Hongera Global TV, TPBO Ngumi Zinataka Haki Wanasubiri
KWANZA kabisa nichukue fursa hii, kuipongeza Kampuni ya Global Publishers kupitia runinga yake ya mtandaoni, Global TV Online, kwa kuweza kudhamini mchezo wa ngumi za kulipwa Tanzania ambao umeanza kupotea katika ramani yake.
Hii ni fursa kubwa ambayo haijawahi kutokea hapa nchini kwa TV ya mtandaoni kudhamini mapambano makubwa ambayo yalipewa jina la Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati. Mapambano hayo yalifanyika wikiendi iliyopita kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala Zakhem jijini Dar.
Wikiendi iliyopita tulishuhudia mabondia wa Tanzania, Idd Pialali, Nasibu Ramadhan na Francis Miyeyusho wakigombania mikanda ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati dhidi ya mabondia kutoka Malawi na DR Congo. Mapambano hayo yalisimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBO), chini ya rais wake, Yasin Abdallah ‘Ustaadh’.
Katika mapambano hayo yaliyohudhuriwa na Balozi wa Malawi, Hawa Ndilowe, bondia Nasibu Ramadhani alipambana na Yohane Banda wa Malawi na Nasibu alishinda kwa TKO ya raundi ya tisa kabla ya Idd Pialali kumchakaza Regin Champion kutoka DR Congo kwa majaji watatu kumpa ushindi. Jaji, Sakwe Mtulia alitoa pointi 99 kwa Pialali na Champion pointi 90, Ibrahim Kamwe alitoa 99-91 na Aga Peter alitoa 10090.
Licha ya Champion kulalamikia matokeo hayo lakini ukweli alizidiwa kwa kiasi kikubwa na Pialali kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kutupa makonde, pambano lao lilikuwa kali ambalo lilivutia mashabiki wengi. Lakini kwa upande wa Miyeyusho ambaye alicheza na Israel Kamwamba, mambo hayakuwa mazuri kwa upande wake kutokana na pambano lake kumalizika kwa sare ambayo ilipingwa na kila mdau aliyeshuhudia pambano hilo kutokea ukumbini na kwa wale ambao walifuatilia ‘live’ katika Global TV Online kupitia simu na kompyuta.
Niwapongeze Idd Pilalai na Nasibu Ramadhani kwa kuonyesha mchezo mzuri wenye ufundi mkubwa dhidi ya wapinzani wao ambao walikuwa imara vya kutosha mpaka kuweza kufanikiwa kuibakisha mikanda miwili ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati licha ya burudani kukosekana kutokana na ulingo kuteleza
kitu ambacho kimelalamikiwa na kila mdau wa mchezo huo.
Watanzania na dunia imeshuhudia uwezo wao na hakuna ambaye alipinga ushindi wa mabondia hao kwa kuwa walicheza vizuri na ngumi zilipigwa kweli, lakini haikuwa picha nzuri kuona majaji wa pambano la Miyeyusho dhidi ya Kamwamba wakishindwa kusimamia ukweli na haki.
Kilichotokea katika pambano hilo ni kitu cha aibu kwa taifa, ukweli Miyeyusho alionekana kuzidiwa kuanzia raundi ya kwanza hadi ya mwisho kwa kupigwa ngumi nyingi lakini mwisho wa siku majaji walitoa matokeo ya sare kwa pointi 95-95, 96-94, 95-95 kitu ambacho ni uongo mkubwa.
Ukweli ni kwamba pambano la ubingwa halina sare na Rais wa TPBO, Yasin Abdallah ‘Ustaadh’ ambao ndiyo walikuwa waratibu wa mapambano hayo walipaswa kutenda haki kwa bondia wa Malawi, kibaya zaidi ubabaishaji ulifanyika mbele ya balozi wa nchi yake ambaye alishuhudia pambano zima. Miyeyusho alipigika vibaya kama hali ya kubebana ikiendelea itapunguza fursa ya wadhamini kujitokeza kwa sababu haki inashindwa kusimamiwa pamoja na kufanya mabondia wa kigeni waogope kuja kucheza ngumi nchini kwetu.
STORI: IBRAHIM MUSSA | CHAMPIONI IJUMAA