The House of Favourite Newspapers

Huddah Amtikisa Zari kwa Utajiri

DAR ES SALAAM: Huku wakidaiwa kuchukuliana mabwana, mrembo maarufu Afrika Mashariki anayetokea jijini Nairobi, Kenya, Huddah Monroe ametajwa kuwa miongoni mwa warembo ambao wana ukwasi wa kutosha unaomshtua zilipendwa wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.  Huddah ambaye ni modo matata nchini Kenya, anatajwa kuwa utajiri wa Dola za Kimarekani milioni 3 (zaidi ya shilingi bilioni 6.8 za Kibongo), utajiri ambao unakaribia kumkuta Zari ambaye ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 4.4 (zaidi ya shilingi bilioni 10 za Kibongo).

KWA NINI ANAMTIKISA?

Mitandao mbalimbali ambayo Gazeti la Ijumaa limechimba habari za mastaa hao, imemtaja Huddah kumtikisa Zari kwa kuanisha vigezo mbalimbali ambavyo endapo Zari asipokuwa makini, huenda akapitwa kwa utajiri.

KIGEZO CHA KWANZA

Kigezo cha kwanza ambacho kimetajwa kwenye mitandao hiyo ni pamoja na suala la umri ambapo imeelezwa kuwa, kiumri Zari ni mkubwa kuliko Huddah hivyo endapo kasi ya mrembo huyo wa Kenya ikiendelea kama ilivyo sasa, Zari ataisoma namba.

“Zari ana umri wa miaka 41, Huddah ana 25, sasa ukiangalia kwa umakini hapo tofauti kwanza ya utajiri siyo kubwa sana kwa kuangalia suala zima la umri,” mmoja wa wachangiaji alichangia mtandaoni.

KIGEZO CHA PILI

Kigezo kingine ambacho kimetajwa ni namna ambavyo wawili hao wameupata utajiri wao. Zari yeye utajiri wake umetokana pia urithi kutoka kwa marehemu mume wake, Ivan Semwanga wakati Huddah yeye ni wa kutafuta mwenyewe. Mitandao imeeleza kuwa, Huddah ana magari ya kifahari, majumba ikiwemo moja aliyomjengea mama yake mzazi nchini Kenya.

SIKIA TAMBO ZAKE…

Kuhusu magari, mara kadhaa Huddah mwenyewe amekuwa akijisifu kumiliki magari ya kifahari huku akieleza gari la kwanza kabisa alinunua akiwa na umri wa miaka 21.

“My first car at 21 was a Range Rover Sport that I turned PINK…PINK defines the Huddah brand…My second car was a White Range Rover Evoque. My 3rd car, a Black Audi Q7. All because I thought cars defined my value….!” Alinukuliwa Huddah akimaanisha;

“Gari lake la kwanza kununua lilikuwa ni Range Rover Sport alipokuwa na umri wa miaka 21 la rangi ya pinki, la pili lilikuwa ni Range Rover Evoque la rangi nyeupe. La tatu ni Audi Q7 la rangi nyeusi. Ninanunua magari haya sababu yanafanana na hadhi yangu.”

BIDHAA ZA UREMBO

Lakini kubwa kuliko yote, mitandao ya nchini Kenya imemtaja mrembo huyo mwenye mvuto wa aina yake, anatarajia kuingiza mkwanja mrefu kupitia kampuni yake ya bidhaa za urembo, Huddah Beauty.

Kampuni hiyo inazalisha bidhaa mbalimbali za urembo ikiwemo lipstick maarufu zinazofahamika kwa jina la Saint Lipstick ambazo zinatajwa kumuingizia fedha nyingi ambazo zitatunisha zaidi utajiri wake.

“Hizi bidhaa za urembo anazosambaza Huddah ni kama zile za mrembo kutoka Marekani Kylie Jenner ambaye anatajwa kuwa na utajiri wa kutisha kutokana na bidhaa hizo za urembo. Sasa unafikiri ndani ya miaka miwili au mitatu atakuwa wapi?” Alitoa maoni jamaa mmoja aliyejiita Ojuku mtandaoni.

ZARI AWE MACHO

Vyanzo mbalimbali mitandaoni vimeeleza kuwa, Zari ambaye sehemu kubwa ya utajiri wake unatokana na vyuo anavyomiliki pamoja na maduka, anapaswa kujiongeza zaidi kwani kwa siku za hivi karibuni, Huddah anakuja kwa kasi si kwa maana ya utajiri pekee, bali pia umaarufu wake ni mkubwa.

ALIPOTOKEA

Huddah ambaye dunia inamfahamu kwa shughuli za umodo, umaarufu wake ulichipuka zaidi mwaka 2013 baada ya kushiriki Shindano la Big Brother Africa msimu wa nane nchini Afrika Kusini.

UGOMVI NA ZARI

Mara kadhaa Huddah na Zari waliwahi kuingia kwenye vita ya maneno wakituhumiana kuibiana wanaume. Hivi karibuni, Huddah alidaiwa kujiachia huko Dubai na King Bae kiasi cha kumsababisha Zari kufunga safari kuwafuata na baada ya kuwakosa ugomvi mkubwa ukaibuka baina ya wawili hao.

Mwaka 2016, wawili hao walidaiwa kutibuana ile mbaya baada ya Huddah kutuhumiwa kuchepuka na Diamond huku akijua ni bwana wa shoga’ke huyo.

Stori: Stori: Erick Evarist, Ijumaa

Comments are closed.