The House of Favourite Newspapers

Hussein Machozi: Kuna Maisha Nje ya Muziki

0

Makala: Ojuku Abraham| RISASI MCHANGANYIKO| RISASI VIBES

MIONGONI mwa wasanii ambao walipata kuliteka soko la Muziki wa Kizazi Kipya ‘Bongo Fleva’, lakini wakafanya makosa ya kiufundi hivyo kushindwa kupaa kama ilivyotarajiwa, ni Hussein Rashid Juma ‘Machozi’.

Ni kati ya wasanii ambao wamefanya kazi nyingi na kupata bahati ya kubamba vilivyo kitaa, lakini ghafla, akaanza kufifia kiasi kwamba leo anaonekana kama mkongwe anayejaribu kurudi. Nani amesahau kile kibao cha Utaipenda?

Siyo hicho tu, bali pia alifanya kazi kibao, kama Kwa Ajili Yako, Maji Yakisha-mwagika, Kafia Gheto, Promise, Nieleze, Mikoba, Full Shangwe na Unanifaa kuzitaja kwa uchache. Kimya cha Hussein kimesababishwa na mambo mengi, ikiwemo kuondoka kwake nchini na kuelekea Italia, yaliko makazi yake kwa sasa.

Risasi Vibes lilimtafuta na kufanya naye mahojiano kuhusu mambo mbalimbali kama ifuatavyo;

Swali: Mambo vipi mzee?

Machozi: Poa kaka, nambie!

Swali: Ni kama sikuoni hivi siku hizi, au macho yangu?

Machozi: Yaa, ni kweli, sipo Bongo siku hizi.

Swali: Uko wapi na unafanya nini?

Machozi: Nipo Italia, nasoma mambo ya mawasiliano kwa muda wa miaka mitatu, huu ni mwaka wangu wa kwanza.

Swali: Lakini ungeweza kusoma hapa nyumbani kozi hiyo?

Machozi: Ndiyo, ningeweza kusomea hapa nyumbani, tena kwa wiki moja tu. Lakini nimekwenda kule kwa sababu wenzetu wako makini zaidi kwenye haya mambo na ukizingatia mimi ni mtundu kidogo kwa siku nyingi katika mambo hayo.

Swali: Vipi tena kusoma, ina maana muziki basi?

Machozi: No, bado nafanya muziki lakini hakuna mtu anaimba hadi anazeeka. Kuna maisha baada ya muziki. Ukitegemea muziki peke yake, siku ukiacha kila kitu kinasimama. Mimi sitaki kuajiriwa, elimu ninayopata ni ya kudumu, ninaweza kuitumia hata nikiwa naburuza miguu.

Swali: Nimeona video ya wimbo wako mpya, hongera sana, unaitwaje?

Machozi: Asante, unaitwa Nipe Sikuachi

Swali: Nikiutazama, naona kama umetoka katika line yako, umeweka zaidi sebene?

Machozi: Ni kweli, mashabiki ndiyo waliotaka nifanye hivyo, wanataka nyimbo za kuchezeka.

Swali: Video inaonekana kufanyika Ulaya, vipi na audio ulifanyia huko?

Machozi: Video imefanyika Italia lakini audio nilifanyia hapahapa kwa Marco Chali.

Swali: Muziki umebadilika, vijana wako vizuri, utaweza kupenya kwa ngoma hii?

Machozi: Nitatoboa kabisa, nimejipanga vizuri, ule ujanjaujanja wa vijana naujua na safari hii siwadharau hata kidogo.

Swali: Una mchumba Mzungu, ulimpataje?

Machozi: Ilikuwa Mombasa kwenye shoo, miaka kama mitatu hivi iliyopita, baada ya shoo akaja msichana mmoja Mtaliano akasema amependa kazi yangu, tukabadilishana namba, tukawa tunawasiliana.

Baadaye yule msichana akanitambulisha kwa dada yake, tukawa tunawasiliana pia. Sasa siku moja dada mtu akamuuliza mdogo wake kama ana uhusiano wa kimapenzi na mimi, akasema hapana, basi akamwambia yeye amenipenda, tukaanza uhusiano.

Swali: Kule Italia unaishi mji gani?

Machozi: Ninaishi Torino, ambako huku tunasema Turin.

Swali: Wewe ni shabiki wa soka? Ulitazama mechi ya Juventus na Barcelona katika Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Machozi: Aisee, watu wote wa ule mji ni mashabiki wa Juventus na bahati nzuri mimi mwenyewe pia ni shabiki mkubwa sana wa Bibi Kizee. Nilinunua tiketi ile mwezi mmoja kabla ya mechi.

Lakini rafiki yangu ile mechi sikwenda nikaishia kuangalia kwenye tv. Unajua baba mkwe (baba wa mchumba wake) ni shabiki hasa wa Juve, akaja akaniambia yeye amepigana amekuta tiketi zimeisha, anaomba nimpe yangu aende, basi akaichukua!

Leave A Reply