The House of Favourite Newspapers

Hussein Machozi: Nilizimia wakajua nimekufa, wakajiandaa kunizika

0

husseinmachoziHussein Machozi.

MCHEZO wa soka una matukio mengi, yapo ya kuhuzunisha na ya kufurahisha. Yapo yanayokatisha uhai wa mchezaji au kumsababishia kuacha kabisa kucheza soka.

Wanasoka wamekuwa wakikumbana na matukio hayo ya kutisha wakiwa ndani ya uwanja ambayo hutokea bila ya kutarajiwa. Mifano ipo mingi kuanzia soka la hapa nyumbani na hata nje ya mipaka ya Tanzania.

Mwaka 2003 mchezaji wa Cameroon, Marc Vivien Foe, alianguka uwanjani ghafla na kupoteza maisha wakati akiipigania timu yake ya taifa ilipokuwa ikicheza dhidi ya Colombia katika michuano ya Kombe la Mabara.

Hivi karibuni, timu ya vijana ya Coastal Union ya Tanga ilimpoteza mchezaji wake akiwa uwanjani baada ya kugongana na mwenzake katika harakati za kuwania mpira.

Pia mchezaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi alikumbana na tukio kama hilo msimu uliopita baada ya kupigwa kiwiko na beki wa Azam FC, Aggrey Morris na kusababisha kupoteza fahamu, lakini alipopatiwa matibabu aliamka.

Msanii wa Bongo Fleva ambaye aliwahi kucheza soka kabla ya kuanza kung’ara kupitia nyimbo zake za Full Shangwe, Utaipenda, Kafia Gheto na nyingine, Hussein Machozi naye yaliwahi kumkuta makubwa.

Mbali na muziki, lakini ni mmoja kati ya wasanii ambao wana vipaji vya kucheza soka. Machozi anafunguka kuhusiana na tukio ambalo hatalisahau katika maisha yake:
“Kuna siku nikiwa mkoani Kagera katika uwanja wa mazoezi wa Kagera, wakati huo nilikuwa nikiichezea Kagera Sugar B, tulikuwa tunafanya mazoezi, kama kawaida, ikatokea kona, katika harakati za kuupiga mpira nikagongwa sehemu ya nyuma ya kichwa na mwenzangu, basi palepale nilipoteza fahamu na kuanza kutoka damu puani, masikioni na mdomoni.

11887107_489827214528874_218821705_n“Kwa jinsi nilivyosimuliwa, ni kuwa baada ya tukio lile nilikimbizwa Hospitali ya Kihaka muda huohuo huku wengi wakiamini kuwa labda nimefariki, nilipofikishwa hospitalini, daktari aliyenipokea naye aliamini nimeshapoteza maisha akalipitisha hilo kuwa nimeshafariki dunia.

“Zikaanza taratibu za mwili wangu kupelekwa monchwari, wakati hayo yanafanyika mimi sikuwa na fahamu kabisa nikiwa nimefikishwa eneo la tukio na tayari nimewekwa pamba masikioni na puani, hapo nikawa nasubiri nichomwe sindano kabla ya mwili wangu kuhifadhiwa.

“Kabla sijachomwa sindano, ghafla nilishtuka na kujikuta nipo sehemu ambayo sijielewi, basi nikaanza kutoa zile pamba ambazo zilikuwa puani na masikioni.

“Wakati naendelea na zoezi hilo, akili ilikuwa haijakaa sawa, kile chumba nilimowekwa aliingia nesi akiwa na vifaa vyake, ile kuniona vile tu akaanza kukimbia, mimi pia nikatoka nduki, hapo akili ilikuwa haipo kabisa, nikawa nakimbia na yule nesi naye akawa anakimbia mpaka tukatoka nje huku nikiwa bado sijielewi.

“Hatua kadhaa mbele nilimuona mama fulani sijui alikuwa nesi yule, hata sikumbuki vizuri, akatoa kanga anifunike kwa kuwa nilikuwa mtupu, sikumjali. Akatokea rafiki yangu mmoja akaniambia kuwa sijavaa nguo, ndiyo nikashtuka na hapo ndipo akili zikawa kama zimerudi ghafla.

“Nikafunikwa palepale na ile kanga, cha kwanza kabisa nikaomba simu nimpigie mama yangu maana naye alijua tayari nimefariki, nyumbani walianza kuweka msiba wangu. Ajabu yule daktari aliyethibitisha nimefariki alitoweka pale hospitali na mpaka leo hii haijulikani yuko wapi.”

Leave A Reply