Huduma za TRA Zarejea Katika Ofisi Zilizoharibiwa

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema huduma za TRA zimerejea katika ofisi zote Saba kwa nchi nzima zilizoathirika wakati wa uchaguzi tarehe 29.10.2025.
Ameyasema hayo Desemba 03.2025 alipotembelea ofisi mpya za TRA kituo cha Buguruni zilizopo Vingunguti jijini Dar es Salaam ambako huduma zimerejea baada ya ofisi za awali kuharibiwa wakati wa uchaguzi na kutoa pole kwa walipa kodi kwa changamoto za kufuata mbali huduma wakati wa ukarabati.
Kamishna Mkuu amesema baada ya ofisi za awali kuharibiwa hatua za haraka zilichukuliwa kurejesha huduma kwa ofisi zote Saba zilizoathirika kwa nchi nzima na hivi sasa ofisi hizo zinaendelea kutoa huduma kama kawaida.
Kuhusu usalama wa taarifa za Walipakodi Kamishna Mkuu Mwenda amesema taarifa za wateja zipo salama maana TRA imekuwa ikitumia mifumo kuhifadhi taarifa zake na mifumo hiyo haipo ofisini.
“Taarifa za wateja wetu wote zipo salama kabisa, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ametuwezesha kuwa na mifumo mizuri ya kidigitali ambayo imerahisisha kazi zetu sambamba na kutunza taarifa zote kidigitali” amesema Mwenda.
Kwa upande wao baadhi ya Walipakodi waliofika kupatiwa huduma katika ofisi za TRA Buguruni akiwemo Omar Abdubari, Omar Abdurahman na Nolasco Godfrey wamepongeza hatua ya kurejea kwa huduma katika ofisi hizo.
Aidha wamempongeza Kamishna Mkuu wa TRA kuwa kuwatembelea katika ofisi hizo hali inayowapa motisha ya kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
Ziara hiyo ya Kamishna Mkuu wa TRA katika ofisi za Buguruni ililenga kuangalia huduma waazopatiwa Walipakodi katika ofisi hiyo pamoja na kuzungumza Watumishi na Walipakodi.

