The House of Favourite Newspapers

HUKU AKIENDELEA NA MATIBABU, ALI CHOKI TUMUOMBEE

HALI ya staa wa muziki wa Dansi nchini, Ali Choki ambaye amelazwa katika Hospitali ya Bugando, Mwanza bado haijatengemaa ambapo madaktari wamekuwa wakipishana kitandani kwake hivyo tuzidi kumuombea, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.  Chanzo makini ambacho kilimtembelea hospitalini hapo juzi kilidai kwamba hali ya mwanamuziki huyo bado siyo nzuri licha ya kwamba ameshatolewa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua ‘oxygen’ na kuanza kuongea lakini bado yupo vibaya.

“Choki hali yake bado siyo nzuri maana kaka yake alikuja Mwanza kwa ajili ya kumchukua wamhamishie Muhimbili lakini kutokana na hali aliyonayo, madaktari wamemtaka asubiri kwanza kwa siku chache hizi akipata nguvu ndiyo asafiri,” kilidai chanzo hicho.

MADAKTARI WAPISHANA

Kutokana na hali aliyonayo Choki chanzo kinazidi kudai kwamba madaktari wanapishana kitandani kwake kwa ajili ya uangalizi maana wanahofia anaweza kuzidiwa zaidi kama mwanzo.

USIRI WATAWALA

Chanzo hicho kilizidi kueleza kwamba kuugua kwa Choki kumetawaliwa na usiri mkubwa kwani familia hata uongozi wa bendi mpya aliyoenda kufanya kazi huko Mwanza hawataki kumzungumzia wala kuruhusu watu wengine kwenda kumuona hospitalini.

“Wale watu wa karibu ndiyo wanaoruhusiwa kumuona Choki maana yuko kwenye wodi binafsi, familia hawataki watu wengine wamuone hata kumzungumzia hawataki, wanafanya kuwa ni siri sijui kwa nini,” kilidai chanzo.

RISASI LAMSAKA MENEJA WAKE

Risasi Mchanganyiko.. ili kujua hali ya Choki inaendeleaje lilimtafuta mwenyewe kwa njia ya simu lakini haikuwa hewani ila lilifanikiwa kuzungumza na meneja wake, Juma Kasesa ambaye alieleza kuwa kwa sasa hali ya mwanamuziki huyo inaendelea vizuri na anaendelea kutengamaa kila siku.

“Choki anaendelea vizuri kwa sasa, nimewasiliana na kaka yake aliyemfuata huko hospitalini Bugando ambapo alieleza kuwa kwa sasa anaongea tofauti na mwanzo alikuwa na hali mbaya, alikata kauli na kupumulia mashine. “Familia inafanya utaratibu wa kumleta Dar kwa ajili ya matibabu zaidi ambapo madaktari wamempa siku kadhaa ili waangalie afya yake akipata nguvu ndipo asafiri.

“Madaktari walisema watatoa taarifa kwa ndugu kama anaweza kusafiri au laa leo jioni (Jumatatu iliyopita) na siku hiyo ndiyo walimtoa kwenye chumba cha uangalizi maalum alikokuwa na kumrudisha kwenye vyumba vya wagonjwa wa kawaida ila ‘private’ maana hatutaki asumbuliwe na watu kwa kuwa anahitaji kupumzika,” alisema Kasesa.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.