Kartra

Huyu Sakho Ataua Mtu Mjue

UWEZO mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha kiungo mshambuliaji mpya wa Simba Msenegali, Pape Ousmane Sakho umewaibua makocha wa timu hiyo ambao wameweka wazi wanajivunia usajili wa nyota huyo, huku kocha Mkuu Didier Gomes akikitabiria makubwa kikosi hicho.

 

Sakho ameanza vizuri majukumu yake ndani ya Simba, ambapo juzi Jumamosi kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa maandalizi ya msimu dhidi ya FAR Rabat, aliifungia Simba bao moja kwenye mchezo ulioisha kwa sare ya mabao 2-2, huku akiwa nyota wa mchezo.

 

Nyota huyo alijiunga rasmi na Simba, Agosti 14, mwaka huu akitokea klabu ya Teungueth ya kwao Senegal, ambapo amekuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichoweka kambi nchini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘pre season’.

 

Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa kwanza kwake, aliwashangaza wengi kutokana na jinsi ambavyo alikuwa akiuchukua mpira na kuwafuata mabeki bila hofu.

 

Inaelezwa kuwa chenga zake za maudhi mara kwa mara ziliwalaza wapinzani chini ambapo alifanikiwa kuwaangusha wachezaji wa Rabbat mara mbili kutokana na chenga za maudhi.

 

Bao lake lilitajwa kuwa bora sana ambapo hadi kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandebroeck alijikuta akishangilia kutokana na ubora wake.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha wa viungo wa Simba, Adel Zrane alisema: “Nimekuwa na nafasi ya kuwafuatilia wachezaji wote ili kuhakikisha wanakuwa na utimamu tosha wa mwili, hivyo namfahamu Sakho vizuri ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vikubwa ambao kama ataendelea kucheza katika kiwango hiki basi tutarajie makubwa.”

 

Naye kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes akizungumzia kikosi chake mara baada ya mchezo wa Jumamosi alisema: “Tumepata nafasi nzuri ya kujipima ni wazi tunapaswa kuendelea kuimarika zaidi ya hapa, naamini kikosi hiki kinaweza kufanya vizuri zaidi kuliko kile cha msimu uliopita.

 

“Tunapaswa kuwa wavumilivu, katika kipindi cha maandalizi tulichonacho na nina uhakika tutakuwa tofauti kabisa.”

Joel Thomas, Dar es Salaam


Toa comment