Hukumu Kesi ya Anayedaiwa Kumuua Mkewe Kisha kuuchoma moto Mwili Na Magunia ya Mkaa leo – Video
Kesi ya mauaji dhidi ya mfanyabiashara Hamisi Luwongo, anayedaiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kisha kuuchoma moto mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam imepanga kutoa hukumu leo Februari 26, 2025.
Katika kesi ya msingi ya jinai namba 44/2019, Hamisi, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, Dar es Salaam anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Naomi Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Anadaiwa alimuua mkewe Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku, baadaye akaenda kuzika masalia ya mwili huo na majivu shambani kwake na kupanda migomba juu yake.
Upande wa mashtaka ulifunga ushahidi Novemba 18, 2024 baada ya kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo tisa, huku upande wa utetezi ukiufunga Novemba 19 baada ya kumuita shahidi mmoja ambaye ni mshtakiwa mwenyewe, bila kuwasilisha kielelezo chochote.
Mshtakiwa katika utetezi wake alikana kumuua mkewe akidai hajafa bali alitoroka na kwamba, taarifa alizowaeleza Polisi kuwa alimuua na kuchoma moto mwili wake akazika majivu na masalia yake shambani hazikuwa za kweli.
Alidai aliwadanganya ili kujinusuru na mateso ya kipigo kutoka kwa askari polisi waliomtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.