The House of Favourite Newspapers

Hoteli Ya Mondi Yafungwa, Msimamizi Afunguka

0

MWAKA mmoja baada ya msanii mkubwa nchini Tanzania, Nasibu Abdul ‘Diamond Platumz’ kununua hoteli ya kifahari, hoteli hiyo imefungwa.

Katika pitapita zake, wikiendi iliyopita, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilifika kwenye hoteli hiyo ya nyota tatu iliyopo Mikocheni B jijini Dar na kukuta imefungwa.

 

Aprili, mwaka jana, staa huyo wa Wimbo wa Waah aliitambulisha rasmi hoteli hiyo kwa mashabiki wake kama sehemu ya kuwahamasisha kwamba, wakifanya kazi kwa bidii nao wanaweza kufikia mafanikio aliyoyafikia yeye.

 

Diamond au Mondi alisema kuwa, baada ya kuinunua ataitoa kwa muda kwa ajili ya kusaidia waathirika wa Corona (COVID-19) kukaa karantini, lakini baada ya hapo angeikarabati kisha kuwa hoteli ya kistaa zaidi jijini Dar.

 

Kama ujuavyo, binadamu hawakosi maneno hivyo baada ya kuona kimya, baadhi ya watu walianza kusema ilikuwa ni kiki.

“Sisi tulijua tu kuwa tumeingizwa chaka, Mondi hana ubavu huo wa kununua hoteli ya kifahari, tatizo ni kwamba anapenda sana sifa; yaani anapenda kujionesha kwa watu kuwa ana pesa wakati hana lolote.

 

“Haya, tangu kipindi kile alivyotuahidi kuwa atairerebisha hoteli hiyo hadi leo hakuna kitu,” kilidai chanzo kimoja.“Kila siku anaahidi au anasema amenunua vitu vikubwa, halafu havifanikiwi au baada ya muda unasikia siyo kweli, hivi tunavyoongea hoteli imefungwa, sasa kwa nini ifungwe wakati alisema anataka kuitengeneza ili iwe bora zaidi?” Alihojia mmoja wa mashabiki wa Mondi anayeishi jirani na eneo hilo ilipo hoteli hiyo.

IJUMAA WIKIENDA LASHUHUDIA

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilipofika kwenye hoteli hiyo lilishuhudia kwa macho yake kuwa imefungwa na hakuna huduma zozote zinazoendelea.

 

IJUMAA WIKIENDA lilibisha hodi kwenye hoteli hiyo na kufunguliwa na kijana mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mlinzi wa hoteli hiyo.

 

IJUMAA WIKIENDA: Naweza kumuona mhusika wa hoteli hii?

 

MLINZI: Bila shaka, subiri hapo nikuitie… Baada ya muda, mhusika alifika na kujitambulisha kuwa yeye ni msimamizi wa hoteli hiyo.

 

IJUMAA WIKIENDA: Nashukuru kukufahamu, mimi ni mwandishi wa Gazeti la IJUMAA WIKIENDA,tumesikia kwamba hoteli ya hii imefungwa, ni kweli?

 

MSIMAMIZI: Ni kweli hoteli hii kwa sasa haitoi huduma zozote zile kwa sababu ndiyo kwanza tunataka tuanze kuirekebisha hivyo kwa ufupi tumeifunga kwa muda mpaka pale tutakapomaliza marekebisho.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ohoo! Kwa hiyo mnatarajia kuanza lini marekebisho maana kuna watu wanadai eti Diamond aliwadanganya hii siyo hoteli yake….

 

MSIMAMIZI: Hajadanganya, hapana, hoteli hii ni ya Diamond na ilikuwa tuanze marekebisho tangu muda ila tumeshindwa kwa sababu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwa hiyo tunasubiri Ramadhani iishe na yeye arudi kutoka safarini (yupo Afrika Kusini) ndipo tuanze rasmi marekebisho.

 

Nadhani mwishoni mwa mwezi wa sita au wa saba, ndiyo tutaanza kuitengeneza na baada ya hapo tutarejesha huduma.

IJUMAA WIKIENDA: Kwani ikishafanyiwa marekebisho itaendelea kuwa hoteli?

 

MSIMAMIZI: Ndiyo, itaendelea kuwa hoteli kama kawaida.

IJUMAA WIKIENDA: Nashukuru sana kwa muda wako.

MSIMAMIZI: Karibu sana.

STORI; MEMORISE RICHARD, DAR

Leave A Reply