Huzuni Yatanda Watu 22 wa Familia Moja Waliokufa Kwa Moto Harusini Wakizikwa
Watu 22 wa familia moja waliopoteza maisha baada ya ukumbi waliokuwa wakifanyia shehere ya harusi kuteketea kwa moto nchini Iraq, wamezikwa huku huzuni na majonzi vikitawala katika tukio hilo lililogusa hisia za wengi duniani kote.
“Huyu ni dada yangu, huyu ni baba yangu, huyu ni mama yangu na huyu ni dada yangu mwingine,” amekaririwa Fuad Silewa, mmoja kati ya ndugu wa familia hiyo akionesha picha za marehemu, wakati wa misa ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa la Hamdaniya, eneo linalokaliwa na Wakristo wengi.
Silewa amekaririwa akisema ndugu zake walikufa kwa kukosa hewa baada ya Ukumbi wa Haitham Royal Wedding Hall kuwaka moto wakati harusi ikiendelea, Jumanne ya wiki iliyopita.
Mamlaka nchini humo zimeeleza kuwa takribani watu 100 walipoteza maisha katika tukio hilo huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa vibaya na moto huo.