mbaya alilazwa Hospitali ya Kairuki (Mikocheni, Dar). “Hata hivyo, akiwa pale Kairuki hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, tukashauriwa apelekwe nchini India kwa matatizo hayohayao ya figo. “Baadaye alipata nafuu kisha akarejea nchini, lakini kiafya alikuwa amedhoofu. Pamoja na kupatiwa matibabu nchini India, alikaa muda kidogo akaanza tena kulalamika maumivu. 

“Ilibidi arejeshwe Hospitali ya Kairuki. Hapo ndipo madaktari wa Kairuki na Muhimbili wakasema apelekwe Afrika Kusini kwani ni karibu ukilinganisha na India. “Tangu hapo Ruge alilazwa na kupitia kwenye mateso makubwa ya kutetea uhai wake, akipita kwenye bonde la mauti hadi Mungu alipochukua roho yake.

 

“Kwa hiyo tangu mwezi Septemba (mwaka jana), Ruge hakurejea kwenye ubora wake zaidi ya kupitia mateso kwa takribani miezi sita sasa hadi kifo chake. “Inauma sana kwa sababu Ruge alikuwa na mchango mkubwa wa kimaisha hasa kwa vijana. Itoshe tu kusema taifa limepoteza rasilimali kubwa,” alimalizia kusimulia kwa uchungu mmoja wa viongozi hao wa Clouds Media Group.

 

UGONJWA WA FIGO

Ugonjwa unaotajwa kumuua Ruge ni matatizo ya figo kufeli kufanya kazi. Kwa mujibu wa Daktari wa Gazeti la Ijumaa, Dk Godfrey Chale, figo zina majukumu muhimu sana kwenye mwili wa binadamu. Kwanza, figo inaondoa sumu kutoka mwili wa binadamu na kusafisha damu na kutoa sumu zote. Kama figo haifanyi kazi vizuri, basi hii inaweza kusababisha mkusanyiko wa sumu katika mwili na inaweza kusababisha baadhi ya matatizo makubwa ya afya.

DALILI

Figo inafanya kazi nyingi muhimu katika mwili wa binadamu kama kuweka katika uwiano mzuri kiwango cha maji. Figo ina uwezo wa kusawazisha kiwango cha maji katika mwili wa binadamu na inashiriki katika kutoa kemikali kwa njia ya mkojo. Figo hufanya kazi ya kutoa taka mwilini, kazi kuu ni kusafisha mwili, kutoa sumu, chumvi na urea.

 

Kama kiwango cha oksijeni kitakuwa chini katika figo, itasababisha kuundwa kwa erythroprotein, homoni ambayo inachochea marrow katika mifupa (bone marrow). Hii ni muhimu sana katika kazi za figo, figo zinawajibika kwa kuweka uwiano sawa wa asidi katika mwili wa binadamu.

 

MAGONJWA YA FIGO

Kuna sababu nyingi tofauti zinazoweza kukusababishia ugonjwa wa figo na kushindwa kufanya kazi, magonjwa kama kisukari, Ukimwi na shinikizo la damu. Shinikizo la damu au presha ni moja ya sababu ya ugonjwa wa figo na hii ndiyo maana inapaswa kujaribu kuweka sukari katika damu na BP katika uwiano wa kawaida.

 

Kwa bahati mbaya dalili za ugonjwa wa figo zinaanza kuonekana katika hatua za mwisho za ugonjwa au wakati figo zinakaribia kabisa kushindwa au wakati ambao kuna protini nyingi kwenye mkojo. Kwa kawaida dalili za awali za matatizo ya figo haziwezi kugundulika, ni asilimia 10 tu ya watu wanaweza kujua kama wana ugonjwa wa figo.

 

ISHARA

Baadhi ya ishara za mwanzo za figo kushindwa kufanya kazi ni pamoja na kubadilika rangi kwa mkojo (mfano damu katika mkojo au kwenda haja ndogo mara kwa mara).

Pia kuwa na uchovu na kukosa nguvu, maumivu ya mgongo hasa juu ya kiuno usawa wa figo, kuvimba miguu au mikono, ukosefu wa umakini na ufafanuzi wa akili, kukosa hamu ya kula na kutokuwa na ladha katika kinywa, kushindwa kupumua vizuri na upele au chronic tingling.

 

JINSI YA KUZUIA

Magonjwa ya figo yanaweza kukuletea matatizo makubwa zaidi katika afya. Inapaswa kufanya mabadiliko katika milo yetu na maisha kwa jumla.

MAZISHI YA RUGE

Mwili wa Ruge uliwasili juzi, Machi 1, 2019 jijini Dar na kupokelewa na maelfu ya wakazi wa jiji hilo ambapo jana uliagwa katika Viwanja vya Karimjee, na leo utasafirishwa kwenda kwao Buko kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho Jumatatu, Machi 4.


Loading...

Toa comment