HUSTAHILI KUTESEKA KWA AJILI YA MAPENZI, CHUKUA HATUA

NI WAKATI mwingine mzuri ninapokukaribisha mpendwa msomaji wangu na mada tutakayoijadili leo ni kama inavyojieleza hapo juu. Nimekuwa nikipokea ujumbe kutoka kwa wasomaji wangu mbalimbali, ambao wanawalalamikia wapenzi wao, kwamba licha ya kuwaonesha mapenzi ya dhati na kujitoa kwa kila kitu, wanachoambulia ni mateso ya moyo kila kukicha. Yawezekana na wewe upo kwenye uhusiano wa namna hiyo, unajitahidi kufanya kila kitu kwa ajili ya mpenzi wako, unajitolea kwa moyo wako wote kumpenda, kumheshimu na kumfanya awe mwenye furaha, lakini mwenyewe hajali.

Wapo baadhi ya watu ambao wanapojua kwamba wanapendwa, basi wanatumia upendo huo kama silaha ya kuwachapia wale wanaowapenda na hali hiyo imesababisha wengi kuishi kwa tahadhari, hata kama anakupenda hawezi kukuonesha kwa sababu anajua utatumia upendo huo kama silaha ya kumchapia! Unaishi na mtu ambaye anajua kabisa kwamba unampenda kwa moyo wako wote na umejitahidi kumuonesha jinsi alivyo muhimu katika maisha yako, lakini matokeo yake anakuwa ndiye mtu anayekusononesha moyo wako na kukutoa machozi kila kukicha.

Wakati mwingine hutakiwi kuvumilia na kufa na tai yako shingoni katika uhusiano wa namna hii, lazima utafute mbinu za kumaliza tatizo na kama ikishindikana kabisa, basi ni bora umwache aende kwa sababu ukiendelea kung’ang’ania, yatakuja kukutokea makubwa zaidi na kukuacha na majuto maisha yako yote. Unapojikuta upo kwenye uhusiano ambao unakuumiza, unakutesa, unalia kila siku na unahisi kama huna tena thamani, jambo muhimu la kwanza ni kutafuta mtu ambaye unamuamini na kumheshimu, uzungumze naye na kumueleza hali unayoipitia.

Wakati mwingine unaweza kuwa unateseka sana, lakini kwa vile unampenda unaamini kwamba ipo siku atabadilika, atakutolea maneno machafu, atakufanyia vitendo vya kiudhalilishaji na kukunyanyasa, lakini hutaweza kujitoa mwenyewe hadi usaidiwe. Lazima mtu unayemfuata kwa ajili ya ushauri, uwe kweli unamuamini na mwenye busara, achana na wale wanaoishia tu kusema ‘ndoa ndivyo zilivyo’. Ndoa inapaswa kuwa kitu cha furaha, yule umpendaye ndiye mtu pekee anayepaswa kukubembeleza, udeke na akudekeze, akupende na akuoneshe thamani yako, hata pale watu wengine wote wanapokuona huna thamani.

Inapokuwa tofauti, basi hiyo inakuwa siyo ndoa tena. Kwa hiyo kama nilivyosema, hatua ya kwanza unatakiwa kumshirikisha mtu wako wa karibu, baada ya hapo, unatakiwa kuanza kujipa muda wa kuwa peke yako ili utafakari kwa kina hatima ya uhusiano wenu. Unapojipa muda wa kutosha wa kukaa peke yako, kwanza unamfanya hata yule anayekudharau aanze kujiuliza mara mbilimbili kwa nini unaonesha mabadiliko ya kitabia? Lakini pia unapojitenga na mtu anayekufanya muda wote ujisikie vibaya, unaanza kupata nguvu mpya za kupambana na matatizo yanayokukabili.

Hutakiwi kuwa na haraka ya kufanya uamuzi na ndiyo maana nakusisitiza kwamba ni lazima ufuate mbinu zote, hatua kwa hatua na ujipe muda wa kutosha ili hata ukija kufikia uamuzi wa mwisho, uwe ni uamuzi sahihi kwa sababu tayari utakuwa umejipa muda wa kutosha kutafakari kila kitu kwa kina.

Itaendelea wiki ijayo.


Loading...

Toa comment