The House of Favourite Newspapers

HIZI NDIZO SIRI 5 UKIONA STAA KAPOZI NA NDINGA KALI !

IMEKUWA kawaida mtu ukiingia kwenye mitandao ya kijamii na kukutana na picha za mastaa tofauti kwa nyakati tofauti wakiwa wamepozi kwenye mikoko mikali. Ni jambo jema unapoona staa akiwa na mafanikio kutokana na sanaa yake. 

 

 Katika hali ya kawaida, kwa haraka mtu unapoona picha za namna hiyo, unajua moja kwa moja staa husika atakuwa mmiliki halali wa dinga hiyo. Naamini siyo jambo geni, mara kibao utakuwa umekutana na mastaa wakiwa na magari ya maana.

 

Jambo hilo huamsha ari kwa chipukizi kutamani kuingia katika sanaa husika wakiwa na lengo la kutusua kimafanikio. Lakini je, ni kweli mastaa wote wanaoonekana kwenye mitandao wamepozi na magari ni yao? Nimefanya uchunguzi usio rasmi kwa kuwahusisha wasanii ambao baadhi yao wamekataa kutajwa majina yao gazetini. Unazijua siri zenyewe nyuma ya ndinga za mastaa? Kama ulikuwa hujui basi leo nakujuza….

 

SIRI NAMBA MOJA

Imebainika kuwa, mastaa wengi wamekuwa na maisha fulani ya mitandaoni. Kwa kutaka sifa au kuonekana wapo vizuri, huamua kuazima magari kwa rafiki zao kisha kuosha nayo nyota kwa kupiga picha na kutupia mitandaoni. Mastaa wa aina hiyo wapo wengi, kutokana na kujulikana kwao na wadau mbalimbali, siyo ishu kwa msanii kuazima gari. Akipewa ndipo anapotumia upenyo huo kufotoa mapichapicha na kutupia mitandaoni.

 

CHEKI HII

Wapo wengine huamua kukodi katika kampuni mbalimbali za  kukodisha magari, kisha hutumia mwanya huo kujionyesha yupo matawi ya juu.

“Kaka asikudanganye mtu, sisi mastaa tunajuana. Kuna watu wanadanganya, eti filamu zinalipa. Siyo kweli, tena siku hizi mambo ndiyo yameharibika kabisa. Hivyo ili kujionyesha kwa mashabiki au kutafuta kiki, wengine huamua kukodi gari na kupiga nalo picha,” alisema mdau mmoja kisha akaongeza:

 

“Kukodi gari siyo dhambi, lakini tatizo ni pale utakapoiaminisha jamii kuwa ni usafiri wako, wakati siyo kweli. Tabia hii wanayo zaidi wasanii wa kike.”

 

HII NAYO DUH!

Kama mjuavyo mastaa wanapokuwa location wanarekodi filamu au video za muziki, magari huwa kama yote! Wapo baadhi ya mastaa hutumia mwanya huo kupiga picha kisha kwenda kuringishia mitandaoni. Akizungumza na Showbiz, Video Vixen mmoja alisema: “Hiyo siyo ya kuuliza kaka. Wewe jiulize, kama ni magari yao kwa nini hawaonekani nayo mitaani, wanaishia mitandaoni tu? Habari ndiyo hiyo.”

 

WAUZA SURA SASA

Hakuna mtu anayependa kitu kibaya, watu hutamani kuonekana wa maana kwenye jamii, hivyo uchunguzi wetu umeonyesha kuwa wapo mastaa ambao wakipita maeneo fulani ya shughuli na kuona ndinga kali, hujifotoa fasta kisha anairusha Insta bila caption!

 

Maeneo yanayotajwa zaidi kwa mastaa kupiga picha na magari ya watu wanapokuwa kwenye mitoko ni pamoja na sehemu zenye fukwe au hoteli kubwa wanazokutana mastaa kula bata au kwenye vikao vyao vya kikazi.

 

WAPO WANAOMILIKI KWELI

Hata hivyo, haina maana kwamba wasanii wote wanaorusha ndinga kwenye mitandao ya kijamii siyo yao. Uchunguzi umeonyesha kuwa wapo wasanii wakubwa ambao wanafanya vizuri kwenye sanaa na wanamiliki mikoko ya maana. Baadhi ya mastaa hao ni pamoja na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ali Kiba, Lulu Diva, Omari Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, Ney wa Mitego, Ambwene Yesaya ‘AY’, Judith Wambura ‘Jide’ wote wa Bongo Fleva.

 

Kwa upande wa wasanii wa filamu kuna Vincent Kigosi ‘Ray’, Kajala Masanja, Jacqueline Wolper, Jacob Stephen ‘JB’, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’, Lucas Mhuvile ‘Joti’, Husna Posh ‘Dotnatha’ na wengineo. Hata hivyo, mastaa wengi wenye ndinga kali, huwa hawapo busy kabisa kuonyesha mikoko hiyo kwenye mitandao. Wanaishi kawaida tu, wakipambana na kutoboa zaidi kisanii.

 

MASTAA KUWENI HALISI

Rais wa Shirikisho la Wasanii Tanzania ‘TAFF’ Simon Mwakifwamba ni miongoni mwa wasanii wanaopinga usanii wa mastaa katika maisha halisi. Alipata kuzungumza nami, akisema: “Tatizo sanaa imevamiwa na wauza sura. Wale wasanii halisi, angalia wanaishi maisha ya kawaida, lakini wale walioingia kwa malengo yao mengine, inabidi wajionyeshe sana mitandaoni.

 

“Mimi nawasihi wasanii wapambane kuinua sanaa badala ya kuonyesha usanii katika maisha ya kawaida. Maisha wanayoyaona Watanzania kwa mastaa wetu ni tofauti kabisa na ukweli halisi ulivyo.” Kuna haja gani ya kujionyesha unacho wakati huna? Ni vyema kuishi maisha halisi, muhimu ni kupambana na kuongeza ubunifu ili kukubalika zaidi kwa mashabiki na hatimaye kupata mafanikio yatakayokufikisha kwenye ndoto zako.

Comments are closed.