Homa ya mapafu kwa watoto (Pneumonia)

Leo tutajadili ugonjwa wa homa ya mapafu kwa watoto maarufu kama Pneumonia (Nimonia), ni aina ya maambukizi yanayoathiri mapafu.

Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio chini ya miaka 5 maisha yao hupotea kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.

Kuna aina kadhaa ya vimelea ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi katika mapafu. Vimelea hivi hujumuisha bakteria, virusi, parasaiti na fangasi.

Vimelea hivi hushambulia mwili wa binadamu kulingana na umri na kinga ya mwili wake. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa watoto wakubwa.

Baadhi ya vimelea wa bakteria wanaoshambulia watoto ni pamoja na Streptococcus Pneumonia, ambao ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto. Wapo pia Haemophilus Influenzae aina ya kundi B (Hib), ambao ni aina ya pili ya bakteria walio maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa ya mapafu kwa watoto.

 Staphylococcus Aureus ni aina nyingine ya bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wachanga. Kwa upande wa virusi, aina ya Respiratory Syncytial virus ndiyo wanaoongoza kwa kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.

Aidha, vimelea wa Pneumocystis Jiroveci ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasaiti ni maarufu zaidi miongoni mwa parasaiti wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini hususan watoto wenye virusi vya Ukimwi. Aina nyingine za bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na Mycoplasma Pneumonia na Chlamydia Pneumonia.

Kuna namna nyingi za kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa kawaida, virusi na bakteria hupatikana katika sehemu ya juu ya mfumo wa njia ya upumuaji yaani Upper Respiratory Tract. Inapotokea kinga ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yoyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji yaani Lower Respiratory Tract na hatimaye kushambulia mapafu.

Hali kadhalika, vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya kuzaliwa yaani kipindi cha mimba.

Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu

hutegemea umri wa mtoto. Kwa watoto wadogo, dalili za awali zinaweza kuwa homa kali pamoja na mtoto kuhangaika na kunyong’onyea. Watoto wanaozaliwa wakiwa na maambukizo ya bakteria aina ya Streptococcus kundi B wanaweza kuwa na homa na kupumua kwa shida.

Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na dalili ambazo si maalumu kama vile kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yoyote ya kushindwa kupumua. Hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.

Dalili za kawaida za homa ya mapafu ambazo huwapata karibu watoto wote wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja na kuwa na homa, kuhisi baridi na kikohozi. Kupumua kwa haraka kuliko kawaida na kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa kupumua.

Dalili nyingine ni mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa kupumua na pia maumivu ya tumbo.

Itaendelea wiki ijayo.

Loading...

Toa comment