The House of Favourite Newspapers

HIZI NI IMANI POTOFU NA UKWELI KUHUSU UGONJWA WA JINO

MOJAWAPO ya mambo ambayo yanayowa-sumbua watu wengi ni dhana potofu kuhusu matatizo ya meno yanayouma. Lakini, jambo ambalo linashauriwa ni kuzingatia kanuni, taratibu ambazo zimewekwa na wataalamu wa kinywa ili meno yasiume au kuoza kwa watu wazima na watoto.  Mara nyingi imani potofu husambaa kwa kasi na huaminiwa na jamii kwa haraka. Hivyo, ni vyema kujua hizi imani potofu lakini pia kujua ukweli wa afya ya kinywa ili jamii ipate ufahamu sahihi kuhusu matatizo ya meno na tiba yake.

Baadhi ya imani potofu na ukweli ni kama ifuatavyo:-

1- Potofu: Using’oe jino au kufanya matibabu ya mzizi wa jino kama una uvimbe hasa usaha.

Ukweli: Kung’oa jino au matibabu ya mzizi wa jino yanasaidia kutoa nafasi/njia kwa usaha kutoka na hivyo kupona haraka pengine bila hata kuhitaji dawa.

2- Potofu: Usile kitu chochote unapokwenda kung’oa jino.

Ukweli: Njaa inaweza kukufanya uzirai katika zoezi la kung’oa jino, hofu ikichanganyika na sukari kidogo mwilini husababisha ubongo kushindwa kufanya kazi sawasawa. Imani hii potofu inahusishwa na sindano ya ganzi, watu wengi wanafikiri kila ganzi inatakiwa mtu awe amekula chakula kwa muda fulani. Hii kwa matibabu ya meno sio kweli kwani ganzi hutolewa kwenye eneo husika tu hivyo haiathiri mwili mzima.

Si meno yote yanayoonekana mazuri na imara ni mazima, mengine yanaweza kuwa yameoza katika maeneo usiyoweza kuona kama vile chini ya fizi na kwenye mizizi, si hivyo tu hata uoto mpya uweza kugundulika mapema kabla ya kufanya uaribifu mkubwa kama utachunguzwa na wataalamu mapema. Kumbuka pia mangonjwa ya mifumo mingine kama ukimwi, kisukari na mengine mengi hujidhihirisha mapema kinywani kabla mgonjwa hajapata dalili zingine.

3- Potofu: Njia ya uhakika ya kutibu jino ni kuling’oa.

Ukweli: Ziko njia nyingi na za uhakika za kutibu jino bila kung’oa. Kung’oa jino kama tiba ni pale tu ambapo jino hilo haliwezi tibika kwa njia yoyote na kukaa kwake kwaweza kuleta madhara zaidi. Kung’oa jino huleta madhara mengine na meno bandia pamoja na kwamba hayawezi kurejesha kazi za meno yaliyong’olewa kwa kiwango halisi, lakini pia utunzaji wake ni mgumu na gharama pia.

Hata hivyo, kama umelazimika kupoteza meno basi meno bandia ndilo chaguo pekee.

4-.Potofu: Kupiga mswaki mara nyingi na kwa nguvu huzuia kuoza kwa meno.

Ukweli: Si mara ngapi

unapiga mswaki na nguvu gani inatumika, suala ni unapigaje mswaki. Kupiga mswaki mara nyingi na kwa nguvu kunaweza kusababisha kukwangua sehemu ngumu ya nje ya jino, kulifanya laini na hatimaye kuuma au hata kuvunjika. Kupiga mswaki mara mbili, taratibu na kwa njia sahihi ndicho kinachosaidia meno kuwa na afya.

5-Potofu: Mama mjamzito hastahili kung’oa jino mpaka atakapojifungua.

Ukweli: Kumuacha mama mjamzito na maumivu pamoja na ugonjwa kwaweza kufanya ugonjwa kusambaa na kuingia kwenye ubongo hata kusababisha kifo cha mama na kiumbe chake. Pia maumivu makali yaweza kusababisha mimba kutoka.

6- Potofu: Huna haja ya kumuona tabibu wa meno kama hujaona au kuhisi una tatizo la meno.

Ukweli: Kila mtu anatakiwa kumuona tabibu wa meno angalau mara mbili kwa mwaka bila kujali meno yake yanaonekana vizuri au imara kiasi gani.

Comments are closed.