Huyu Ndiye Mchawi wa Akina Nandy
DAR: “Ni vipi naweza kunogesha furahisha na pendo likolee…
Nieleze kitu gani sijafanya au unafanya nahisi nakosea…
Ni wapi nitashika ukaridhika burudika na pendo liendee…
Maana imekuwa nongwa kisa rika unaniambia siwezi menginee…
Mapenzi ya upepo, maana bendera mama wee…
Mwenzako moto! Hauzimi hauzimi!…
Mwenzako moto! hauzimi!…
Basi slow tempo, namaliza sabuni…
Mwenzako moto! Hauzimi hauzimi!…
Mwenzako moto hauzimiii!…”
Haya ni baadhi ya mashairi na melodi tamu kutoka katika ngoma ya Hauzimi ambayo imekuwa ikafanya poa katika vyombo vya habari na kusikika katika spika za MADJ kibao kutokana na utamu wa mashairi yake.
Benson William Masinde almaarufu Benson Hauzimi, kijana mwenye kipaji na sauti ya kipekee ambayo imechanganyika na melodi tamu.
Kipaji chake kiligundulika na kukua kwenye Nyumba ya Kukuza Vipaji Tanzania (THT) chini ya marehemu Ruge Mutahaba.
Benson ambaye ametokea katika uhudumu wa baa hadi kuwa msanii mwenye kipaji cha kitofauti, kwani anakiri kuwa Ufukwe wa Escape One ndiyo njia ya yeye kufika hapo alipo.
Safari yake ilianzia hapo alipopata bahati ya kutumbuiza katika Bendi za Skylight na B-Band ya Banana Zorro.
Benson ameanza kutambulika kwa mashabiki na Wimbo wa Hauzimi aliouachia mwaka 2018 ambao umekuwa ukifanya vizuri hadi sasa katika Mtandao wa YouTube.
Nyimbo zake nyingine ni kama Naichote, Toto, Mashallah, Bwagamoyo ambazo mpaka sasa zinaendelea kufanya vizuri.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limekusogezea mkali huyu na kupiga naye stori, ambapo amefunguka mengi ikiwemo ishu nzima ya uandishi wa nyimbo za wasanii mbalimbali akitajwa kuwa ndiye mchawi wao;
IJUMAA WIKIENDA: Hauzimi ni ngoma ambayo imekuwa ikifanya vizuri mpaka sasa, je, ulitoa wapi idea hiyo?
BENSON: Idea ya Hauzimi ni historia ya maisha yangu ya kimahusiano.
IJUMAA WIKIENDA: Tayari umeshatoa ngoma zingine, je, unazungumziaje mapokeo yake?
BENSON: Kiukweli nashukuru wote wanaosapoti muziki wangu, hasa media kwani mapokeo ni mazuri na ngoma zangu zinaendelea kusikika.
IJUMAA WIKIENDA: Je, mipango yako ya kutoa kazi mpya ikoje?
BENSON: Kazi zipo na zinakuja ila kwa kipindi hiki cha Corona nimepata wasaha wa kuwa studio muda mwingi na kutengeneza kazi ambazo zitatoka.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako unaizungumziaje Corona kama msanii?
BENSON: Kiukweli imeathiri mishe nyingi sana, mikusanyiko imezuiliwa, hakuna shoo hata studio unaenda kwa sababu maalum, pesa imekuwa ngumu hata kwa wadau.
IJUMAA WIKIENDA: Utunzi na uandishi wa ngoma zako umekuwa ukiandika mwenyewe au unaandikiwa?
BENSON: Idea ni zangu na ninaandika, pia napata ushirikiano wa wasanii wenzangu kama J Melody alishiriki kuandika Ngoma ya Hauzimi. THT tuna utaratibu wa kushirikiana kuandika nyimbo. Pia nimeshiriki kuandika nyimbo kama ya Nandy Aibu, Haleluyah, Namwaga Mboga na nyingine.
IJUMAA: Uko slow sana katika kazi zako tofauti na wenzako ambao ulianza nao kwa nini?
BENSON: Mara nyingi napenda kuzipa nafasi changamoto katika kazi zangu ili nijue nakosea wapi au nimepatia ili nifanye vizuri.
IJUMAA: Unaizungumziaje THT kama sehemu iliyokulea?
BENSON: THT ni familia yangu iliyonikuza hadi kufika hapa nilipofika, imenitengenezea msingi mzuri, imetunyanyua vijana wengi na kutimiza ndoto zetu.
IJUMAA WIKIENDA: Unazungumziaje mchango wa marehemu Ruge Mutahaba katika kazi zako?
BENSON: Bosi Ruge namshukuru sana kwa moyo wake wa upendo kwangu na kunifungulia dunia, amenionesha njia iliyo sahihi, namuahidi huko aliko sitatetereka kamwe, nitazidi kufanyia kazi yote aliyonifundisha na kunielekeza. Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.
IJUMAA WIKIENDA: Wasanii wengi wamekuwa na utaratibu wa kuachia Extended Playlist (EP) au album, kwa upande wako iko vipi?
BENSON: Mashabiki wangu wategemee lolote kwa sababu mipango ipo na kazi zipo nyingi za kuweka kwenye EP, hivyo nasubiri muda sahihi upite kwa ajili ya kufanya hivyo.
IJUMAA WIKIENDA: Muziki wa sasa umekuwa na ushindani, je, kwa upande wako umejizatiti vipi?
BENSON: Kiukweli ushindani ni mkubwa, nashukuru Mungu bado niko na watu wangu wanaoniamini na kunipa nguvu kila siku, kazi nzuri ndiyo itafanya nibaki hapa nilipo na kuendelea mbele.
IJUMAA WIKIENDA: Je, kwa sasa uko katika menejimenti?
BENSON: Ndiyo, nina meneja wangu anaitwa Pappy, amekuwa ni mtu muhimu kwenye maisha yangu na kazi yangu.
IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu kolabo za ndani na nje ya Bongo, kwa upande wako iko vipi?
BENSON: Kolabo zipo maana kwa muda nimefanya kazi nyingi peke yangu, hivyo zinakuja ladha tofautitofauti na wasanii wengine.
IJUMAA WIKIENDA: Changamoto gani umepitia katika muziki wako?
BENSON: Kubwa ni kukosa mtu wa kuwekeza ili kufanya kazi kwa ukubwa kama kushuti video kali.
IJUMAA WIKIENDA: Mafanikio gani unajivunia katika muziki wako?
BENSON: Mafanikio makubwa kwa upande wangu ni kutengeneza mashabiki wengi na kukutana na watu tofauti. Nimefanikiwa kupata mahali pa kupumzika na usafiri, kwa hayo namshukuru Mungu.
MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA