The House of Favourite Newspapers

HUWEZI KUAMBUKIZWA / KUAMBUKIZA VIRUSI VYA UKIMWI KWA NJIA HIZI


KUNA imani potofu kwamba kupata maambukizi ya Ukimwi ndiyo mwisho wa maisha. Hii si kweli, kwa kupima na kujitambua mapema na kuanza kutumiwa dawa za ARV, kutakufanya kuishi maisha marefu yenye afya njema kwa muathirika. Wala huwezi kuambukizwa Ukimwi kwa kuumwa na mbu, kwa jasho, kuchangia vyoo, vifaa vya gym, bwawa la kuogelea au kuchangia taulo.
Huwezi pia kuambukizwa Ukimwi kwa kwenda shule pamoja au kuwa na rafiki mwenye Virusi Vya Ukimwi (VVU), kupiga chafya au kukohoa, kushikana mikono, kukumbatia au kupigana busu kavu na mtu mwenye Virusi Vya Ukimwi na kuvuta hewa moja na mtu mwenye Virusi Vya Ukimwi.

Ieleweke pia kwamba huwezi kumtambua mwathirika wa Ukimwi kwa kuangalia kwa macho. Watu wengi hawana dalili yoyote ya maambukizi ya Ukimwi japokuwa wana virusi kwa miaka kadhaa. Hivyo, njia pekee na ya uhakika kujua kama mwenza wako kama ana maambukizi au la, ni kupima nyote. Na sasa hivi upimaji wa HIV umerahisishwa zaidi na unatolewa bila gharama yoyote.
Tohara kwa wanaume inazuia kabisa maambukizi ya Ukimwi. Ukweli ni kwamba, tohara inapunguza hatari ya maambukizi ya virusi ya Ukimwi kwa kiasi kikubwa kama ilivyoandika hapa, lakini si kweli kwamba inazuia maambukizi.

Ieleweke pia kwamba hadi sasa bado hakuna tiba ya ugonjwa wa Ukimwi. ARV husaidia kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi. Hivyo matumizi bora ya ARV hufanya virusi kufubaa na kushindwa kuzaliana hivyo kumuwezesha mtu anayeishi na virusi kuisha maisha marefu na yenye afya, lakini si kweli kwamba zinatibu ugonjwa wa Ukimwi.
Wenye Ukimwi wana uwezo wa kupata mtoto ilimradi viwango vya virusi (viral load) ikiwa ipo chini na imechungwa vyema ndani ya miezi sita. Wenza ambao mmoja ana maambukizi na mwingine hana, wana uwezo wa kutumia njia ya tendo la ndoa kwa ajili ya kupata ujauzito, lakini wanatakiwa kuzingatia viwango vya virusi (viral load).


Hivyo basi, unashauriwa kupima na kuongea na washauri nasaa au madaktari watakaofuatilia wingi wa virusi na kukushauri muda muafaka wa kushika ujauzito.
Dawa za kufubaza makali ya ugonjwa wa Ukimwi husababisha virusi hivyo visiendelee kuzaliana na kama havitaendelea kuzaliana, basi seli za kinga za mwanadamu zitaishi kwa muda mrefu na kusababisha mwili kutengeneza ulinzi thabiti kukukinga na magonjwa nyemelezi.

Kimsingi Virusi Vya Ukimwi hushambulia seli hizi, hivyo wingi wake huwa ni tishio kwa seli na hata husababisha mwili wa binadamu kupoteza uwezo wake wa kupambana na magonjwa na ndiyo sababu mtu aliyeathirika na Ukimwi na hatumii dawa za kufubaza makali, hunyemelewa na magonjwa ya mara kwa mara na hata kuzorotesha afya yake.Matumizi bora ya dawa hizi husaidia kupunguza idadi ya virusi kwenye mwili kwa kuwa hawaendelei kuzaliana, hivyo hupunguza sana uwezekano wa wewe kumuambukiza mtu mwingine.
Mtu anayetumia dawa za ARV kwa ufasaha kama alivyoelekezwa na daktari huku akiishi maisha yenye kuzingata afya bora (mazoezi na chakula bora), uwezekano wa kumuambukiza mtu mwingine ambaye hana Virusi Vya Ukimwi unapunguzwa kwa asilimia 96.

USHAURI MUHIMU
Nenda kapime kujua hali ya afya yako na kama utagundulika umeambukizwa, uanze kutumia dawa za ARV mapema iwezekanavyo kwa afya bora na kuzuia maambukizi kwa umpendaye.
Kwa kujikumbusha tu ni kwamba Ukimwi ni ugonjwa unaosababishwa na Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi). Ugonjwa huu husababishwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Njia kubwa inayosababisha maambukizi ya ugonjwa huu ni ngono zembe. Hadi sasa, bado hakuna tiba ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini kuna dawa zinazotumika kupunguza makali ya ugonjwa huu (ARV) hivyo matumizi ya mapema ya ARV yatakuwezesha kuishi ukiwa na afya njema na ndiyo sababu tunahimizwa sana kupima afya zetu ili kujitambua na kuchukua hatua mapema. Ingawa maarifa ya ugonjwa huu ni mengi, ila bado kumeendelea kuwa ni changamoto kubwa katika jamii yetu na nchi nyingine zinazoendelea. Moja ya changamoto hizi ni imani potofu iliyojengeka katika jamii inayowanyanyapaa wagonjwa wa Ukimwi hivyo watu kuogopa kupima kwa kuwa wakishajulikana watanyanyapaliwa. Hii hurudisha nyuma harakati za mapambano ya ugonjwa huu.

Comments are closed.