The House of Favourite Newspapers

Huyu Naye…fuata Maelekezo – 02

0

“Naweka baba, nisamehe sana.”

“Usijali, weka.”

Baba alisimama kwenye mlango wa bafuni, nikachota maji na kuingiza bafuni, wakati natoka ili yeye aingie akanishika mkono na kuniita kwa sauti ya chini sana…

“Jamila…”

TAMBAA NAYO MWENYEWE…

“Abee…”

“Mimi nani?”

“Baba au bosi wangu.”

“Kama nilivyokwambia, mvumilie sana mama Rehema, sawa Jamila?”

“Sawa baba.”

Niliondoka hapo nikiwa na nguvu mpya na ya ziada. Hata kama mama mwenye nyumba hanipendi lakini mume wake kanikubali.

Baada ya baba kuondoka kwenda kazini, nikabaki na mama sasa maana yeye alikuwa si mfanyakazi, mama wa nyumbani. Afadhali hata angekuwa na kibarua chochote mjini ili niwe huru…

“We Jamila,” aliniita mama Rehema…

“Abee…”

“Nguo utafua saa ngapi wewe?”

“Nikimaliza kunywa chai mama…”

“Yaani kunywa chai ndiko kulikokuleta hapa kwangu siyo?”

“Hapana mama…”

“Sasa? Nenda kafue kule.”

Nilitoka jikoni na kikombe cha chai mkono wa kushoto, mkono wa kulia kipanda cha mkate. Nilifika nje na kuanza kufua huku nakunywa chai…

“Ole wako zisitakate sasa,” alisema mama Rehema.

Nikiwa nafua mama aliniita, nikainuka kwenda kumsikiliza.

“Abee mama!” niliitikia wito wake.

“Abee mama,” mama alifuatisha kauli yangu huku kaibana pua yake.

Wakati nikijiuliza nilikuwa nimekosea nini mama alianza kunifokea akisema kwa nini niliacha sabuni ya kuogea kwenye maji.

Swali lake lilinishangaza sana kwa sababu tangu nilipoamka sikuingia bafuni zaidi ya baba.

Kabla sijajitetea alinishambulia kwa maneno makali kwamba pale kwake hapakuwa na kiwanda cha sabuni hivyo niache kumpa hasara.

Akanisogelea na kunivuta sikio la kushoto na kuniambia ole wangu nirudie upuuzi huo, kisha akanitaka nikaendelee kufua.

Nilikwenda kufua huku nikiwa sina raha. Nilifua mpaka ikafika mahali nikasema kama ataziona hazijatakata, potea kwa mbali bwana!

“Ufanye haraka ukanunue mboga. Siyo unafua kama mikono imelemaa,” mama Rehema alinizukia na kuniambia maneno hayo.

“Sawa mama.”

“Sawa mama,” mama Rehema alirudia maneno yangu huku akiwa amejibana pua na mkono hivyo sauti kutoka kwa tabu kama vile eti mimi ndiyo sauti yangu kama alivyofanya awali.

Nilimaliza kufua, nikaenda kununua mboga, niliporudi nikaanza kupika. Nilipomaliza, nikamtengea mezani, akakaa kula kama kapika yeye…

“Jamila,” aliita…

“Abee mama…”

“Maji ya kunywa siyo ya baridi mbona?”

Nikampelekea maji ya baridi huku moyoni nikisema…

“Wenzako wanaogopa vitu vya baridi we unang’ang’ania ndiyo maana litumbo linafutuka.”

“Jamila…”

“Abee mama…”

“Chumvi…kila siku nakwambiaga chumvi lazima iwemo kwenye kisosa pembeni.”

Nilichukua kisosa, nikaweka chumvi nikampelekea huku nikisema moyoni…

“Kesho na keshokutwa useme una ugonjwa wa presha kumbe ni haya machumvi yako.”

“Hebu lete na mapapai.”

“Sawa mama.”

“Halafu kuna zile nyama zilibaki jana usiku, pasha moto lete vipande vinne.”

“Sawa mama.”

Nilikwenda jikoni huku naguna moyoni…

“Mama anakula huyu! Vitu alivyoagiza hata watu watatu hawawezi kumaliza,” nilisema mwenyewe…

“Halafu ule mchemsho wa usiku si upo?”

“Upo mama.”

“Lete.”

“Mh!” nilijikuta nimeguna kwa sauti…

“We Jamila njoo hapa…kwa nini umeguna?”

“Hata, nimeguna mwenyewe tu mama.”

“Hapana, niambie kwa nini nilipokuagizia mchemsho umeguna?”

“Mama haingiliani na wewe kuagizia mchemsho, kwani ulaji wako wa siku zote si ndiyo huohuo mama.”

“Wewe…angalia sana. Patakushinda hapa nyumbani.”

Kuanzia hapo sikuwa na raha mpaka jioni aliporudi baba Rehema…

“Shikamoo baba,” alisalimia Rehema maana naye alikuwa amesharudi toka shule…

“Marahaba mwanangu…hujambo Jamila?”

“Sijambo baba shikamoo…”

“Marahaba… za hapa mama Rehema?”

“Kwa hiyo mimi ndiyo unaniweka mwishoni, unamtanguliza Jamila kwanza siyo?” mama Rehema alimjia juu mume wake mpaka aibu…

“Kwani we mama Rehema hujajua kuwa, wengi katika kusalimia wale wenye umuhimu mkubwa ndiyo wanakuwa wa mwisho? Kwa sababu najua lazima utaniuliza za kazi, utanipa pole, utanipongeza kwa kazi nzuri na utaniambia lolote la hapa nyumbani…”

“Lolote la hapa nyumbani ni huyu Jamila, ananitafuta sana. Hajui kama mimi ni bosi wake…mimi nahisi amechoka sasa, anataka kuacha kazi arudi kwao,” alinisema mama Rehema mpaka nikaanza kutetemeka.

Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

Leave A Reply