HUSTAHILI KUTESEKA KWA AJILI YA MAPENZI , CHUKUA HATUA -2

NI WIKI nyingine ninapokukaribisha msomaji wangu, wiki iliyopita tulianza kuielezea mada ya hapo juu kama inavyojieleza. Nilikusimulia kwa kifupi kuhusu mkasa uliomtokea dada yetu ambaye pia ni msomaji wa siku wa safu hii, akieleza jinsi mwanaume aliyekuwa akimpenda alivyokuwa anamtesa. Leo tunaendelea kuangalia mbinu za namna ya kuondokana na dharau, manyanyaso na mapenzi kutoka kwa mtu umpendaye. Nilikueleza kwamba unapoishi kwenye uhusiano ambao muda wote unakufanya ujihisi kukosa amani, kukosa furaha na kujawa na majuto, unatakiwa kuchukua hatua.

Upo ushahidi wa watu waliofikia maamuzi maishani mwao, wengine wakiyakatisha maisha yao kutokana na kunyanyaswa na wapenzi wao, wengine wakiuawa na watu waliowapenda kwa sababu ya kuvumilia manyanyaso ndani ya nyumba.

Narudia tena, ni makosa makubwa kumvumilia mtu anayekunyanyasa eti kisa unampenda. Unaweza kumvumilia mtu ambaye hana fedha kwa sababu tatizo lake siyo kwamba hakupendi, anakupenda lakini anashindwa kukutimizia unachokihitaji, lakini huwezi kumvumilia mtu anayekupa kila kitu, lakini akawa anakupiga, anakutukana hovyo, anakudhalilisha na kukufanyia kila aina ya jambo baya.

Kwa hiyo kama upo kwenye uhusiano wa aina hii, hatua tatu za mwanzo za kujikomboa ni zile nilizokutajia mwanzo, tafuta mtu unayemuamini, msimulie magumu unayopitia, hatua ya pili anza kupata muda wa kukaa peke yako na kupunguza ukaribu naye kwani kadiri unavyozidi kumganda ndivyo atakavyokuwa anazidi kukutesa na hatua ya tatu jipe muda wa kutafakari kwa kina hatima ya mapenzi yenu.

Kwa kawaida, mtu aliyezoea kukufanyia mambo mabaya, anapoona unaanza kukwepa kuwa karibu naye, hata kama ni jeuri kiasi gani, lazima taa nyekundu itawaka kwenye kichwa chake na kama anakuhitaji, lazima ataanza kuonesha mabadiliko fulani.

Ukiona hilo pia halijasaidia chochote, utakuwa na nafasi ya kuchagua nini unataka katika maisha yako. Unashauriwa kwamba unapokuwa wakati huu wa kuchagua kama uendelee kuwa naye au ufanye maamuzi magumu, ni vizuri ukajipa muda wa kutosha. Unaweza hata kusafiri kwenda mazingira tofauti, kama kuwatembelea ndugu na jamaa wanaoishi mji mwingine.

Ukishajipa muda wa kutosha, hatua inayofuata inakuwa ni kuzungumza na mhusika. Unaweza kuzungumza naye ukiwa mbali naye kwa sababu kama alishazoea kukudhalilisha, atakaposikia kwamba unataka kuachana naye, anaweza kukudhuru. Zungumza naye, mweleze kwa nini umeamua kutoka katika maisha yake, mkumbushe mambo yote mabaya anayokufanyia ambayo huyapendi.

Kwa mtu mwenye akili, kama bado anakuhitaji lazima atakuwa tayari kubadilika ili asikupoteze, lakini ukiona umefanya yote hayo, lakini bado mtu haoneshi kujali, tambua kwamba huyo hakupendi kabisa na anaweza kukufanyia mambo mabaya zaidi kama utaendelea kumchekea, chukua hatua mara moja kwa sababu mlango mmoja unapojifunga mwingine unafunguka.

Kama ataonesha kujali na kuonesha kwamba hayupo tayari kukupoteza, mnapaswa kukaa chini na kuelekezana upya namna ya kuendesha maisha yenu, yaani inakuwa ni kama vile mna-renew mkataba. Lazima mkubaliane mapema kwamba muishi vipi ili kesho na keshokutwa yasijirudie kama yale. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.


Loading...

Toa comment